KOCHA mpya wa Transit Camp, Vicent Barnabas amesema ataendelea kusimamia malengo ya timu hiyo ya kuhakikisha inapanda Ligi Kuu Bara msimu huu, licha ya ushindani mkubwa uliopo katika Ligi ya Championship, hususani mechi hizi za mwishoni.

Akizungumza na Mwanaspoti, Barnabas, amesemalicha ya kukabidhiwa majukumu hayo makubwa, ila jambo analojivunia ni kukaa na timu hiyo kwa zaidi ya mwezi mmoja, hivyo, haitakuwa shida kwake kwa sababu anajua falsafa za kikosi hicho msimu huu.

“Ni furaha kwangu kuona nimeaminiwa na kupewa majukumu haya makubwa na mazito, natambua kiu kubwa ni kuona timu inapanda daraja na kwenda kushiriki Ligi Kuu, sio kazi rahisi, ila naamini kwa ushirikiano tutafikia malengo,” amesemaBarnabas.

Awali, Barnabas alikuwa ni kocha msaidizi, ingawa amepewa majukumu hayo baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’, kuondoka na kwenda kujiunga na maafande wa Tanzania Prisons, akichukua nafasi ya Mkenya Zedekiah ‘Zico’ Otieno.

Barnabas ni miongoni mwa makocha wenye rekodi za kuvutia katika soka la Tanzania, ambapo aliipa timu ya vijana ya Mtibwa Sugar chini ya miaka 20, mataji matano mfululizo, kuanzia mwaka 2018 hadi 2022, baada ya kuichezea pia kwa mafanikio.

Kabla ya kujiunga na kikosi hicho cha maafande wa Transit Camp, msimu uliopita wa 2024-2025, Barnabas aliipa pia ubingwa timu ya Yanga chini ya miaka 17, baada ya kuachana na Mtibwa Sugar, akiendeleza rekodi bora kwa kila timu anayofundisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *