Chanzo cha picha, Getty Images
Waislamu wa Afrika Mashariki wataadhimisha Eid-ul-Fitr siku ya Ijumaa baada ya kuonekana kwa mwezi mpevu Alhamisi jioni, kuashiria kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Kaimu Kadhi Mkuu wa Kenya Sukyan Hassan alisema mwezi huo umeonekana katika maeneo kadhaa ya nchi, na uthibitisho wa kutosha kutoka Kaunti ya Kwale.
Tangazo hilo lilitolewa na Ofisi ya Kadhi Mkuu, kuthibitisha mwanzo wa mwezi wa Shawwal na kufikisha mwisho wa siku 29 za mfungo unaozingatiwa na waumini kote nchini.
Kuandamwma kwa mwezi huo kumethibitishwa nchini Tanzania na mataifa mengine ya waislamu wengi kama vile Saudia
Bwana Sukyan Hassan amesema mwezi huo umeonekana katika maeneo kadhaa ya nchi, na uthibitisho wa kutosha kutoka Kaunti ya Kwale.
“Mwezi mpevu unaoashiria mwanzo wa mwezi wa Shawwal umeonekana kwa mafanikio jioni hii katika maeneo mbalimbali nchini. Hasa, katika Kaunti ya Kwale, haswa eneo la Ramisi, watu watatu wamethibitisha kuwa wameuona kwa wakati ufaao.
Uaminifu wa watatu hao ulithibitishwa na imamu wa eneo hilo,” Sukyan alisema.
Ameongeza kuwa muandamo huo unakidhi matakwa ya Kiislamu yanayotumika kubainisha mwisho wa Ramadhani.
“Mwezi wa Ramadhani umefika mwisho, na kesho itakuwa siku ya kwanza ya Shawwal na siku ya Eid-ul-Fitr,” alisema.
Eid-ul-Fitr ni moja ya sherehe muhimu zaidi katika kalenda ya Kiislamu, kuashiria hitimisho la Ramadhani, mwezi mtukufu ambao Waislamu hufunga kuanzia alfajiri hadi jioni, hushiriki katika sala, na kutekeleza vitendo vya hisani.