DAR ES SALAAM: Tanzania inaendelea kupiga hatua katika kujenga uchumi unaotegemea maarifa na ubunifu, kupitia sera na mikakati mbalimbali, huku Serikali ikiweka mazingira yanayowezesha watafiti, wabunifu kukuza mawazo yao na kuyageuza kuwa suluhisho halisi kwa jamii.
Msukumo huu unalenga kuhakikisha maendeleo ya kiteknolojia yanayotokea duniani yanatumika kama fursa ya kujifunza, kubuni na kuzalisha bidhaa na huduma zinazokidhi mahitaji ya Watanzania.

Akizungumza jana Februari 27, katika Wiki ya Ubunifu ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Hussein Mohamed Omar ameeleza kuwa katika sekta ya afya, ubunifu ni jambo lisiloepukika.
Amesema idadi ya watu inaendelea kuongezeka, mifumo ya magonjwa inabadilika, na matarajio ya kupata huduma za afya zinazopatikana kwa urahisi, nafuu, na zenye ubora yanaongezeka.
“Ili kukidhi mahitaji haya kwa njia endelevu, ni lazima tuzalishe suluhisho za ndani, zana za uchunguzi, mifumo ya utoaji huduma, majukwaa ya afya ya kidijitali, teknolojia za dawa, na mikakati ya kinga iliyoendelezwa ndani ya taasisi zetu wenyewe,” amesema Dk Omar.
Amesema kuwa vyuo vikuu lazima viwe injini za ubunifu, uanzishaji wa biashara, na uhamishaji wa teknolojia huku akisifu kuona kwamba Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kinachukua jukumu hilo kwa uzito.

Dk Omar ameeleza kuwa moja ya ishara kubwa zinazoibuka kutoka Wiki ya Ubunifu ya mwaka huu ni kuongezeka kwa msisitizo juu ya ulinzi wa haki miliki na mifumo ya kibiashara akidai kuwa ni jambo la kupongezwa.
“Ili ubunifu ustawi, wabunifu lazima wawe na uhakika kwamba mawazo yao yatalindwa, mchango wao utatambuliwa, na manufaa yao yatagawanywa kwa haki. Mifumo imara ya haki miliki inahamasisha ubunifu, huvutia wawekezaji, na huwezesha vyuo vikuu kujenga mifumo endelevu ya uhamishaji wa teknolojia,” amesema Dk Omar.
Amekipongeza Chuo cha Muhas kwa kuimarisha sera na mifumo yake ya kitaasisi ili kuongoza ulinzi, umiliki, na uendelezaji wa kibiashara wa ubunifu pamoja na mwelekeo unaendana na ajenda ya Serikali ya kuendeleza sayansi, teknolojia, na ubunifu kama vichocheo vya ujenzi wa viwanda na ushindani wa kiuchumi.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Appolinary Kamuhabwa amesema kuwa baadhi ya bunifu za chuo hicho tayari zimeingia sokoni na kuleta matokeo halisi. Hii ni pamoja na Afya Lead, Pona Health, May Care, na Saratani AI, zote zimeonesha suluhisho.
Amesema hatua hiyo inaonesha ubunifu unaotokana na vyuo vikuu unaweza kusonga mbele zaidi ya mifano ya awali na kuingia katika matumizi halisi, kuboresha utoaji wa huduma za afya na kuongeza thamani ya kiuchumi.
“Katika wiki hii, tumeshuhudia maonesho ya mifano ya awali na teknolojia zinazoibukia, mijadala kuhusu ulinzi wa haki miliki, vikao vya utayari wa kibiashara, majadiliano ya ufadhili, ushirikishwaji wa walezi, na uunganishaji wa kimkakati kati ya wabunifu na wawekezaji.

Hii inaakisi uelewa wa wazi wa ubunifu kama mnyororo unaoanzia uzalishaji wa wazo na uthibitishaji hadi ulinzi, upanuzi, na kupokelewa sokoni, mtazamo wa mfumo wa ikolojia ambao Tanzania inauhitaji ili kutafsiri utafiti kuwa athari endelevu za kijamii na kiuchumi,” amesema Prof . Kamuhabwa.
Aidha, Prof. Kamuhabwa amesema MUHAS itaendelea kuimarisha juhudi za kuhamasisha rasilimali ili kudumisha na kukuza ajenda ya ubunifu, kwa kushirikiana na wadau kikamilifu ili kusaidia dhamira yao.

Amesema kuanzia mwaka huu na kwa miaka minne ijayo, MUHAS itatenga Sh milioni 35 kila mwaka kusaidia moja kwa moja wabunifu na kuimarisha mnyororo wa ubunifu.
“Pia tunatoa shukrani zetu za dhati kwa CRDB Foundation kwa kutoa mkono wa ushirikiano kusaidia juhudi za ubunifu wa afya za MUHAS,” amesema.
Sambamba na hilo, MUHAS imesaini hati ya makubaliano na CRDB yenye lengo la kuimarisha mfumo wa ikolojia wa ubunifu, ikiwemo njia za ufadhili na msaada wa kujenga uwezo.
“Ushirikiano wa aina hii ni muhimu katika kuhakikisha kwamba ubunifu hauendelezwi tu bali pia unadumishwa na kupanuliwa,” amesema Prof. Kamuhabwa.