UN yatoa tamko kufuatia amri ya jeshi la Sudan Kusini kuyataka mashirika ya kutoa misaada kuondoka AkoboUN yatoa tamko kufuatia amri ya jeshi la Sudan Kusini kuyataka mashirika ya kutoa misaada kuondoka Akobo

Katika taarifa yao ya pamoja iliyotolewa leo huko Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuratibu Misaada ya Kibinadamu OCHA, wamezisihi pande zote kujiepusha na shughuli za kijeshi katika maeneo yenye watu wengi na kutatua tofauti zao kupitia mazungumzo kwani watu wa Sudan Kusini wanahitaji amani.

Taarifa hiyo pia imewahimiza wadau wote kutimiza ahadi walizotoa wakati wa ziara ya hivi karibuni ya Mratibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Misaada ya Kibinadamu na Masuala ya Dharura, Tom Fletcher, ambaye pia ni Mkuu wa OCHA, za kuhakikisha ulinzi wa raia, wafanyakazi wa misaada pamoja na miundombinu yao. 

Mwanamke akiendesha kilimo Akobo Sudan Kusini kufuatia FAO kutoa mbegu za mboga mboga kwa wakazi.

Photo: FAO

Mwanamke akiendesha kilimo Akobo Sudan Kusini kufuatia FAO kutoa mbegu za mboga mboga kwa wakazi.

Maisha ya raia na sheria za Kimataifa

Eneo la Akobo kwa sasa ni makazi ya takriban watu 270,000, wakiwemo waliohamishwa makazi yao na wenyeji wanaotegemea misaada ya kibinadamu ili kuishi, ambapo zaidi ya nusu yao ni wanawake na watoto. Timu hiyo imetahadharisha kuwa shughuli yoyote ya kijeshi kwenye eneo lenye idadi hiyo kubwa ya watu, itasababisha janga kubwa la kibinadamu, huku kukiwa na ripoti za watu kuanza kukimbilia nchini Ethiopia na uporaji kuanza kujitokeza huko Akobo.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa raia hawapaswi kulengwa au kulazimishwa kuhama makazi yao bila hiari, na kwamba hatua yoyote lazima izingatie utu na sheria za kimataifa kwani tangu kuanza kwa mapigano mwezi Desemba 2025, eneo la Akobo limekuwa kimbilio muhimu kwa watu wanaokimbia ghasia kote jimboni Jonglei, na sasa kusitishwa kwa huduma za misaada kumeweka maisha ya maelfu ya watu rehani.

Timu hiyo imesisitiza kuwa itaendelea kupigania hatua madhubuti za kuokoa maisha ya watu walio kwenye mzozo huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *