Niliumia sana nilipoona wenzangu wanaenda shule, nami siendi – SanitaNiliumia sana nilipoona wenzangu wanaenda shule, nami siendi – Sanita

Kupitia video ya shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) nchini Tanzania, Sanita ni mkazi wa wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, kaskazini-magharibi mwa taifa hilo la Afrika Mashariki.

Ndoto yake ilikuwa akiwa mtu mzima awe muuguzi lakini kukatishwa masomo kumlitia machungu mno.

Usuli wa MEMKWA

Ingawa hivyo ndoto yake ilirejea tena kufokana na hatua za serikali ya Tanzania na wadau kupitia Mradi wa Elimu Kwa Waliokosa, au MEMKWA.

Mradi wa MEMKWA ulitambua kuwa zaidi ya watoto milioni 2 wenye umri wa kuwa shule ya msingi nchini Tanzania hawako shuleni hivyo serikali kwa kushirikiana na wadau UNICEF na serikali ya Qatar wakafanikisha MEMKWA na tangu mwaka 2022 zaidi ya watoto elfu 98 katika mikoa 3 ya Tanzania ikiwemo Kigoma, wamenufaika na MEMKWA.

Uwezo wa Sanita darasani; Mwalimu wake abainisha

Sanita alijiunga na darasa la 4 la shule ya msingi mwezi Januari mwaka 2025 ambapo Rashid ambaye ni mwalimu wake anasema, “ni mtoto ambaye alijiunga hapa shule tayari akiwa na malengo na matarajio yake. Anapenda kujibu maswali darasani, na anajikita kwenye malengo yake anayotaka kuyafikia. Alijiunga hapa akitokea MEMKWA akilenga kutimiza lengo la kuwa muuguzi ili hatimaye aweze kutibu na kusaidia watu.”

Sanita baada ya kujibu swali ubaoni na kupigiwa makofi kwa kuwa amepata jibu sahihi anasema mwalimu ni kama mlezi wake ambaye anamtegemea ili ampatie ushauri.

Kitendo cha Sanita kupata haki ya elimu kinamwezesha hata Rhoedesia ambaye ni mama mzazi wa Sanita kuwaza mustakabali wa binti yake akisema, “ninavyomuona mwanangu anaenda shule asubuhi ninajisikia faraja sana. Natamani na mimi mwanangu aende mbele ili apate kazi.”

MEMKWA inaondoa watoto mitaani

Mwalimu Rashid anatamatisha na tathmini ya mradi wa MEMKWA akisema “kwa kweli, MEMKWA ambayo imedhaminiwa na UNICEF imetusaidia kupunguza wimbi la watoto mitaani. Wengi wamekuja shule na kuipenda shule kwa sasa. Tunachoomba ni UNICEF waendelee kufadhili MEMKWA ili tuweze kuwavuta watoto wengi katika mfumo wa elimu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *