Dar es Salaam. Msanii kutoka lebo ya African Princess, Faustina Mfinanga maarufu Nandy ni miongoni mwa wageni walioalikwa kwenye tukio kubwa la mitindo duniani Paris Fashion Week linalofanyika katika jiji la Paris, nchini Ufaransa.
“Nina furaha kubwa kualikwa paris fashion week huu mwezi huko Paris . Kwakweli ni hatua kubwa kwenye mziki wangu.”anasema Nandy
Ziara hiyo ya kuonyesha mavazi na mitindo mbalimbali ilikuwa ya siku tatu huku Nandy akiwa msanii pekee kutoka Afrika Mashariki kualikwa.
Nandy anakuwa msanii wa pili kutoka Tanzania kualikwa kwenye onyesho hilo baada ya awali Diamond Platnumz (2024) kushuhudia matukio hayo yaliyomfungulia milango ya kimataifa.
Kwa mwaka huu wasanii kama Teyana Taylor, Anya Taylor-Joy, Willow Smith, Tyla, Paris Jackson na wengineo walikuwepo nchini humo ni sehemu inayokutanisha watu mashuhuri kutoka tasnia mbalimbali kama muziki, filamu na burudani. Mwananchi linakumegea mambo matano atakayonufaika mkali huyo wa kibao cha ‘Sweety’.
Kwanza kabisa, ziara hiyo inaweza kusaidia kuongeza umaarufu wa kimataifa kwa msanii huyo. Paris Fashion Week ni moja ya matukio makubwa ya mitindo duniani yanayohudhuriwa na mastaa, wanahabari na wadau wa burudani kutoka mataifa mbalimbali.
Hivyo, uwepo wa Nandy katika tukio hilo unampa nafasi ya kujitangaza kwa watu wapya ambayo huenda hawajawahi kusikia muziki wake au hata kukutana nao.
Kupitia mahojiano anayoendelea kuyafanya nchini humo, picha, video na machapisho ya mitandao ya kijamii, jina lake linaweza kuwafikia mashabiki wapya kutoka Ulaya, Marekani na sehemu nyingine duniani.
Hii ni kubwa kwa msanii yeyote anayetamani kuvuka mipaka ya Afrika Mashariki na kuingia kwenye soko la kimataifa.
Faida ya pili ya Nandy kuwepo kwenye tamasha hilo itampa fursa ya kupata kolabo na wasanii na maprodyuza wa muziki kutoka mataifa mbalimbali. Kwenye matukio hayo ni rahisi kukutana na wanamuziki, waandaaji wa muziki, mameneja au watu wanaosimamia majukwaa makubwa ya burudani.
Kukutana nao ana kwa ana inaweza kuwa fursa nzuri ya kuanzisha mazungumzo na kufanya kazi pamoja.Ikumbukwe Nandy amefanya kolabo nyingi na wasanii wa Afrika nyota kama Joeboy, Koffi Olomide, Sautisol.
Lakini kufanya kazi na wasanii wakubwa kimataifa inaweza kusaidia kuupeleka mziki wake duniani, kuongeza idadi ya wasikilizaji n ahata kumuwezesha kufanya maonyesho nje.
Ziara hiyo inaweza kumuongezea kujenga mtandao mkubwa wa watu katika tasnia ya burudani, kujuana na watu mbalimbali ni jambo muhimu kwa msanii.
Katika Paris Fashion Week hukutana na watu kutoka sekta ya mitindo, muziki, filamu, biashara na hata mambo ya urembo hivyo kukutana na watu kunaweza kumpa fursa Nandy ya kujenga uhusiano wa baadae unaoweza kuzaa matunda.
Mfano anaweza kupata mialiko ya kushiriki kwenye matamasha ya kimataifa, kushirikiana na brand kubwa au hata kupata usaidizi wa kusambaza muziki wake katika makubwa duniani.
“Nilipata nafasi ya kukutana na designer mkubwa paris Emmanuel Ungaro nimekuwa niki mfatilia kwa muda na kutamani kuvalishwa na yeye, tulikubaliana na kuunganisha brand zetu kwa pamoja.” anasema wakati alipokuwa nchini humo
KUKUZA CHAPA
Msanii anaposhiriki katika matukio makubwa kama Paris Fashion Week anajijengea heshima kwani kualikwa kwenye tukio hilo ni miongoni mwa mambo yanayoweza kukuza chapa yake.
Inaweza kuvutia makampuni mbalimbali ya nguo kama Balenciaga, Dior, Channel na nyinginezo ambazo zinashirikiana na tamasha hilo. Kwa Nandy inaweza kumpatia mikataba mipya ya udhamini, matangazo au miradi ya biashara itakayomuongezea minoti na kuimarisha kipato chake.
“Onyesho la siku ya pili ilikuwa poa sana tumejifunza na kuinjoi kila hatua naamini kila nilichokifanya kitaleta matokeo mazuri hata kama sio leo,” anasema Nandy.
Faida ya tano ni kupata inaweza kumsukuma mwanadada huyo kufanya ubunifu katika kazi zake za muziki.Ikumbukwe Ufaransa ni miongoni mwa nchini zinazojulikana kwa ubunifu wa Sanaa, mitindo na utamaduni. Kukutana na watu tofauti wenye mawazo mapya kunaweza kumpa Nandy hamasa ya kujaribu mitindo mipya ya muziki au kuongeza ubunifu katika kazi zake.
Mara nyingi wasanii hupata mawazo mapya wanapokutana na tamaduni na mazingira tofauti na yale waliyozoea.
Aidha, ziara hiyo inaweza kumsaidia kujifunza namna tasnia ya burudani inavyoendeshwa kwenye nchi zilizoendelea. Kwa kushuhudia jinsi matukio makubwa yanavyoandaliwa, jinsi brand zinavyojitangaza na jinsi wasanii wa kimataifa wanavyojitengeneza.
Kiujumla uwepo wa Nandy katika Paris Fashion Week ni hatua muhimu inayoweza kuleta manufaa makubwa katika safari yake ya muziki. Kupitia tukio hilo, anaweza kuongeza umaarufu kimataifa, kupata kolabo, kujenga mtandao wa wadau wa burudani, kukuza chapa yake na kupata msukumo wa ubunifu.
Ikiwa atatumia vizuri fursa hiyo, ziara yake katika jiji la Paris inaweza kuwa moja ya hatua kubwa katika kupeleka muziki wake kimataifa na kuendelea kuitangaza Tanzania katika ramani ya muziki duniani.
PARIS FASHION WEEK NI NINI?
Ni maonyesho makubwa ya mitindo ambapo wabunifu huonyesha makusanyo mapya ya nguo, viatu, mikoba na mitindo mbalimbali ambayo itavaliwa katika misimu ijayo. Maonyesho hayo mara nyingi hufanyika mara mbili kwa mwaka.
Tukio hilo lililoanzishwa mwaka 1973 hufanyika kila mwaka katika jiji la Paris, nchini Ufaransa na hukusanya wabunifu wakubwa wa mitindo, wanamitindo, mastaa wa muziki, waigizaji na wadau wa tasnia ya mitindo kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Ni sehemu ya matamasha manne makubwa ya mitindo duniani yanayojulikana kama ‘Big Four Fashion Weeks’, ambayo pia hufanyika katika miji ya New York, London, Milan na Paris.