MWANZA: Wahudumu wa afya wanaotarajiwa kutoa huduma katika jengo jipya la watoto njiti lililopo Hospitali ya Wilaya ya Kwimba wamepatiwa mafunzo maalumu ya namna bora ya kutumia vifaa vya kisasa pamoja na kuwahudumia watoto hao ili kuboresha huduma kwa watoto na mama zao.

Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wahudumu hao katika utoaji wa huduma kwa watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti), kwa kuwapatia elimu ya nadharia na vitendo ili kuhakikisha wanatoa huduma kwa weledi na ufanisi mkubwa.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkuu wa Kitengo cha Watoto Wachanga katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na Daktari Bingwa Mbobezi wa Watoto Wachanga, Dk. Martha Mkony, ambaye pia ni mkufunzi wa mafunzo hayo, amesema kuwa mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka kwa hospitali hiyo ambayo ipo katika hatua za kufungua jengo maalumu la kuhudumia watoto wachanga.

“Mafunzo haya ya Mama na Mtoto yamekuja wakati sahihi kwa Hospitali ya Wilaya ya Kwimba, ambayo ipo katika maandalizi ya kuanza kutoa huduma katika jengo maalumu la watoto wachanga.

Mafunzo haya yamewahusisha watoa huduma wa Hospitali ya Wilaya ya Kwimba pamoja na watoa huduma kutoka vituo vya afya vyenye wagonjwa wengi katika wilaya za Kwimba na Misungwi,” amesema Dkt. Mkony.

Ameongeza kuwa wahudumu hao wanapatiwa mafunzo ya nadharia na vitendo ili kujifunza mbinu madhubuti za utoaji huduma kabla ya kuanza kuhudumia wagonjwa moja kwa moja.

Aidha, amepongeza juhudi za Doris Mollel Foundation kwa kuunga mkono juhudi za Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha watoto wanapata huduma bora za afya.

Kwa mujibu wa Dk Mkony, wodi hiyo mpya ni ya kwanza nchini kukidhi vigezo vya Shirika la Afya Duniani (WHO) katika utoaji wa huduma kwa watoto wachanga.

Kwa upande wake, Elizabeth Honela, mfanyakazi wa Hospitali ya Wilaya ya Kwimba na mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, amesema mafunzo hayo yamewapa uelewa mpya ikiwemo dhana ya “zero separation” kati ya mama na mtoto, inayolenga kuhakikisha mtoto anapata uangalizi wa karibu kutoka kwa mama yake hata akiwa kwenye matibabu.

“Tupo kwenye mafunzo ya utoaji huduma kwa watoto njiti. Kitu kipya kwetu ni dhana ya ‘zero separation’ kati ya mama na mtoto. Tunaamini baada ya mafunzo haya tutaimarika zaidi katika kuwahudumia watoto.

Tumepokea jengo muhimu kutoka Doris Mollel Foundation lenye vifaa vya kisasa, tofauti na hapo awali ambapo kulikuwa na changamoto zilizolazimu kuwapa wagonjwa rufaa,” amesema Elizabeth.

Mafunzo hayo yameratibiwa na Doris Mollel Foundation (DMF) kwa uwezeshaji wa Shirika la Afya Duniani (WHO), huku wauguzi walioshiriki wakitolewa na Serikali ya Tanzania.

Lengo kuu ni kuhakikisha huduma za watoto njiti katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba zinakuwa za kiwango cha juu na zinazokidhi viwango vya kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *