Dar es Salaam. Mwimbaji Angelique Kidjo (65), kutokea Benin ndiye mwanamuziki solo Afrika aliyeshinda tuzo nyingi za Grammy akiwa amepambana na muziki kwa zaidi ya miaka 40 huku akitoa albamu 16 tangu mwaka 1989 hadi 2021 aliposhinda tuzo yake ya mwisho.
Yupo katika orodha ya wasanii wachache Afrika walioshinda Grammy kwa kazi zao wenyewe akiwa ni wa sita kufanya hivyo baada ya Miriam Makeba (Afrika Kusini), Sade Adu (Nigeria), Ali Farka Toure (Mali), Cesaria Evora (Cape Verde) na Youssou N’Dour (Senegal).
Angelique Kidjo alizaliwa Julai 14, 1960 huko Ouidah, Benin katika familia inayopenda sanaa, Baba yake alikuwa mwanamuziki na Mama yake akiwa dansa na mkurugenzi wa ukumbi wa michezo.
Licha ya kukua akisikiliza muziki wa kitamaduni kutoka jamii za Yoruba na Fon, bado alivutiwa na wasanii wengine kutoka mataifa mengine. Alisikiliza nyimbo za Fela Kuti, Miriam Makeba, Hugh Masekela, James Brown, Stevie Wonder, Osibisa, Manu Dibango n.k.
Akiwa na umri miaka sita tayari alikuwa akitumbuiza na kikundi cha Mama yake, na punde tu akaanza kuimba katika bendi ya shule, Les Sphinx na akapata mafanikio baada ya kuurudia wimbo wa Miriam Makeba ‘Les Trois Z’ uliochezwa kwenye redio ya taifa.
Nyota yake ikiwa imeanza kung’aa Afrika Magharibi, Kidjo alilazimika kuondoka Benin mwaka 1983 kutokana na migogoro ya kisiasa na kuhamia Paris, Ufaransa aliposomea muziki katika chuo cha CIM licha ya awali kuwa na ndoto ya kusoma sheria.
Katika chuo hicho alikutana na mwanamuziki na mtayarishaji kutokea Ufaransa, Jean Hebrail ambaye walishirikiana katika muziki kabla ya kufunga ndoa mwaka 1987 na kujaliwa mtoto mmoja, Naima aliyezaliwa 1993.
Akiwa Ufaransa Kidjo alianza kuimba katika bendi ikiwemo Pili Pili na kushiriki katika albamu tatu, Jakko (1987), Be In Two Minds (1988) na Hotel Babo (1990), kazi zilizompa umaarufu kabla ya kutoa albamu yake ya kwanza kama solo, Parakou (1989).
Kipaji chake kilimvutia mwanzilishi wa Island Records, Chris Blackwell na kuamua kumsaini na kutoa albamu nne, chini ya mikono ya Blackwell jina la Kidjo lilikuwa kwa kasi na tangu wakati huo amefanya kazi na lebo mbalimbali hadi kuweza kutoa albamu 16.
Mwaka 1995 Kidjo alirejea kwao Benin akiwa na mume wake, Hebrail na kuzunguka sehemu kubwa ya nchi hiyo wakirekodi vionjo vya asili ambavyo vilitumika katika albamu yake ya nane, Fifa (1996).
Hata hivyo, haikuwa rahisi kushinda tuzo za Grammy kwani ilimchukua miaka mingi huku akifanya kazi nyingi, alipambana hadi alipotoa albamu yake ya nane, Djin Djin (2007) iliyoshinda Grammy 2008 kama Albamu Bora ya Muziki Duniani.
Akaja kushinda tuzo nyingine nne katika kipengele hicho hicho kupitia albamu zake nne tofauti ambazo ni Eve (2014), Angelique Kidjo Sings with the Orchestre Philharmonique Du Luxembourg (2015), Celia (2019) na Mother Nature (2021).
Kidjo anaamini nyimbo zake zinaweza kuhamasisha umoja unaosababisha mabadiliko makubwa. Alisema albamu yake, Mother Nature (2021) ni barua ya upendo kwa Mama Dunia na maadili yote tunayoyathamini ambayo ni ukweli, uaminifu, upendo na uhusiano mzuri.
“Katika maisha yetu wenyewe, tunahitaji kutambua ubinadamu ambao sote tunashiriki na kujifunza jinsi ya kuishi pamoja. Hakuna njia nyingine zaidi ya hiyo,” alisema Angelique Kidjo anayetamba na kibao chake, Joy (2024) akimshirikisha Davido.
Mwimbaji huyo ambaye mwaka 2021 Jarida la Time lilimjumuisha katika orodha ya watu 100 wenye ushawishi mkubwa zaidi duniani, pia ametajwa kuwania tuzo za 67 za Grammy zitakazotolewa katika ukumbi wa Crypto.com Arena, Los Angeles.
Ikumbukwe baada ya Kidjo kushinda Grammy ya kwanza kupitia kazi yake binafsi, wasanii wengine Afrika waliofuatia ni RedOne (Morocco), Tinariwen (Mali), Burna Boy (Nigeria), Black Coffee (Afrika Kusini), Tyla (Afrika Kusini) na Tems (Nigeria).
Kidjo anazungumza lugha tano ikiwemo Kifaransa, Kiingereza na Kiyoruba ila muziki wake unamfanya kuwasiliana na watu wengi na kufanya kazi na wasanii wenzake kutoka kila pembe ya dunia.
Tayari ameshirikiana na wasanii kama Tina Turner, Carlos Santana, Ziggy Marley, Tony Allen, John Legend, Bono, Branford Marsalis, Alicia Keys, Dave Matthews, Yemi Alade, Jimmy Buffett, Peter Gabriel, Burna Boy, Philip Glass, Sting, Davido n.k.
Wakati Angelique Kidjo akiwa kinara wa Grammy Afrika, kwa dunia nzima rekodi hiyo inashikiliwa na Beyonce Knowles (43), ambaye ameshinda tuzo 35 na kuchaguliwa kuwania mara 99 na pia ndiye mwanamuziki anayeongoza katika eneo hilo akimpiku Jay Z.