Musoma. Wajasiriamali wadogo wa saluni za kike na kiume zaidi ya 60 wamepewa vifaa vya kazi kwa ajili ya kuboresha shughuli zao huku wakitakiwa kurasimisha biashara hizo ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea, endapo hawatafanya hivyo.
Msaada huo wa mashine za kukaushia nywele, za kunyolea, majaketi, sabuni na spiriti,umetolewa na Mbunge wa Viti Maalumu, Agnes Marwa.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo mjini Musoma leo Jumanne Machi 3, 2026 mbunge huyo amesema ametoa vifaa hivyo ili kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuimarisha shughuli za wananchi, hususan wale wa makundi yasiyokuwa rasmi.
Amesema wafanyabiashara wasio rasmi wana mchango mkubwa katika uchumi wa kaya, jamii na taifa kwa ujumla, hivyo ipo haja ya wadau mbali kuungana na Serikali katika kuwasaidia ili waweze kuboresha shughuli zao.
“Mimi mwenyewe nimetokea huku, nilikuwa muuza dagaa, nimeuza mahindi hivyo najua changamoto za sekta hii na nimeamua kuwa nitawafikia wote, kwa leo nimeamua kutumia sehemu ya mshahara wangu wa Februari kusaidia kuboresha shughuli zao,” amesema.
Amesema msaada huo hauna itikadi ya chama chochote cha siasa, anautoa kwa lengo la kuboresha shughuli za wajasiriamali wlote kwa maelezo kuwa maendeleo hayana chama bali ni suala la jamii nzima.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Agnes Marwa akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi vifaa vya kazi kwa baadhi ya wamiliki wa saluni za kike na kiume mjini Musoma. Picha na Beldina Nyakeke
Mbunge huyo amesema licha ya kuwepo kwa mikopo isiyo na riba, baadhi ya wajasiriamali bado wanashindwa kuipata kutokana na changamoto za kijamii, hivyo hawapaswi kuachwa nyuma katika maendeleo.
Akizungumza na wajasiriamali hao, Ofisa Biashara wa Manispaa ya Musoma, Charles Sayungu amewataka kuhakikisha wanarasimisha shughuli zao ili waweze kutambuliwa na kuunganishwa na fursa mbalimbali.
Amesema urasimishaji wa shughuli zao unahusisha kukata leseni na kulipa ada ya Baraza la Sanaa Tanzania (Basata).
“Kwa Sh40,000 unapata leseni yako huku ada ya Basata ikiwa ni Sh20,000 tu hivyo kwa mwaka mzima unatakiwa kulipa jumla ya Sh60,000,” amesema.
Amesema miongoni mwa madhara yanayoweza kuwapata endapo hawatarasimisha biashara zao ni pamoja na kufungiwa shughuli zao na kukosa fursa mbalimbali ikiwa ikiwemo mikopo kutoka taasisi za kifedha.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka amemshukuru mbunge huyo kwa msaada huo ambao amesema kwa kiwango kikubwa utaboresha shughuli za walengwa na maisha yao kwa ujumla.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka akikabidhi mashine ya kukaushia nywele kwa mmiliki wa saluni ya kike mjini Musoma. Mashine hiyo ni sehemu ya vifaa vilivyotolewa na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mara Agnes Marwa kwa wajasiriamali wa saluni za kike na kiume mjini Musoma. Picha na Beldina Nyakeke
“Umekuwa sehemu ya suluhisho la changamoto mbalimbali katika jamii yetu hii ina maana kuwa umeamua kuongeza nguvu kwenye kile ambacho Serikali inakifanya,” amesema.
Chikoka amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itahakikisha sekta zote zinafikiwa ili kuleta mapinduzi ya kiuchumi katika Manispaa ya Musoma.
Wanufaika wa msaada huo mbali na kumshukuru mbunge huyo pia wamesema vifaa hivyo vitasaidia katika kuboresha shughuli zao.
“Huwezi amini mashine yangu ya kukausha nywele imeharibika wiki mbili zilizopita, kwa hiyo mashine hii imekuja muda muafaka namshukuru sana mbunge,” amesema Joyce Manyama.
Kwa upande wake, Eliya Pius amesema mashine aliyopata itasaidia kuongeza kasi ya utendaji kazi kwani awali alikuwa na mashine moja pekee, ambayo husababisha kukosa wateja hasa wale wenye haraka.