Video inatupeleka kando ya bandari ya jiji la Gaza, watoto wanajaribu kutengeneza nafasi ndogo za kuchezea katikati ya mahema yaliyosongamana ya familia zilizokimbia makazi yao, kando ni magofu ya nyumba zilizobomolewa.
Kinachowazunguka hapa ni mabaki ya kuta za zege zilizoporomoka, baadhi yao wanacheza juu ya magofu, huku, milio ya ndege zisizo na rubani za upelelezi zikisikika mfululizo, jambo linalotengeneza taswira ya ukuaji wao na kumbukumbu za vita kwa siku zijazo.
Mmoja wao ni Qassem Adwan, aliyekimbia kambi ya wakimbizi ya Jabalia ambaye anasema..“nilikuwa na furaha kabla ya vita. Sasa hakuna kitu kizuri hapa, na sina furaha.”
Hofu kuhusu kesho inaendelea kutawala mioyo ya watoto hawa, Amal Suhweil, aliyekimbia kutoka Beit Hanoun, ameeleza.
“Ninaona kuwa maisha ya baadaye hapa Gaza hayajulikani. Maisha yetu katika nyumba zetu yalikuwa mazuri zaidi; tulizoea kucheza ndani ya nyumba zetu, siyo barabarani kama sasa. Tunacheza barabarani, na tumeunguzwa na jua na kuloeshwa na mvua. Maisha hapa ni magumu sana.”
Wasichana wawili wa Palestina wanacheza katikati ya uharibifu katika mji wa Gaza
Hali ya kukata tamaa pia imejitokeza kwa baadhi ya watoto, ambapo Mohannad Saadat, aliyekimbia kutoka Beit Hanoun, amesema, “Maisha yetu ya baadaye… hakuna maisha ya baadaye. Sioni maisha yoyote ya baadaye. Uharibifu huu wote uliotokea Gaza, na hakuna aliyesimama nasi. Kiwango cha uharibifu ni kikubwa. Hakuna shule, hakuna hospitali, hakuna magari ya wagonjwa, na hakuna elimu pia.”
Nihad Jundiya, aliyekimbia kutoka mtaa wa Shujaiya upande wa mashariki wa Gaza amekumbuka vitu vyake vya nyumbani.
“Kila ninapotoka nje, ninaona nyumba zimeporomoka, barabara zimeharibiwa, na vifusi kila mahali. Natamani ningeweza kwenda kwenye vifusi vya nyumba yetu na kuchukua vitu vyetu vingi kutoka hapo.”
Wakati watoto wengine wakikimbia peku juu ya mchanga na vifusi, Mena Qaddoura, aliyekimbia kutoka Jabalia, ametoa wito kwa dunia.
“Nazitaka nchi za dunia kutusaidia kupata nyumba zinazohamishika, kujenga upya nyumba zetu, na kuondoa hivi vifusi vyote. Sasa panya wameongezeka katika uchafu. Natamani tungekuwa na nyumba. Je, inakubalika kwa baadhi ya watu kuishi katika nyumba wakati wengine wanaishi katika mahema wakipigwa jua? Hicho ndicho kitu pekee ninachotamani.”
Uharibifu huu wa makazi na miundombinu umewaacha watoto wa Gaza bila matumaini ya wazi ya elimu au afya, huku mazingira yao ya kila siku yakitawaliwa na magofu na kelele za kijeshi. Licha ya jitihada zao za kutafuta furaha kupitia michezo, ukweli wa maisha magumu katika mahema na barabarani unaendelea kuathiri ukuaji wao na mtazamo wao juu ya nchi yao.