
Wakati Tanzania ikiadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kila ifikapo Machi 8, hiyo ni fursa kwa wanawake na wasichana wa Tanzania ya kutafakari pia, si mafanikio tu yaliyopatikana, bali pia wajibu unaowakabili wanawake na wasichana wa Kitanzania katika kujenga taifa linalojitegemea, lenye usawa na maendeleo jumuishi.
Maadhimisho haya yasiishie kwenye sherehe na hotuba, bali yawe chachu ya kuamsha ari ya kupambana, kujiamini na kuthibitisha kwa vitendo kuwa mwanamke anaweza kusimama na kufanya makubwa bila kusubiri kubebwa.
Katika historia ya Tanzania, wanawake wamekuwa nguzo muhimu katika familia, jamii na uchumi.
Hata hivyo, mchango wao mara nyingi haujatambuliwa kwa uzito unaostahili. Leo hii, taswira hiyo inabadilika kwa kasi. Wanawake wanazidi kuonekana katika nafasi za uamuzi, biashara, taaluma na ubunifu. Huu ni ushahidi kwamba uwezo upo; kinachohitajika ni uthubutu, maandalizi na msimamo thabiti.
Kisiasa na kiuongozi, mwanamke wa Kitanzania anapaswa kuamini kuwa ana haki na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kufanya uamuzi.
Uongozi si suala la jinsia, bali ni suala la maono, uadilifu na uwezo wa kusimamia rasilimali na watu. Wasichana wanaokua leo wanahitaji kuona mifano hai ya wanawake waliothubutu kuingia katika ulingo wa siasa na uongozi, wakasimama imara na kuonyesha kwamba wanaweza kuongoza kwa ufanisi.
Lakini zaidi ya mifano hiyo, wanapaswa kujitayarisha mapema kwa kujifunza, kujenga hoja zenye mashiko na kushiriki mijadala ya kitaifa kwa ujasiri.
Katika nyanja ya elimu, ndiko kunakopatikana msingi wa mapinduzi ya kweli ya mwanamke. Elimu humjengea mtu maarifa, kujiamini na uwezo wa kuchanganua masuala kwa kina. Msichana anayesoma kwa bidii leo ndiye mwanamke atakayesimama kesho kama daktari, mwanasheria, mhandisi, mwalimu au kiongozi wa taasisi kubwa.
Hivyo, kupambana katika elimu si chaguo, bali ni wajibu. Ni lazima kuondoa dhana potofu kwamba baadhi ya taaluma ni za wanaume pekee. Sayansi, teknolojia, uchumi na siasa ni maeneo ambayo wanawake wanaweza kung’ara kwa ubora sawa au hata zaidi.
Kijamii, bado kuna vikwazo vinavyoweza kumrudisha nyuma mwanamke, vikiwamo mila kandamizi, mitazamo hasi na shinikizo la kijamii. Hapa ndipo nguvu ya kujitegemea inahitajika zaidi.
Mwanamke anayejitambua hatayumba kirahisi mbele ya maneno ya kukatisha tamaa. Atatambua kuwa heshima yake haitokani na kumtegemea mtu, bali na juhudi, maadili na mchango wake katika jamii.
Kujitegemea kiuchumi ni nguzo mojawapo ya ukombozi wa kweli wa mwanamke. Wanawake wanapaswa kuthubutu kuanzisha na kuendeleza biashara, kushiriki katika vikundi vya uzalishaji na kutumia fursa za mikopo na mafunzo zinazotolewa na taasisi mbalimbali.
Ni muhimu pia kwa wanawake wenyewe kuaminiana na kusaidiana. Mafanikio ya mwanamke mmoja yawe chachu kwa mwingine, si sababu ya wivu au chuki. Mtandao wa wanawake wanaosaidiana katika taaluma, biashara na uongozi unaweza kuwa nguvu kubwa ya mabadiliko ya kijamii na kiuchumi. Pale mwanamke anapopata nafasi ya uongozi, anapaswa kuifanyia kazi kwa bidii ili kuondoa dhana kwamba amewekwa tu kwa ajili ya kujaza takwimu.
Kwa wasichana wadogo, ujumbe ni mmoja: ndoto zenu ni halali. Msikubali mipaka ya mawazo ya watu iwafunge. Jifunzeni, ombeni ushauri, fanyeni kazi kwa bidii na kubalini changamoto kama sehemu ya safari ya mafanikio. Hakuna mafanikio yasiyo na juhudi. Kushindwa mara moja au mara mbili si mwisho wa safari, bali ni somo la kujiimarisha zaidi.
Kadiri dunia inavyobadilika, ndivyo nafasi za wanawake zinavyopanuka.
Tanzania inahitaji nguvu, akili na ubunifu wa wanawake wake ili kufikia maendeleo endelevu. Hivyo, Siku ya Wanawake Duniani iwe ni zaidi ya kumbukumbu; iwe ni kiapo cha upya kwamba mwanamke wa Kitanzania atasimama, atapambana na atathibitisha kwa vitendo kuwa anaweza kufanya jambo kubwa kwa taifa lake katika nyanja zote za kisiasa, kiuongozi, kielimu na kijamii, kwa kujitegemea na kujiamini. 0713235309