KATIKA mechi zenye ushindani na msisimko mkubwa zinazoteka hisia za wengi hapa nchini, ile inayozikutanisha Yanga na Simba inashika namba moja.

Zinapokutana timu hizo si Tanzania pekee, bali nje ya mipaka ya nchi pia inafuatiliwa ndio maana katika Dabi bora Afrika, yenyewe inashika nafasi ya nne kwa msisimko zaidi baada ya Cairo Derby (Al Ahly vs Zamalek nchini Misri), Casablanca Derby (Raja Casablanca vs Wydad Athletic nchini Morocco) na Soweto Derby (Kaizer Chiefs vs Orlando Pirates nchini Afrika Kusini).

Dabi ya Kariakoo inayochezwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja ikiwa ni mechi ya Ligi Kuu Bara na litachezeshwa na mwamuzi Nassoro Mwinchui kutoka Tanga akisaidiwa na Kassim Mpanga (Dar) na Hamdan Said (Mtwara) huku Ramadhan Kayoko atakuwa mezani na Mtathimini wa Waamuzi ni mkongwe ni Israel Mjuni Nkongo (Dar).

Pambano hilo la kwanza la Ligi Kuu Bara kwa msimu huu na la kwanza kwa vigogo kukutana huko kwa mechi ya Ligi Kuu, japo kimahesabu ni la saba kwa michuano yote kupigwa Amaan tangu 1975.

Ndio, Simba na Yanga zilishakutana mara sita katika mechi za michuano ya Kombe la Mapinduzi, Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kagame Cup) na Ligi Kuu ya Muungano, ambapo katika mechi hizo Yanga imeshinda mbili tu na Simba mara nne ikiwamo ya Kagame, Ligi Kuu ya Muungano na mbili za Kombe la Mapinduzi fainali yaa 2011 na nusu fainali ya mwaka 2017.

Kama zilivyo mechi za dabi, pambano la kesho linatazamiwa kuwa na ushindani kama kawaida.

Uwekezaji wa mabosi wa timu hizo, umezidisha utamu wa Dabi ya Kariakoo ambayo itakuwa ya 115 katika Ligi Kuu Bara, huku Yanga ikiingia na ubabe wake kufuatia kushinda mechi nne mfululizo za mwisho kwenye ligi hiyo dhidi ya Simba.

Mbali na hilo, Yanga pia inashikilia rekodi ya kuwa timu iliyocheza mechi nyingi zaidi za ligi bila kupoteza ambazo ni 30, ikishinda 28 na sare mbili.

Sasa basi, katika mechi hii, usajili uliofanyika ule wa dirisha kubwa na dogo, unaifanya kuwa Dabi ya Kishua kutokana na majembe yanayounda vikosi vya timu hizo.

Ikumbukwe kwamba, kwa kiasi kikubwa, hii ikiwa ni Dabi ya Kariakoo ya kwanza katika ligi msimu huu, makocha Pedro Goncalves wa Yanga na Steve Barker upande wa Simba wanakwenda pia kuicheza kwa mara ya kwanza tangu watue katika timu hizo.

Ile Kariakoo Dabi ya Ngao ya Jamii, Yanga ilikuwa inafundishwa na Romain Folz na kushinda bao 1-0, wakati Simba kocha ni Fadlu Davids.

KIKOSI CHA YANGA

Muonekano wa kikosi cha Yanga upo hivi; Djigui Diarra, Israel Mwenda, Mohamed Hussein, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Mohamed Damaro, Maxi Nzengeli, Duke Abuya, Pacome Zouzoua, Laurindo Depu na Allan Okello. Kikosi hicho, thamani yake ni euro 2,875,000 (Sh8.6 bilioni) kwa mujibu wa Transfermarket.

Mchanganuo wa thamani ya kikosi cha Yanga kwa mujibu wa Transfermarket upo namna hii; Djigui Diarra – Euro 400,000 (Sh1.2 bilioni), Israel Mwenda – Euro 75,000 (Sh225.3 milioni), Mohamed Hussein – Euro 250,000 (Sh751 milioni), Dickson Job – Euro 200,000 (Sh600.8 milioni), Ibrahim Bacca – Euro 300,000 (Sh901.2 milioni), Mohamed Damaro – Euro 50,000 (Sh150.2 milioni), Maxi Nzengeli – Euro 400,000 (Sh1.2 bilioni), Duke Abuya – Euro 50,000 (Sh150.2 milioni), Pacome Zouzoua – Euro 450,000 (Sh1.4 bilioni), Allan Okello – Euro 500,000 (Sh1.5 bilioni) na Laurindo Depu – Euro 200,000 (Sh600.8 milioni).

Hapo ni mbali na wachezaji wa akiba ambao huenda kocha Pedro akaamua kuwapanga ili kusaka pointi tatu muhimu mbele ya wapinzani wao hao.

KIKOSI CHA SIMBA

Kwa upande wa Simba, Kocha Steve Barker mechi mbili za mwisho katika ligi dhidi ya Tanzania Prisons na Dodoma Jiji, hakufanya mabadiliko ya kikosi kilichoanza, hiyo inamaanisha hilo ndilo jeshi lake la kazi atakaoingia nalo kucheza dhidi ya Yanga.

Kikosi hicho kipo hivi; Djibril Kassali, Shomari Kapombe, Nickson Kiba bage, Rushine De Reuck, Ismael Toure, Yusuph Kagoma, Libase Gueye, Inno Loemba, Clatous Chama, An icet Oura na Seleman Mwalimu.

Kwa mujibu wa Transfermarket, kikosi hicho kina thamani ya euro 1,723,000 (Sh5.2 bilioni).

Mchanganuo wake upo hivi; Djibril Kassali – Euro 75,000 (Sh225.3 milioni), Shomari Kapombe – Euro 75,000 (Sh225.3 milioni), Nickson Kiba bage – Euro 50,000 (Sh150.2 milioni), Rushine De Reuck – Euro 650,000 (Sh2 bilioni), Ismael Toure – Euro 300,000 (Sh901.2), Yusuph Kagoma – Euro 75,000 (Sh225.3 milioni), Libase Gueye – Euro 48,000 (Sh144.2 milioni), Inno Loemba – Euro 100,000 (Sh300.4 milioni), Clatous Chama – Euro 100,000 (Sh300.4 milioni), An icet Oura – Euro 200,000 (600.9 milioni), Seleman Mwalimu – Euro 50,000 (Sh150.2 milioni).

Hapo ni mbali na nyota wanaoanzia benchi ambao wamekuwa wakitumika na Barker kuipa matokeo mazuri timu hiyo inayotafuta nafasi ya kujivua unyonge mbele ya watani wao hao, kutoka kapa bila ya ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho kwa misimu minne mfululizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *