
KIGOMA: TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kigoma imesema mpango wa taasisi hiyo kusikiliza kero za wananchi maarufu kama ‘TAKUKURU RAFIKI’ umefanikisha ujenzi wa zahanati kijiji cha Kabare kilichopo Wilaya ya Kakonko mkoani humo.
Mkuu wa taassi hiyo mkoani humo, Asha Kwariko akitoa taarifa ya utendaji wa taasisi hiyo kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba 2025, alisema wananchi wa kijiji hicho hawakuwa na zahanati ,hivyo wakati wa Program ya TAKUKURU RAFIKI wananchi hao walitoa malalamiko ya changamoto wanayopata kwa kutokuwa na zahanati hivyo kufuata huduma za afya umbali mrefu.

Kutokana na hali hiyo, mkuu huyo wa TAKUKURU Kigoma alisema kuwa ndipo lilipojitokeza Shirika la World Vision ambalo lilikubali kutoa kiasi cha Sh milioni 246 ambapo zahanati hiyo ilijengwa na kuanza kutoa huduma na kwa sasa wananchi wanashukuru kwa kutatuliwa kwa changamoto hiyo.
Akielezea kuhusu usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa mkoani humo Kwariko alisema kuwa wamefanikiwa kusimamia thamani ya fedha kwenye miradi 27 yenye thamani ya Sh bilioni 7.1 ambapo baadhi ya miradi ilikiuka mikataba na kununua vifaa ambavyo havikuwa na ubora.
