Dar es Salaam. Muziki una siri kubwa sana. Kila kabila hapa nchini lina muziki wake wa asili. Na kwa kawaida muziki huu ukisikika tu, mwenye kabila lake husikia aina ya msisimko ambao hutokea ndani yake, hata kama ni mara ya kwanza kuusikia  muziki huo. 

Kuna tafiti za kisayansi zinasema kuwa mimba ikiwa tumboni iksha fikia umri fulani huanza kusikia sauti, sauti ya kwanza kuwa ni mapigo ya moyo wa mama mzazi, mapigo haya yako tofauti mama akiwa  amepumzika  akiwa hana tatizo, lakini mapigo hayo huwa tofauti kama mama ana masikitiko au ana furaha na yote hayo mtoto anayasikia. 

Lakini pia mtoto huanza kusikia muziki ambao mama yake anasikiliza na hapo ndipo inadaiwa binadamu  huanza kujengwa aina ya muziki wa kudumu katika ubongo wake. Hi ndio sababu inayodaiwa kwanini mtu akisikia muziki wa kabila lake mwili unaanza kusikia raha.

Muziki wa kiasili humfanya mtu ajitambue. Katika miaka iliyopita,  zilifanyika jitihada  kubwa hapa nchini kuhakikisha muziki wa asili unapata nafasi ya kusikika  kila mahala. Kulikuwa na vipindi vya muziki huo redioni, kipindi maarufu kiliitwa ‘Mkoa kwa Mkoa’ kilichokuwa kikiendeshwa na mtangazaji maarufu marehemu Michael Katembo. 

Kuanzia shule za msingi mpaka chuo kikuu wakati huo kulikuwa na vikundi vya muziki wa asili. Kulikuwa na mashindano makubwa ya muziki huo, kuanzia darasa kwa darasa, mpaka vyuo kwa vyuo kwa vyuo. Siku za sikukuu za kitaifa  vikundi kutoka makabila mbalimbali vilionyesha umahiri wa ngoma za makabila yao.  Ngoma hizi zilisaidia sana kujitambua na  kuongeza hali ya uzalendo.

Muziki umekuwa ukitumika sana katika kuelimisha. Katika awamu za zamani za uongozi wa nchi, wanamuziki walihamasishwa kutunga nyimbo za kueleimisha jamii kwa maazimio ya aina mbalimbali. 

Tukianzia na Azimio la Arusha, azimio la kisiasa lililoiingiza nchi katika mfumo mpya wa imani ya kisiasa. Zilitungwa nyimbo kwa maelfu, nyimbo za asili, nyimbo za dansi, nyimbo za taarab, nyimbo za kwaya, zote zikiongelea sura mbalimbali za Azimio la Arusha, hakika katika miaka ya mwanzo ya 1970, haikuwa rahisi kwa Mtanzania yeyote mwenye akili kutokuwa na taarifa ya Azimio la Arusha na muziki ulichukua sehemu kubwa sana ya uelimishaji.

Katika miaka hiyohiyo zikatungwa nyimbo nyingi za kuunga mkono juhudi za ukombozi wa nchi zilizokuwa bado zikitawaliwa na wakoloni. Nyimbo zilizotia ushujaa vijana wakajiona wako tayari kubeba silaha na kwenda kuzikomboa nchi hizo. Muziki hakika una nguvu ya ajabu.

Tanzania ilipoingia mgogoro na Iddi Amin wa Uganda, zilitungwa nyimbo nyingi za kuhamasisha nchi nzima kuwa na msimamo mmoja kuhusu Iddi Amin, na hakika kuhamasisha vijana wakati ule kujiunga na jeshi kwenda kumuondoa Amin. 

Kwa wale ambao wamewahi kupitia mafunzo ya jeshi wanajua muziki ulivyo muhimu katika shughuli mbalimbali, zikianzia na mchakamchaka. Nyimbo hufanya askari atembee au kukimbia muda mrefu bila kufikiria kuhusu uchovu wa safari.

Kwa njia hiyohiyo makabila mbalimbali huwa na nyimbo maalumu wakati wa kilimo, nyimbo ambazo huwezesha  kundi la wakulima kulima sehemu kubwa bila ya kuchoka. Makabila mengine yalikuwa na wapiga ngoma ambao wao kazi yao ilikuwa kupiga ngoma na kuimba tu wakati wenzao wanalima.

Kuna muziki uliokuwa ni siri. Nyimbo zilizotumika kwenye jando na unyago,  zilikuweko nyimbo ambazo zilikuwa maalumu kwa wahusika tu na zilikuwa si nyimbo za kuimba hovyo hadharani.  Kulikuwa pia na nyimbo za watoto tu.

Nyimbo zilizosindikizwa na hadithi, nyimbo ambazo zilimfanya mtoto ajisikie yumo ndani kabisa ya hadithi. Nyimbo hizo zilifanya hadithi ziaminike kuliko hata sinema za kisasa ambazo zimetumia mamilioni ya dola kutengenezwa.

Muziki ni chombo kikubwa cha kuvutia biashara, biashara ya utangazaji, inategemea muziki, jaribu kufikiria matangazo ya redio au luninga bila muziki. Hata mtangazaji awe mzuri vipi, muziki ndio gundi ya kuwaweka watazamaji au wasikilizaji wabaki kufuatilia matangazo katika kituo. 

Kwa sababu ya nguvu hii ya muziki, wengine huhusisha hata na nguvu  za shetani, na kuna watu duniani ambao humuita shetani, kuwa ni mfalme wa muziki, kwani katika muziki mengi mabaya huweza kufanyika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *