
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewakuta na kesi ya kujibu wakazi watatu wa Majohe wanaokabiliwa na kesi ya kuchoma moto jengo la Chama cha Mapinduzi (CCM) Kivule, hivyo wanatakiwa kujitetea Machi 5, 2026.
Uamuzi huo umetolewa leo Jumatatu, Machi 2, 2026, na Hakimu Mkazi Mkuu, Rahim Mushi, baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao.
Washtakiwa katika kesi hiyo ya jinai namba 28997 ya mwaka 2025 ni Mohamed Madea (28), maarufu Teacher, Fredy Chacha (21), maarufu Chank na Peter Chobe (49).
Washtakiwa wanakabiliwa na kosa moja la kuchoma jengo la CCM, kinyume na kifungu 319(a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Hakimu Mushi amesema amepitia ushahidi wa mashahidi watano wa upande wa jamhuri na hivyo kuwakuta washtakiwa wote watatu wana kesi ya kujibu.
“Baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi watano wa upande wa mashtaka, mahakama imewakuta na kesi ya kujibu, hivyo mnatakiwa kuanza kujitetea Machi 5, 2026,” amesema Hakimu Mushi.
Awali, kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kuendelea na ushahidi, lakini upande wa mashtaka ulidai hawana shahidi, hivyo walimuomba mahakama kufunga ushahidi.
Kutokana na ombi hilo, mahakama ilipoitwa ushahidi wa mashahidi wote na kisha kuwakuta na kesi ya kujibu, wataanza kujitetea Machi 5.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Novemba 5, 2025, wakikabiliwa na kesi mbili za uhaini, na Desemba 23, 2025, walifunguliwa kesi nyingine ya kuchoma moto jengo la CCM.
Miongoni mwa mashahidi wa jamhuri waliyetoa ushahidi dhidi ya kesi hiyo ni Mkaguzi wa Polisi mwenye namba PF 20122, Jafari Nguli, ambaye amedai chanzo cha moto ulioungua na kuteketeza jengo la CCM Kivule, lililopo Kata ya Majohe, Wilaya ya Ilala.
Nguli alikuwa mpelelezi mkuu katika kesi hiyo na amedai kuwa upelelezi wake ulibaini chanzo cha kuchoma jengo hilo kilitokana na vurugu zilizofanywa na watuhumiwa, ambao pia walikiri kosa lao kwa polisi.
Vilevile, ripoti ya wataalamu kutoka Kikosi cha Zima Moto na Uokoaji ilieleza kuwa washtakiwa hao walichoma moto jengo hilo kwa makusudi kwa kutumia mafuta ya petroli, si ajali ya moto ya kawaida, kama ilivyoelezwa awali.
Nguli, aliyekuwa shahidi wa nne wa jamhuri, amedai Oktoba 30, 2025, saa mbili asubuhi akiwa kituo cha Polisi Stakishari, aliitwa na mkuu wake wa kazi, SP Abugast Kilulumo, ambaye ni Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Polisi Ukonga, na kupewa jalada lenye kumbukumbu namba STS/IR/7518/2025 kwa ajili ya uchunguzi.
“Baada ya kupewa jalada hilo, nililisoma na kubaini kuwa lilihusisha watuhumiwa watatu– Peter Masote, Mohamed Steven na Frank Samson,” amedai Nguli, ambaye ana uzoefu wa miaka 18 katika Jeshi la Polisi, huku katika kitengo cha upelelezi akiwa na uzoefu wa miaka tisa.
Amedai kuwa alibaini watuhumiwa walikuwa wamehojiwa na maelezo yao kuchukuliwa muda mfupi baada ya kufika kituo cha polisi Stakishari.
“Baada ya kugundua wamehojiwa, nilibaini kuwa washtakiwa walikiri maelezo yao ya onyo ya kutenda kosa la kuchoma moto ofisi ya CCM Kivule, iliyopo eneo la Bwera,” amedai.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kulitenda kosa hilo Oktoba 30, 2025, usiku, katika eneo la Bwera, Kivule, Kata ya Majohe, ambapo walichoma moto jengo la CCM Kivule.