Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa bidhaa nyingi zinazozlishwa nchini hazifiki sokoni kwa sababu hazina uthibitisho wa ubora na usalama ambapo kati ya asilimia 30 hadi 40 ya bidhaa hizo hazikidhi viwango vinavyohitajika.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa kitengo cha Chakula na Bioteknolojia wa Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania, (TIRDO), Dk Ivy Matoju, alipokuwa akielezea kuhusu maabara zao ambazo zimethibitishwa na Ithibati ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini Mwa Afrika (SADCAS) tangu mwaka jana (2025)
Kutokana na hilo, Dk Matoju amesema changamoto hiyo sasa inaweza kushughulikiwa kupitia maabara hizo zinazotumia vifaa vya kisasa ambazo zinazatambua na kupima kemikali hatarishi, ikiwa ni pamoja na viuatilifu hatari kwa matumizi ya binadamu
“Maabara hizi hupima virutubisho na kemikali kama protini, wanga, mafuta, vitamini, madini, na sumu kuvu , pamoja na uchambuzi wa bakteria na fangasi hatarishi kwenye bidhaa na hivyo kuhakikisha bidhaa zako zinakuwa salama, zenye ubora, na zinazoweza kushindana sokoni,”amesema Dk Matoju.
Anazitaja faida za kupima bidhaa kabla ya kwenda sokoni kuwa ni pamoja kuhakikisha kuzalisha bidhaa zenye ubora, huongeza imani ya wateja na kupanua soko ,kupunguza hatari za bidhaa zisizo salama na kuongeza ushindani sokoni.
Naibu Waziri Wizara ya Viwanda na Biashara Dennis Londo(Wa pili kutoka kulia ) akipata maelezo juu ya shughuli zinazofanyika katika maabara ya ngozi na nguo Kutoka Kwa Mhandisi Yusufu Sampuli. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO Profesa Mkumbukwa Madundo Mtambo.
Faida zingine ni wajasiriamali hupata ushauri wa kitaalamu wa kuboresha bidhaa zao utakaowasaidia kufikia viwango na kusajiliwa na mamlaka husika pamoja na upatinakanaji wa huduma kwa gharama inayoweza kumudu wajasiriamali wadogo na viwanda vya kati.
Kwa upande wake Mtaalam wa Maabara Mhandisi Francis Mawazo, amesema katika Maabara ya Mikrobiolojia ya Chakula wanapima_bakteria hatari na fangasi, ikiwemo Listeria monocytogenes, Salmonella spp., E. coli, familia ya bakteria Enterobacteriaceae, Chachu na Fangasi , Staphylococcus aureus, jumla ya Coliforms) na Total Plate Count (TPC).
“Pia katika Maabara ya Kemia ya Chakula tunapima virutubisho na kemikali hatarishi kwa kutumia GC MS na HPLC, ikiwemo protini, wanga, mafuta, vitamini, madini, sumu ya kuvu na viumbe vya wadudu,”amesema.
Mawazo anaongeza kuwa pamoja na upimaji wa kimaabara pia wanatoa Ushauri wa kitaalamu kwani matokeo ya vipimo hutoa mwongozo wa kisayansi kwa wajasiriamali kuboresha bidhaa zao na michakato ya uzalishaji.
Naye Mkuu wa Kitengo cha huduma za Shirika na Mipango, David Langa akiielezea TIRDO, amesema ni taasisi ya serikali iliyoanzishwa kwa lengo la kuendeleza sekta ya viwanda kupitia utafiti wa kisayansi, ubunifu wa teknolojia, na ushauri wa kitaalamu.
Langa amesema taasisi hii ina jukumu muhimu katika kusaidia maendeleo ya viwanda nchini Tanzania, hasa kwa kuunganisha utafiti wa kisayansi na mahitaji halisi ya viwanda vya ndani na kupitia shughuli zake mbalimbali, imekuwa nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa viwanda na kuongeza thamani ya rasilimaliza ndani.
Ametaja moja ya shughuli zake kuu ni kufanya utafiti wa kisayansi na kiteknolojia unaolenga kuboresha uzalishaji wa bidhaa viwandani ambapo taasisi hii huchunguza njia mpya za kutumia malighafi zinazopatikana nchini ili kuzalisha bidnaa bora na zenye ushindani katika soko la ndani na la kimataifa.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Balozi Waziri Rajab Saluma akiangalia Moja ya bidhaa ya COCOA inayozalishwa na vijana wanaohatamiwa katika Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda (TIRDO) alipotembelea shirika hilo hivi karibuni.
“Kwa mfano, TIRDO imekuwa ikifanya tafiti juu ya maturnizi ya mazao ya kilimo kama vile pamba, alizeti, na mazao ya misitu ili kutengeneza bidhaa za viwandani kama mafuta ya kula, sabuni, na vifaa vingine vya matumizi ya kila siku. Tafiti hizi husaidia kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi na kuongeza thamani ya rasilimali za ndani,”amesema Langa.