Katika siku ya nne ya mashambulizi ya anga ya Israel na Marekani dhidi ya Iran, na wakati ghasia na ukosefu wa utulivu vikiongezeka Mashariki ya Kati, Umoja wa Mataifa umetaka kwa dharura ulinzi wa raia na kuonya kuhusu kuongezeka kwa watu wanaokimbia makazi yao pamoja na mahitaji ya kibinadamu.

media:entermedia_image:dcaba87c-4170-423b-af01-c8899c4212a3

United Nations

Ravina Shamsadani, Msemaji wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu.

Msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR), Ravina Shamdasani, amekumbusha pia tukio la kutisha la shambulizi lililoripotiwa Jumamosi ambalo liliua na kujeruhi makumi ya wasichana katika shule ya msingi huko Minab, kusini mwa Iran.

“Watoto, wadogo wasichana mwanzoni wa siku ya shule kuuawa kwa namna hii, mabegi yao ya mgongoni yakiwa na madoa ya damu hili ni jambo la kutisha sana,” amesema. “Ikiwa kuna picha yoyote inayobeba kiini cha uharibifu, kukata tamaa na ukatili usio na maana wa mzozo huu, basi ni picha hizo.”

Bi. Shamdasani akizungumza mjini Geneva Uswisi amesema kuwa Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, ameshtushwa sana na athari za mapigano hayo kwa raia na miundombinu ya kiraia, na ametaka “uchunguzi wa haraka, usioegemea upande wowote na wa kina kuhusu mazingira ya shambulizi la Minab”.

Amesisitiza kuwa “Wajibu uko kwa vikosi vilivyotekeleza shambulizi hilo kuchunguza tukio hilo. Tunavitaka viweke wazi matokeo ya uchunguzi na kuhakikisha uwajibikaji na fidia kwa waathiriwa”.

Bi. Shamdasani pia ameeleza kuwa iwapo itabainika mashambulizi yalilenga raia au mali za kiraia, au yalikuwa ya kiholela, basi hayo ni “ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu na yanaweza kufikia kiwango cha uhalifu wa kivita.”

Kukatika kwa umeme Tehran

Msemaji huyo wa OHCHR ameeleza wasiwasi kuhusu ustawi wa raia wa Iran “ikizingatiwa historia ya Serikali kutumia nguvu za mauti kwa kiwango kikubwa dhidi ya wanaopinga utawala wake na vitisho vipya vya maafisa waandamizi dhidi ya aina yoyote ya upinzani kwa wakati huu.”

Ametoa wito kwa mamlaka kulinda uhuru wa msingi wa Wairani na akalalamikia upatikanaji mdogo wa taarifa muhimu kufuatia kuzimwa kwa mtandao kote nchini.

Tangu mzozo uanze Jumamosi kwa mashambulizi ya Israel na Marekani dhidi ya Iran, Tehran ilijibu kwa mashambulizi ya kulipiza dhidi ya Israel na washirika wengine wa Marekani katika ukanda huo. 

Bi. Shamdasani amesisitiza kuwa mbali na Iran na Israel, mapigano hayo tayari yameathiri nchi nyingine 12, yakiharibu nyumba, biashara, viwanja vya ndege na miundombinu ya nishati.

Mtambo wa nyuklia ulioko Bushehr nchini Iran.

© IAEA/Paolo Contri

Mtambo wa nyuklia ulioko Bushehr nchini Iran.

Uharibifu katika mtambo wa nyuklia wa Natanz Iran

Shirika la Umoja wa Mataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) leo limethibitisha kuwepo kwa “uharibifu kutokna na mashambulizi ya hivi karibuni katika majengo ya kuingilia Kituo cha Kurutubisha Mafuta ya Nyuklia cha Natanz”, kilichoko takribani kilomita 240 kusini mwa Tehran katikati mwa Iran. 

Kwa mujibu wa shirika hilo, tathmini ya picha za satelaiti imeonesha athari hizo kufuatia mashambulizi ya kijeshi ya karibuni, hata hivyo hakuna dalili ya madhara ya mionzi. “Hakuna athari za mionzi zinazotarajiwa na hakuna madhara ya ziada yaliyogunduliwa katika Kituo cha Kurutubisha Mafuta ya Nyuklia (FEP) chenyewe, ambacho kiliharibiwa vibaya katika mzozo wa mwezi Juni,” imesema IAEA, ikisisitiza kuwa hali ya usalama wa nyuklia katika eneo hilo inaendelea kufuatiliwa kwa karibu.

