Mbeya. Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Mbeya umeanza kufunga taa za kisasa katika maeneo yenye kona kali kwenye barabara ya Mbeya–Chunya ili kudhibiti ajali za mara kwa mara.
Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kupunguza ajali sambamba na kuziba mashimo yaliyojitokeza kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Meneja wa Tanroads Mkoa wa Mbeya, Seleman Bishanga, amesema hayo leo Jumanne Machi 3, 2026 wakati akiwasilisha taarifa ya matengenezo ya barabara katika kikao cha bodi ya barabara kilichofanyika jijini humo, kikiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Beno Malisa.
Kikao hicho kilihusisha wadau mbalimbali wakiwemo kutoka taasisi za Serikali, wabunge, wenyeviti na wakurugenzi wa halmashauri, pamoja na kupitia taarifa za fedha kwa mwaka 2024/25 na 2025/26.
Bishanga amesema barabara ya Mbeya–Chunya imepewa kipaumbele kutokana na ajali zinazotokea katika kona kali, na tayari mkandarasi amepewa maelekezo ya kuanza haraka ufungaji wa taa hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bano Malisa akifungua kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa kilicho fanyika leo Jumanne Machi 3,2026. Picha na Hawa Mathias
Mbali na hilo, amesema Tanroads imeanza kuziba mashimo yaliyoathiriwa na mvua ili kupunguza usumbufu kwa madereva na wananchi. Maeneo yanayohitaji matengenezo ya kudumu kwa kuweka zege imara, hasa katika kona kali, tayari yameanza kufanyiwa kazi.
Katika kujiandaa na athari za mafuriko, Tanroads imepokea karavati 400 zitakazotumika kuinua na kuimarisha barabara zilizo kwenye hatari ya kuathirika.
Bishanga amesema hali ya barabara kwa ujumla inaridhisha kutokana na utaratibu wa kutenga fedha za matengenezo kila mwaka. Hadi Desemba 2025, ukaguzi wa “road condition survey” umeonesha kuwa asilimia 44.62 ya barabara kuu za lami ziko katika hali nzuri, asilimia 28.90 ziko katika hali ya wastani na asilimia 26.48 ziko katika hali mbaya.
Kwa upande wa barabara kuu za changarawe, asilimia 16.57 ziko katika hali nzuri, asilimia 69.83 wastani na asilimia 10.42 ziko katika hali mbaya.
Akizungumza katika kikao hicho, Malisa, ameagiza changamoto za wananchi zitatuliwe kwa haraka ili kutekeleza azma ya Serikali ya awamu ya sita ya kuboresha huduma za miundombinu.
Baadhi ya Wabunge wa majimbo ya Mkoa wa Mbeya walioshiriki kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa kilichofanyika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Picha na Hawa Mathias
“Sikilizeni na kutatua kero za wananchi kwa wakati ili kuharakisha maendeleo,” amesema Malisa, huku akiipongeza Tanroads kwa juhudi za kutekeleza miradi ya barabara kwa wakati, jambo linalochochea shughuli za kiuchumi.
Kwa niaba ya wabunge wa Mkoa wa Mbeya, Mbunge wa Lupa, Masache Kasaka, ameishukuru Tanroads kwa maboresho ya miundombinu akisisitiza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana bila barabara bora.