Azam FC imeshindwa kufurukuta ugenini baada ya leo, Jumatatu, Machi 2, 2026 kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Pamba Jiji katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Katika mchezo huo ambao Pamba Jiji walionekana kutawala kwa muda mrefu, Azam walilazimika kusubiri hadi kipindi cha pili kusawazisha baada ya wenyeji wao Pamba Jiji kutangulia kwa mabao mawili.
Bao la kwanza la Pamba Jiji lilikuwa la kujifunga la Himid Mao katika dakika ya 44 alipokuwa akijaribu kuokoa mpira wa faulo wa Hassan Kibailo.
Bao hilo lilidumu hadi Refa Saady Mrope alipouliza filimbi ya kuashiria muda wa mapumziko.
Dakika mbili baada ya kipindi cha pili kuanza, John Nakibinge aliipatia Pamba Jiji bao la pili kwa shuti kali la mguu wa kulia baada ya walinzi wa Azam FC kushindwa kuokoa mpira kwenye eneo lao la hatari.
Pamba Jiji FC na Azam FC zimetoshana nguvu baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza. Picha na Pamba Jiji FC.
Dakika ya 55, Azam ilipata bao la kwanza kupitia kwa Jean Jacques Ngita aliyemaliza kwa kichwa mpira uliopanguliwa na kipa Yona Amos wa Pamba Jiji.
Bao hilo liliwarudisha Azam FC mchezoni na walionekana kubadilika kwa kupeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa Pamba Jiji, na juhudi zao zikazaa matunda, dakika tatu baadaye, ilipopata bao la kusawazisha kupitia kwa Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyefunga kwa mkwaju wa penalti ambayo walipata baada ya Jean Ngita kufanyiwa faulo na Abdulmajid Mangalo katika eneo la hatari la Pamba Jiji.
Katika dakika ya 63, Fei Toto alionyeshwa kadi nyekundu na Refa Mrope baada ya kumcheza faulo, Hassan Kibailo.
Sare hiyo imeifanya Pamba Jiji kubakia nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikifikisa pointi 24 huku Azam FC ikibaki katika nafasi ya tano na pointi 23.
Kwingineko katika Uwanja wa Airtel, mkoani Singida, wenyeji Singida Black Stars waliutumia vyema Uwanja huo ambao jana wameutumia kwa mara ya kwanza kwenye Ligi Kuu baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ya Coastal Union.
Bao pekee la Singida Black Stars limefungwa katika dakika ya 77 na Joseph Guede.
Ushindi wa leo umeifanya Singida Black Stars kupanda hadi katika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi ikifikisha pointi 19.