Watu wanakimbia Lebanon

Nchini Lebanon, ambako wanamgambo wa Hezbollah waliingia katika mzozo huo na kusababisha mashambulizi ya Israel, “watu wengi wameripotiwa kufungasha virago na kukimbia makazi yao katika maeneo ya kusini mwa Lebanon, Bekaa na vitongoji vya kusini mwa Beirut,” amesema msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Babar Baloch.

Israel ilitoa maonyo ya kuhama kwa wakazi wa zaidi ya vijiji 53 vya Lebanon na kufanya mashambulizi makali ya anga katika sehemu zote tatu za nchi hiyo, amesema.

Hadi Jumatatu wiki hii “makadirio ya tahadhari yanaonesha kuwa karibu watu 30,000 wamepokelewa na kusajiliwa katika makazi ya pamoja,” amesema Bwana. Baloch. “Wengine wengi walilala ndani ya magari yao kandokando ya barabara au walikwama kwenye misongamano ya magari wakiondoka kusini kuelekea Beirut.”

Wanajeshi wawili wa amani wa UNIFIL wakiwa wamevaa kofia za rangi ya bluu wanatazama eneo hilo kwa kutumia vioo vya macho, wakiwa wamesimama kando ya Mstari wa Bluu huko Lebanoni.

Wanajeshi wa amani wa UNIFIL wanafuatilia Mstari wa Bluu nchini Lebanon.

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari leo Jumanne, wanajeshi wa ardhini wa Israel wameingia kusini mwa Lebanon kufuatia mashambulizi ya Hezbollah dhidi ya kaskazini mwa Israel.

Msemaji huyo wa UNHCR amesisitiza kuwa nchi nyingi zilizoathiriwa na mzozo huu mpya “tayari zinahifadhi mamilioni ya wakimbizi na watu waliokimbia makazi yao ndani ya nchi zao.”

Ameonya kuwa ghasia na uhamaji zaidi vinaweza kuzidi uwezo wa jamii zinazowahifadhi.

Wasiwasi wa minyororo ya usambazaji

Usumbufu mkubwa katika usafirishaji wa bidhaa kutokana na kuongezeka kwa mapigano katika ukanda huo pia unaathiri njia za usambazaji wa misaada ya kibinadamu na watu wanaotegemea misaada hiyo kwa mlo wao ujao.

Akizungumza kutoka Cairo Misri, Samer Abdel Jaber, Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), amebainisha usumbufu katika Mlango wa Bahari wa Hormuz na Bahari Shamu ambao “utatatiza njia za baharini na kusababisha ucheleweshaji pamoja na kuongeza gharama kwa operesheni zetu nyingi zinazotegemea njia hizo.”

“Kwa kuwa bahari zinagombaniwa na anga zikifungwa, tunalazimika kubadilika na kutumia mitandao yetu ya wasambazaji katika nchi nyingine kama Uturuki, Misri, Jordan na Pakistan kusaidia njia za usafirishaji wa nchi kavu,” amesema.

Afisa huyo wa WFP ameongeza kuwa bandari za Misri na Mfereji wa Suez, “kitovu muhimu kwetu kusaidia operesheni zetu Gaza na pia Sudan, bado zinafanya kazi”.

media:entermedia_image:6c9d7272-2965-41a2-aac7-3faeedcbba18

UN Photo/JC

Amesema uamuzi wa Israel kufunga vivuko vya mpaka wa Gaza tangu kuanza kwa mzozo huo ulikuwa wa kutia wasiwasi, lakini leo Jumanne kumekuwa na “habari njema za kufunguliwa kwa kivuko cha Kerem Shalom.”

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, kivuko hicho kilichoko mpakani kusini mwa Ukanda wa Gaza kilifunguliwa tena leo Jumanne.

“Hiyo ni kwa wakati muafaka kwetu na tunahitaji kuingiza misaada haraka iwezekanavyo,” amesema Bwana. Jaber akihitimisha kuwa “Tuna unga wa ngano wa kutosha kwa siku 10 tu na vifurushi vya chakula vitakavyodumisha programu zetu kwa wiki mbili na nusu pekee. Tunapaswa kuhakikisha kuwa kuna mtiririko endelevu na unaoweza kuongezwa wa chakula kuingia Ukanda wa Gaza”.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *