Taasisi ya kimataifa ya sekta ya mawasiliano ya simu, GSMA, imemtunuku Tuzo ya Maisha (Lifetime Achievement Award) Sunil Bharti Mittal, Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Bharti Enterprises, kwa kutambua mchango wake mkubwa katika kubadili na kuunda upya taswira ya mawasiliano ya simu duniani pamoja na kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa waendeshaji, serikali, biashara na mabilioni ya watumiaji.

Tuzo hiyo adimu, ambayo imetolewa kwa viongozi wachache tu katika historia ya GSMA, hutambua mchango wa kipekee ulioacha alama ya kudumu na yenye mwelekeo katika mfumo wa kimataifa wa mawasiliano. Ilikabidhiwa rasmi Machi 2, 2026 wakati wa mkutano wa Mobile World Congress uliofanyika Barcelona, Hispania, mbele ya viongozi waandamizi akiwamo Mfalme Felipe VI wa Hispania, Waziri Mkuu Pedro Sanchez na Rais wa Catalonia Salvador Illa, pamoja na wakuu wa kampuni na taasisi mbalimbali za mawasiliano kutoka duniani kote.

Kupitia uongozi wake wa maono, Mittal ameijenga Bharti Airtel kuwa miongoni mwa waendeshaji wakubwa zaidi wa huduma za simu duniani, ikiwa na shughuli zake India na barani Afrika. Kampuni hiyo imeorodheshwa miongoni mwa waendeshaji watatu wakuu duniani na kwa sasa inahudumia zaidi ya wateja nusu bilioni, hatua iliyochangia kwa kiasi kikubwa kupanuka kwa huduma za mawasiliano katika masoko yanayoibukia.

Mbali na mafanikio hayo ya kibiashara, Mittal aliwahi kuwa Mwenyekiti wa GSMA kati ya mwaka 2017 na 2018, ambapo alitetea sera zinazochochea uwekezaji, ubunifu na ujumuishwaji wa kidijitali, akisisitiza umuhimu wa kuunganisha watu wasiofikiwa na huduma za mawasiliano ili kukuza maendeleo jumuishi.

Awali, Mittal alitunukiwa Tuzo ya Mwenyekiti wa GSMA mwaka 2008 na tena mwaka 2016 kwa mchango wake katika kukuza sekta ya simu duniani, na aliheshimiwa pia wakati wa Mobile World Congress mwezi Februari 2019 kwa kutambua uongozi wake kama Mwenyekiti wa GSMA.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mittal amesema: “Nimeheshimiwa sana kupokea tuzo hii na ninaishukuru kwa dhati GSMA kwa kunitambua. Naipokea si tu kama mafanikio binafsi, bali kama heshima kwa safari ya sekta ya mawasiliano ya India, ari ya pamoja ya Bharti na kuibuka kwa kampuni za mawasiliano za India katika jukwaa la kimataifa.”

Ameongeza: “Sekta ya mawasiliano ni nguvu inayopanua fursa, inayoweka huduma muhimu mikononi mwa kila mtu na kufungua uwezo wa kibinadamu. Kushiriki katika kuunda mageuzi yake na kuifanya kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kisasa ni jukumu la heshima kubwa. Kadiri ubunifu unavyozidi kushika kasi, tutaendelea kushirikiana na wadau wetu kuhakikisha ukuaji unaendeleza usawa na kuleta fursa endelevu kwa vizazi vijavyo.”

Tuzo ya Maisha ya GSMA ni heshima ya juu inayotolewa kwa watu wachache waliodhihirisha uongozi na ubunifu uliobadili mwelekeo wa sekta ya mawasiliano kwa namna ya kudumu duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *