
Aliyeanza kuzungumza baada ya kukaribishwa na Rais wa Baraza la Umoja wa Mataifa ni Bwana Guterres ambaye amaesema uhamaji wa binadamu ni sifa kuu ya dunia ya kisasa lakini mara nyingi hukabiliwa na hofu na migawanyiko badala ya suluhisho za pamoja. Ameonya kuwa sera zinazozuia njia halali zinawalazimisha wahamiaji kutumia njia hatari ambako hukumbana na unyonyaji, ukatili na vifo mikononi mwa mitandao ya kihalifu ya magendo na biashara haramu ya watu. Amesisitiza kuwa wahamiaji si wahalifu, akitaka juhudi za kimataifa kuimarishwa ili kuvunja mitandao hiyo na kupanua njia salama na halali za uhamiaji.
Ripoti kuhusu Mkataba wa Kimataifa wa Uhamiaji Salama, Wenye Utaratibu na Halali inaonesha kuwa ingawa baadhi ya nchi zimepanua njia za kisheria za uhamiaji, zimeimarisha mipango ya uhamaji wa ajira na kuboresha mifumo ya utafutaji na uokoaji, maendeleo kwa ujumla hayatoshi kukidhi mahitaji ya sasa. Serikali, miji na mashirika ya kiraia zimetambuliwa kwa juhudi bunifu, lakini Katibu Mkuu amesisitiza kuwa hakuna taifa linaloweza kusimamia uhamiaji peke yake, hasa wakati mabadiliko ya tabianchi, mabadiliko ya idadi ya watu na mageuzi ya kiuchumi yanabadilisha mienendo ya uhamaji duniani.
IOM
Kwa upande wa Amy Pope amesema mijadala kuhusu uhamiaji mara nyingi huzingatia mipaka na uhamiaji usio wa kawaida pekee, na hivyo kuficha ukweli mpana kwamba uhamiaji unaweza kuleta manufaa makubwa ikiwa utasimamiwa vizuri. Amebainisha kuwa wahamiaji huziba pengo la ajira muhimu, huanzisha biashara na kutuma fedha zinazosaidia familia na jamii kote duniani. Pia amesisitiza umuhimu wa nchi kushirikiana katika njia za uhamiaji, kubadilishana taarifa na kuunda sera zinazoratibiwa ili kulinda maisha na kuongeza manufaa ya uhamaji.
Viongozi hao wamezihimiza nchi kutumia mkutano ujao wa mapitio utakaofanyika New York, Marekani kama fursa ya kutoa ahadi madhubuti, kuimarisha ushirikiano na kuwekeza katika ubia wa vitendo kupitia Mtandao wa Umoja wa Mataifa wa Uhamiaji. Wametoa wito kwa sera zitakazojengwa juu ya ushahidi, haki za binadamu na uwajibikaji wa pamoja, wakisisitiza kuwa swali kuu si kama uhamiaji utaendelea, bali ni kama mataifa yatachagua kuuelekeza kwa pamoja kupitia ushirikiano badala ya hatua za upande mmoja.
Miongoni mwa wengine aliyezungumza ni Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambaye katika kuonesha umuhimu wa uhamiaji ametoa mfano wa mchezaji wa mpira wa miguukutoka Argentina, Lionel Messi ambaye alihamia Hispania kucheza mpira na hata Ufaransa na Marekani.