Marekani, ambayo inashikilia urais wa mzunguko kwa mwezi Machi, imeamua kumfanya Mke wa Rais Melania Trump kuongoza mkutano huo. Kwa kawaida, balozi mwakilishi wan chi katika Umoja wa Mataifa au afisa mwandamizi wa nchi inayoshikilia urais ndiye huongoza kikao. Ingawa kumekuwa na matukio ambapo wake wa marais wameshiriki katika mikutano ya Baraza la Usalama, leo ni mara ya kwanza kwa Mke wa Rais kuongoza.

Akifungua kikao hicho kama Rais wa Baraza kwa mwezi Machi, Melania Trump, Mke wa Rais wa Marekani, amesisitiza umuhimu wa elimu katika kufikia amani ya kudumu.

“Amani ya kudumu itapatikana pale maarifa na uelewa vitakapothaminiwa kikamilifu katika jamii zote,” amesema, akibainisha kuwa mataifa yanayolinda elimu pia yanalinda mustakabali wao. Amewahimiza wajumbe wa Baraza kulinda elimu na kupanua upatikanaji wa teknolojia, ikiwemo akili mnemba (AI), ili watoto popote walipo hata katika maeneo ya mbali  waweze kupata maarifa.

 

Idadi ya watoto walioathiriwa na vita yafikia kiwango cha juu

Baraza limepokea tathmini nzito kutoka kwa Rosemary DiCarlo, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Kisiasa na Ujenzi wa Amani, ambaye ameonya kuwa dunia inashuhudia idadi kubwa zaidi ya migogoro inayotumia silaha tangu Vita Vikuu Vya Pili Vya Dunia.

“Vita vinapozuka, watoto huwa miongoni mwa waathirika wakubwa zaidi,” amesema.

Rosemary DiCarlo, Naibu Katibu Mkuu wa Katibu Mkuu wa Mambo ya Siasa na Ujenzi wa Amani, akizungumza katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu watoto, teknolojia, na elimu katika maeneo ya migogoro.

Umoja wa Mataifa

Kote duniani, mtoto mmoja kati ya watano anaishi au anakimbia eneo la migogoro  jumla ya watoto milioni 473. Amerejelea kufungwa kwa shule katika baadhi ya maeneo ya Mashariki ya Kati kutokana na operesheni za kijeshi, na pia taarifa kutoka Iran kuhusu vifo vya “huenda watoto kadhaa” kufuatia shambulio lililolenga shule ya msingi huko Minab.

Shule lazima ziwe mahali salama

Wajumbe kadhaa wamesisitiza kuwa shule lazima zibaki kuwa sehemu salama.

Mwakilishi wa Somalia ameonya kuwa mashambulizi dhidi ya taasisi za elimu yanawanyima watoto haki yao ya kujifunza na kuondoa matumaini na uthabiti wa jamii. Ametoa wito wa kuimarishwa kwa utekelezaji wa sheria za kimataifa na kuhakikisha shule, walimu na wanafunzi wanalindwa wakati wote.

Akitoa mfano wa Gaza, amesema zaidi ya asilimia 97 ya shule zimeharibiwa au kubomolewa, huku nyingi zikihitaji kujengwa upya kabisa au kufanyiwa ukarabati mkubwa ili ziweze kufanya kazi tena.

Katika enzi ya kidijitali, ameongeza kuwa kupanua upatikanaji wa AI na roboti pekee haitoshi. “Ni lazima tuongoze maendeleo haya kwa uwajibikaji,” amesema, akihimiza juhudi za kuziba pengo la kidijitali kupitia suluhisho bunifu na yanayozingatia mazingira husika, hasa kwa watoto katika maeneo ya migogoro wanaokosa vifaa, umeme au mtandao wa intaneti.

media:entermedia_image:45e12c08-8feb-4172-b83a-000a3c382b10

© UNICEF/Marko Kokic

Msichana amesimama katika darasa kaskazini mashariki mwa Nigeria ambalo liliharibiwa na waasi.

Wasichana wako hatarini zaidi

Mwakilishi wa Uingereza amebainisha kuwa wasichana katika mazingira ya migogoro wana uwezekano mkubwa wa kukosa shule kuliko wavulana, jambo linalowaweka katika hatari kubwa zaidi ya unyonyaji, ndoa za utotoni, usafirishaji haramu wa binadamu na ukatili wa kijinsia.

Ameeleza kuwa nchi yake inaunga mkono elimu ya wasichana katika nyakati za dharura kupitia Mfuko wa Education Cannot Wait, yaani Elimu Haiwezi Kusubiri ambao umewasaidia zaidi ya wasichana milioni saba, na kutoa wito kwa sekta binafsi kushirikiana na serikali na asasi za kiraia kuhakikisha teknolojia inakidhi mahitaji maalum ya wasichana.

Elimu kama msingi wa kupona baada ya vita

Mwakilishi wa Liberia ametumia uzoefu wa nchi yake baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu miaka 14, akisisitiza kuwa njia ya kupona baada ya vita “hupitia darasani”.

“Elimu inapoporomoka wakati wa vita, vita vyenyewe haviishi  hubadilika tu sura,” amesema, akikumbusha jinsi watoto walivyoandikishwa vitani kabla hata hawajajua kusoma na walimu kutawanyika.

Ameeleza jinsi redio za jamii zilivyotoa masomo wakati shule za ana kwa ana hazikuwa salama, akionesha thamani ya teknolojia. Leo, amesema, nchi za Afrika zinatengeneza mifumo inayotumia intaneti kidogo, nishati ya sola na mbinu za ujifunzaji zinazoendeshwa na jamii kulingana na mazingira yao.

“Tukishindwa watoto katika migogoro leo, kesho tutakuwa tunajadili migogoro yao,” ameonya.

Teknolojia ni nyenzo, si mbadala wa walimu

Mwakilishi wa Panama ameonya kuwa ingawa teknolojia imekuwa “mwokozi” wakati wa dharura, haiwezi na haipaswi kuchukua nafasi ya elimu ya ana kwa ana. Amesisitiza umuhimu wa mifumo madhubuti ya maadili katika ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi na kuonya dhidi ya kupanua pengo la kidijitali.

Amehimiza kuwa kuwaunganisha watoto na masomo kunapunguza uwezekano wa kujiunga na makundi yenye silaha au kukumbwa na unyonyaji.

Mwakilishi wa Ufaransa ameeleza wasiwasi kuhusu matumizi mabaya ya teknolojia mpya katika migogoro, akitaja matumizi ya droni na athari zake kwa watoto, hususan nchini Ukraine. Ameshukuru uongozi wa Mke wa Rais wa Marekani katika juhudi za kusaidia kurejesha watoto wa Ukraine waliokuwa wamehamishwa kwa nguvu.

Denmark na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pia zimetaka uwekezaji zaidi katika upatikanaji wa teknolojia ya kidijitali, uwajibikaji kwa ukiukwaji mkubwa dhidi ya watoto na kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa.

Wito wa kuchukua hatua

Akihitimisha, Mke wa Rais amewahimiza wajumbe wa Baraza kuahidi kulinda ujifunzaji na kukuza upatikanaji wa elimu bora kwa watoto wote.

“Njia ya kuelekea amani inategemea uwajibikaji wetu katika kuwawezesha watoto kupitia elimu na teknolojia,” amesema, akitoa wito wa kujenga kizazi kijacho cha viongozi watakaokumbatia amani kupitia elimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *