Marekani. Akiwa ameuza rekodi zaidi ya milioni 300 duniani kote na kutambulika kama mwanamuziki wa kike aliyeuza zaidi kwa wakati wote bado Madonna (67), ni mama wa watoto sita na safari yake ya malezi ina maajabu yake.
Hata hivyo, Madonna anakiri kuwa mama wa watoto sita sio kazi rahisi. Januari 2023 aliliambia Jarida la Vanity Fair kuwa kazi ya malezi ni ngumu na hadi sasa katika umri wake bado hajaelewa jinsi ya kuwa mama.
“Kuwa na watoto na kuwalea ni kazi ya sana na hakuna mtu anayekupa muongozo. Unapaswa kujifunza kutokana na makosa, ni taaluma inayohitaji muda mwingi kuielewa na inachosha kwa sababu hakuna kupumzika kamwe.” alisema Madonna.
Utakumbuka kwa mara ya kwanza Madonna aliolewa na Sean Penn Agosti 16, 1985 na wakadumu hadi mwaka 1989 walipoachana. Mwaka 2000 alikuja kuolewa tena na Guy Ritchie na kudumu hadi mwaka 2008.
Alijaliwa mtoto wake wa kwanza, Lourdes hapo Oktoba 14, 1996 na aliyekuwa mpenzi wake, Carlos Leon, ilikuwa furaha kwake hadi kuandika wimbo, Little Star unaopakana kwenye albamu yake, Ray of Light iliyoshinda tuzo ya Grammy mwaka 1998.
Kwa sasa Lourdes ni Mwanamitindo aliyefanikiwa kwa kiasi chake, amefanya kazi katika katika kutangaza bidhaa za urembo za Rihanna, Savage x Fenty, huku akitokea kwenye kava za majarida makubwa duniani kama Vogue na Vanity Fair.
Baada ya kutengana na Carlos Leon Mei 1997, Madonna alianzisha uhusiano na Guy Ritchie mwaka 1998, walijaliwa mtoto wa kiume, Rocco aliyezaliwa Agosti 11, 2000 na kubatizwa huko Scotland katika Kanisa Kuu la Dornoch hapo Desemba 20, 2000.
“Wakati fulani nilifunga tu macho yangu na kufikiria tu, ‘kwa nini jikoni kwangu hakujajaa watoto wanaocheza dansi?’ kuna watoto wengi wanaohitaji nyumba, nilifikiria, ‘ninangojea nini? fanya kitu kwa ajili yao’.” Madonna aliliambia Jarida la People.
Kauli ya Madonna alikuja baada ya kuasili watoto wanne kutoka nchini Malawi ambao ni David (2006), Mercy (2009) na mapacha Esther na Stella (2017), na kumfanya kuwa na jumla ya watoto sita akiongeza na wake wawili, Lourdes (29), na Rocco (25).
David Banda (20) alizaliwa huko Malawi Septemba 24, 2005. Kufika Oktoba 2006 Madonna akatembelea nchi hiyo akiongozana na aliyekuwa mumewe, Ritchie baada ya kuanzisha shirika lake la hisani, Raising Malawi
Waliamua kumuasili David aliyekuwa na umri wa mwaka mmoja wakati huo. Alikuwa akilelewa na kituo cha watoto yatima, Home of Hope katika mji mkuu wa Lilongwe.
Hata hivyo, wanandoa hao walikabiliwa na upinzani kwa sababu sheria za Malawi zinataka wazazi wa kuwaasili kuishi nchini humo kwa angalau miezi 18, lakini mpango huo ulikuja kuidhinishwa Mei 28, 2008.
Mwaka 2019 Madonna aliliambia Jaridi la Vogue kuwa David ndiye mtoto ambaye anaendana naye sana. Anahisi ana DNA zake zaidi kuliko mtoto wake yeyote yule. David amekuwa akifanya mitindo na mara nyingi amejumuishwa katika maonyesho ya Madonna kama Pride Variety Show huko New York 2022.
Chifundo ‘Mercy’ James (20) alizaliwa Januari 22, 2006 nchini Malawi, mwaka 2008 Madonna alipoachana na mumewe kwa talaka. Aliomba kumuasili Mercy kama mama asiye na mwenzi kutoka kituo cha watoto yatima huko Blantyre, Malawi.
Awali Mahakama Kuu ilitupilia mbali ombi lake, lakini baadaye Juni 12, 2009 lilikubaliwa.
Julai 2017, Madonna alifungua Taasisi yake, Mercy James Institute for Pediatric Surgery and Intensive Care. Lengo ni kusaidia upasuaji wa watoto wagonjwa mahututi nchini Malawi.
3. Stella na Estere
Mapacha Stella na Estere (13) walizaliwa nchini Malawi Agosti 24, 2012, Madonna aliasili mabinti hawa walipokuwa na umri wa miaka mitano hapo Februari 2017.
Katika mahojiano na Jarida la People, Madonna alisema Stella na Estere ni kama walikuwa naye kwa wakati wote maana hawakuchua muda mrefu kuzoea mazingira ya Marekani. Na wamejifunza kwamba yeye ndiye mama yao na hakuna kitakachobadilisha hilo.
Ikumbukwe Madonna amekuwa akitoa misaada sehemu mbalimbali duniani, baada ya kuanzisha mfuko wake wa hisani, Ray of Light Foundation mwaka 1998 na Raising Malawi mwaka 2006.
Kwa mujibu wa Forbes, utajiri wake kwa sasa ni Dola575 milioni, wastani wa Sh1.4 trilioni, anakadiriwa kutengeneza kitita cha Dola1.2 bilioni, wastani wa Sh2.7 trilioni katika maisha yake ya muziki. Ndiye mwanamuziki wa kike aliyelipwa fedha nyingi zaidi kila mwaka katika miongo minne, kuanzia mwaka 1980 hadi 2010.
Na ukiachana na muziki uliompatia tuzo saba za Grammy, umaarufu wa Madonna uliongezeka kwa kucheza filamu kama vile; Desperately Seeking Susan (1985), Dick Tracy (1990), A League of Their Own (1992) na Evita (1996).