
UJUMBE wa kiungo raia wa Uganda, Khalid Aucho, aliouchapisha katika ukurasa wake wa Instagram kupinga tuhuma za utovu wa nidhamu na kupewa adhabu ya kusimamishwa kwa miezi mitatu, umeibua hisia na mjadala mkubwa miongoni mwa mastaa wa soka wanaocheza na waliowahi kucheza Ligi Kuu Bara.
Aucho, ambaye ni mchezaji wa Singida Black Stars, amesimamishwa pamoja na kipa Amas Obasogie anayesubiri uchunguzi wa tuhuma zinazohusiana na upangaji wa matokeo.
Kupitia ujumbe wake, Aucho amesisitiza kuwa katika maisha yake yote ya soka amekuwa akijituma kwa weledi na heshima kubwa kwa kila klabu aliyowahi kuitumikia, akieleza kuwa hajawahi kuhusishwa na tukio lolote la utovu wa nidhamu.
Aidha, amewashukuru mashabiki wake kwa kuendelea kumuunga mkono, akiamini kuwa hali hiyo itapita.
Baadhi ya mastaa waliompa sapoti hadharani ni pamoja na Clatous Chama aliyeandika: “Be at peace this too shall pass brother 🫂 @auchokhalidofficial.” akiwa na maana kwamba “Kuwa na amani hili nalo litapita kaka.”
Naye Saido Ntibazonkiza aliweka alama za kuonesha kumtia moyo, huku Skudu Makudubela akiandika: “A true leader with high morals 🙌👏❤️.” Maana yake ni “kiongozi wa kweli mwenye maadili ya hali ya juu.”
Aidha, aliyewahi kuwa msemaji wa klabu za Simba na Yanga, Haji Manara, naye alitoa maoni yake kwa kuandika: “Timu ndo haina nidhamu😢”.
Mwitikio huo wa mastaa mbalimbali umeongeza uzito wa mjadala kuhusu sakata hilo, huku wadau wa soka wakisubiri hatima ya Aucho ndani ya klabu hiyo na matokeo ya maamuzi yaliyotangazwa.