Katika taarifa iliyotolewa mjini Geneva, UNHCR imesema kuwa nchi nyingi zilizoathiriwa tayari zinahifadhi mamilioni ya wakimbizi na watu waliokimbia makazi yao ndani ya nchi zao . 

Shirika hilo limeonya kuwa kuongezeka kwa vurugu kunaweza kuzidi uwezo wa mashirika ya kibinadamu na kuongeza shinikizo kwa jamii zinazowapokea wakimbizi.

“Vurugu zaidi zina hatari ya kuzidi uwezo wa mashirika ya kibinadamu na kuweka shinikizo la ziada kwa jamii zinazowahifadhi wakimbizi,” imesema taarifa hiyo, ikisisitiza mzigo unaoongezeka kwa huduma za kijamii, miundombinu na mifumo ya ulinzi katika nchi ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikitoa hifadhi kwa watu wanaokimbia migogoro.

Mashariki ya Kati ina idadi kubwa ya wakimbizi

Kwa mujibu wa UNHCR eneo la Mashariki ya Kati linaendelea kuwa miongoni mwa maeneo yenye idadi kubwa ya watu waliolazimika kuhama duniani, huku migogoro ya muda mrefu ikiendelea kuvuruga maisha na kipato cha familia nyingi. 

Mashirika ya kibinadamu yamekuwa yakionya mara kwa mara kuhusu upungufu wa rasilimali na changamoto za kufikia wahitaji, hali inayopunguza uwezo wa kutoa msaada unaohitajika.

UNHCR pia imeunga mkono wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kutaka mazungumzo ya haraka na kupunguza mvutano, ikisisitiza umuhimu wa kuheshimu haki za binadamu, kulinda raia na kuzingatia kikamilifu sheria za kimataifa.

Shirika hilo limesisitiza kuwa kulinda maisha ya raia kunapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza, na limethibitisha tena dhamira yake ya kuendelea kusaidia watu waliolazimika kuhama katika eneo hilo, huku likitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuimarisha msaada wa kibinadamu na juhudi za kidiplomasia ili kuzuia mateso zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *