Alya Abu Shawish, mwanamke aliyeko mstari wa mbele kuondoa hatari ya mabomu Gaza Alya Abu Shawish, mwanamke aliyeko mstari wa mbele kuondoa hatari ya mabomu Gaza 

Hakika Gaza ni moja ya mazingira hatari duniani kwa sasa. Alya Abu Shawish anaposhuka kwenye gari kabla ya kuingia ofis iza UNMAS zilizoko Deir al-Balah katikatimwa Gaza, anavaa jaketi la kujikinga na risasi.

Ndani ya ofisi amesimama mbele ya ramani ya kidijitali, akifuatilia mienendo ya timu za wafanyakazi walioko mitaani zilizosambazwa kote katika ukanda huo wa Gaza ili kufanya kazi za kuondoa mabaki ya vilipuzi vya vita katika eneo hilo.

Baada ya mipango yote kukamilika ofisini, sasa Alya Abu anaendesha gari akiwa na wenzake kuelekea kazini nje ya ofisi. Anaeleza akisema,“kazi yangu kama mwanamke katika eneo hili inaonyesha kwamba wanawake wanaweza kuwa na nafasi muhimu katika kuhakikisha usalama na kuleta mabadiliko yanayoonekana, hata katika mazingira hatari na yenye changamoto kubwa zaidi katika Ukanda wa Gaza.”

Alya Abu Shawish anaonekana na wenzake mitaani wakifanya kazi. Watoto wanafuata, kwa vyovyote wakitambua kazi muhimu inayofanywa na UNMAS kufanya mazingira yawe salama dhidi ya vilipuzi.

Hata hivyo, nyuma ya dhamira hii ya kitaaluma kuna hadithi binafsi inaloakisi hali halisi ya maelfu ya wanawake huko Gaza.

“Kama mwanamke na mama, nimepitia changamoto nyingi ambazo wanawake wa Kipalestina huko Gaza hukabiliana nazo wakati wa vita hofu, kuhama makazi, uhaba wa mahitaji muhimu, na hali ya kutokuwa na uhakika kila wakati. Kama wanawake wengi hapa, nimelazimika kuilinda familia yangu huku nikikabiliana na hali hizi ngumu.” Anasema.

Bi Alya Abu Shawish akifafanua, kwenye ramani ya maingiliano, maeneo ya harakati ya timu za shamba katika ukanda wa Gaza.

Licha ya changamoto hizi, Alya Abu Shawish anasema uzoefu wake umeimarisha azma yake ya kuwasaidia wengine na kumhamasisha kufanya kazi katika uwanja ambao mara nyingi huonekana kutawaliwa na wanaume.

“Uzoefu huu haukunidhoofisha; uliimarisha azma yangu ya kuwasaidia wengine. Ulinitia moyo kufanya kazi katika masuala ya kuondoa mabomu na usalama na UNMAS uwanja ambao mara nyingi huonekana kuwa wa wanaume. Katika jukumu hili, ninachangia kupunguza hatari zinazosababishwa na mabaki ya vilipuzi vya vita na kusaidia jamii kuishi kwa usalama zaidi.”

Wanawake wengine katika timu za UNMAS pia hushiriki katika shughuli za kuhamasisha jamii kuhusu hatari za mabaki ya vilipuzi, ambayo sasa yamekuwa moja ya changamoto kubwa zaidi za kibinadamu huko Gaza kadri uharibifu unavyoendelea kuenea. Kwa Abu Shawish, juhudi hizi hubeba ujumbe unaokwenda mbali zaidi ya kazi kwani inaonesha uimara na mnepo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *