Wahusika wa mzozo huu unaoendelea kutokota wameeleza wanachoona ni chachu ya mashambulizi Danny Danon ni mwakilishi wa Kudumu wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa anasema “Iran ililazimika kuacha kuzalisha urani, lakini haikufanya chochote. Badala yake, imeimarisha vituo vyake vya nyuklia na kuongeza uzalishaji wa makombora.”
Maneno haya yanaonyesha mtazamo wa Israel, kwamba Iran imeendelea na miradi inayoonekana kuwa tishio. Kwao, mashambulizi ni kujilinda. Lakini upande wa Iran unatoa hoja tofauti.
Mwakilishi wa kudumu wa Iran kwenye Umoja wa Mataifa Amir-Saeid Iravani anasema “Vita hii inayoendeshwa na Marekani na Israel inakiuka sheria za kimataifa ni vita dhidi ya Katiba ya Umoja wa Mataifa.”
Ni kauli nzito ya kuonesha mgawanyiko wa kina. Na kwa Marekani kwakilishi wa kudumu kwenye Umoja wa Mataofa Michael Waltz amesisitiza kuwa “Amani hailindwi kwa kuwafurahisha wanaoitishia. Amani inalindwa kupitia nguvu mbele ya ugaidi. Historia imetufundisha kwamba gharama ya kutochukua hatua ni kubwa zaidi kuliko mzigo wa hatua madhubuti, na rais wetu, Donald Trump, amechukua hatua hiyo madhubuti leo.”
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililokutana kwa dharura Februari 28 kujadili kuhusu Iran
Je, diplomasia imefeli?
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali kinachoendelea Mashariki ya Kati akisema “Tunashuhudia tishio kubwa kwa amani na usalama wa kimataifa. Hatua za kijeshi zina hatari ya kuanzisha mfululizo wa matukio ambayo hakuna anayeweza kuyadhibiti katika eneo lenye misukosuko zaidi duniani. Ni wazi kwamba hakuna mbadala unaofaa wa kutatua migogoro ya kimataifa kwa njia za amani. Amani ya kudumu inaweza kupatikana tu kupitia njia za amani, ikiwa ni pamoja na mazungumzo ya kweli na mijadala.”
Onyo hili linatoka juu kabisa katika mfumo wa kimataifa. Umoja wa Mataifa unasema mapigano yanaweza kuzalisha mfululizo wa matukio yasiyodhibitika na kuathiri mamilioni ya watu katika Ukanda huo wa Mashariki ya Kati.
Lakini si diplomasia pekee inayohojiwa. Hatari ya nyuklia imeingia kwenye mjadala. Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la nishati ya atomiki IAEA Mariano Grossi amesema “Hakuna dalili za kuharibiwa kwa mitambo ya nyuklia ya Iran, mashambulizi dhidi ya vituo vya nyuklia yanaweza kusababisha madhara makubwa ya mionzi. Hebu nisistize kwamba hali ilivyo leo inatia wasiwasi mkubwa. Hatuwezi kuondoa uwezekano wa kuachiliwa kwa mionzi yenye madhara makubwa, ikiwemo ulazima wa kuhamisha watu kutoka maeneo makubwa au hata makubwa kuliko miji mikuu.”
Kauli hiyo ya Mkuu wa IAEA inaonya, malengo ya nyuklia si tu changamoto ya kijeshi, bali tishio la kibinadamu.
Watoto wanacheza kando ya mto huko Tehran. (Maktaba)
Raia ndio wanaobeba mzigo mkubwa
Na raia je? Hapa ndipo simulizi inakuwa nzito. Kamishina Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk anasema“Kama ilivyo kila wakati kwenye vita wanaolipa gharama kubwa ni raia. Mabomu na makombora sio njia ya kutatua tofauti , lakini yanachofanya ki kusababisha vifo, uharibifu na madhila kwa binadamu. Ili kuepuka athari hizo mbayá kwa raia, natoa wito wa kujizuia, kwa pande zote kuona sababu ya kupunguza mvutano na kurejea kwenye meza ya mazungumzo ambako wamekuwa wakisaka suluhu.”
Kauli hii inarudia historia, vita huumiza wasiohusika. Shule, hospitali, na maisha ya kawaida yanageuka uwanja wa maumivu.
Mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa yanatoa tahadhari kwamba “Watoto hulipa gharama kubwa zaidi katika migogoro ya silaha, huathiri upatikanaji wa chakula na kuongeza mateso. Na huduma za afya hazipaswi kulengwa au kuzuiwa.”
Haya ni maombi ya msingi kulinda maisha.
Hadi sasa, mashambulizi yameripotiwa katika maeneo kadhaa Mashariki ya Kati ikiwemo Bahrain, Jordan, Oman, Kuwait, Qatar, Saudi Arabia, United Arab Emirates na Israel.
Takwimu zinaonesha watu zaidi ya 500 wameuawa, hospitali zimeharibiwa, na hofu ya kuenea kwa vita inatanda.
Mkutano wa kupitisha Chata ya Umoja wa Mataifa huko San Francisco kuanzia Aprili 25 hadi 26 mwaka 1945
Chata ya Umoja wa Mataifa
Je, msingi wa kisheria unasemaje? Mjadala unarudi kwenye Chata ya Umoja wa Mataifa ambapo
- Kifungu cha 2(4) kinakataza matumizi ya nguvu.
- Kifungu cha 51 kinatoa haki ya kujilinda.
Hivyo pande zote zinatoa tafsiri tofauti lakini dunia inasubiri suluhu.
Umoja wa Mataifa unatoa wito kusitisha mapigano, kupunguza mivutano, kurudi kwenye mazungumzo. Kwa sababu historia inaonyesha vita vinaweza kuanza kwa dakika, lakini kuponya majeraha yake huchukua miongo.
Endendelea kufuatilia kupata kwa taarifa zaidi za yale yanayojiri katika mzozo huu.