Ili tuendelee kufurahia manufaa na uzuri wa asili, juhudi za pamoja zimekuwa zikifanyika kuhakikisha mifumo ya ikolojia inastawi na aina za mimea na wanyama zinaendelea kuwepo kwa vizazi vijavyo.

media:entermedia_image:d1d868f8-d31f-4c5f-b5f3-3ca3e20a2bb5

© UNESCO/Spiti Wildlife Division Kasa

Miongoni mwa wanyama maarufu wa eneo hilo ni chui wa theluji, Mbweha Mwekundu (anayeonekana hapa) Ibex ya Himalaya, kondoo wa bluu, na mbwa mwitu adimu wa Himalaya.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa Siku ya Wanyamapori Duniani ni fursa ya kusherehekea aina mbalimbali za wanyama na mimea pori, kuongeza uelewa wa faida zake nyingi, na kukumbusha umuhimu wa kupambana na uhalifu dhidi ya wanyamapori na kupungua kwa aina mbalimbali za voumbe hai kunakosababishwa na binadamu, ambako kuna athari za kiuchumi, kimazingira na kijamii.

Mwaka 2026, kaulimbiu ya siku hii ni “Mimea ya Dawa na Manukato: Kuhifadhi Afya, Urithi na Riziki”, ikiangazia mchango mkubwa wa mimea hii katika afya ya binadamu, urithi wa kitamaduni na maisha ya jamii, pamoja na shinikizo linaloongezeka kutokana na uharibifu wa makazi, uvunaji kupita kiasi na mabadiliko ya tabianchi.

Mimea ya dawa hutumika kuanzia tiba za jadi hadi vipodozi na dawa za kisasa, huku mahitaji yakiongezeka kwa kasi.

Umuhimu wake kwa mazingira na uchumi

Wataalamu wanaeleza umuhimu wa mimea hii. Danna J. Leaman, aliyekuwa mwenyekiti mwenza wa Kikundi cha Wataalamu wa Mimea ya Dawa chini ya Tume ya Uhai wa viumbe ya Muungao wa Kimataifa kwa ajili ya uhifadhi wa asili (IUCN), anasema mimea ni mhimili muhimu wa mifumo ya ikolojia na uchumi.

“Katika miaka 15 iliyopita, mwanga umeanza kuelekezwa kwa viumbe mbalimbali ambavyo si tu vinategemewa kwa afya na riziki ya binadamu, bali pia kwa uhai wa mfumo mzima wa bioanuai,” ameiambia UN News.

Mimea ya dawa ni nini?

Hakuna tafsiri moja rasmi ya mmea wa dawa, lakini jamii duniani zimekuwa zikitumia aina mbalimbali tangu enzi za kale. 

Leo, matumizi yake hayapo tu katika tiba za jadi bali pia katika dawa za kisasa, chakula, manukato, vipodozi na sabuni. 

Kadri hamasa ya bidhaa asilia inavyoongezeka, mjadala kuhusu matumizi sahihi na uhifadhi wake unakuwa muhimu zaidi.

Mageuzi katika uhifadhi

Kwa muda mrefu juhudi za uhifadhi zililenga zaidi wanyama, lakini mtazamo huo sasa umebadilika. 

Chini ya Mkataba wa Biashara ya Kimataifa wa viumbe vilivyo Hatarini Kutoweka vya Wanyama na Mimea Pori (CITES), kipaumbele kimepanuka kujumuisha mimea inayouzwa kimataifa.

“Kimsingi, huu ni uthibitisho kwamba hatujishughulishi na wanyama pekee,” amesema Bi. Leaman, akibainisha kuwa CITES inatambua kuwa aina nyingi katika biashara ya kimataifa ni mimea.

Picha ya mimea ya Nardostachys grandiflora, inayoonyesha mmea wenye maua ya waridi, majani ya kijani, na michoro ya kina ya mfumo wake wa mizizi na sehemu za maua.

Mfano wa botani wa Nardostachys grandiflora, mmea wa dawa ulio na michoro ya anatomi ya kina.

Aina 30,000 na hatari zake

Takribani aina 30,000 zinatambuliwa kuwa mimea ya dawa au manukato. Hata hivyo, kama ilivyo kwa bioanuai kwa ujumla, zinakabiliwa na shinikizo la kuongezeka upanukaji wa kilimo, mabadiliko ya matumizi ya ardhi, uvunaji usio endelevu na mabadiliko ya tabianchi, hasa katika maeneo nyeti kama vinamasi na milimani.

Mfano wa mmea ulio hatarini

Mmea mmoja unaoonesha umuhimu na udhaifu wa mimea ya dawa ni nardostachys jatamansi (spikenard), mmea wa milima ya Himalaya unaotumika katika tiba za jadi kama Ayurveda. Mizizi yake yenye harufu hutumika kutengeneza dawa na mafuta muhimu, lakini kwa kuwa sehemu inayovunwa ni mzizi, mara nyingi uvunaji huua mmea.

Ukiwa umeorodheshwa kama hatarini sana kutoweka katika Orodha Nyekundu ya IUCN, juhudi zinafanyika kuhakikisha uvunaji endelevu, hususan Nepal, ambako vikwazo vya biashara vimewekwa kulinda aina pori hata kama hatua hizo zinaweza kuathiri kipato cha jamii za vijijini.

Wajibu wa walaji na kampuni

Mahitaji ya kimataifa ya mimea ya dawa yanaongezeka haraka. Wataalamu wanahimiza walaji kuhakikisha bidhaa wanazonunua zinatoka katika vyanzo endelevu na vyenye maadili.

Zana huru kama jukwaa la mtandaoni la WildCheck, lililoandaliwa kwa ushirikiano na mtandao wa ufuatiliaji wa biashara ya wanyamapori TRAFFIC, wataalamu wa IUCN na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), husaidia kutathmini kama viambato vya mimea vimevunwa kwa njia endelevu na kwa kuzingatia haki za jamii.

Viwango vya uthibitisho kama FairWild Standard pia vinahakikisha kuwa uvunaji na biashara vinazingatia vigezo vya kimazingira, kijamii na kibiashara kuanzia uvunaji hadi uuzaji wa mwisho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *