
Dar es Salaam. Katika kusherehekea miaka 50 ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Taifa linatafakari safari ndefu ya mafanikio iliyochagiza ukuaji wa sekta ya biashara na uwekezaji, huku ikifungua milango ya masoko ya kimataifa kwa bidhaa za Tanzania.
Tangu kuanzishwa kwake, TanTrade imeendelea kuwa mhimili mkuu wa kukuza biashara ya ndani na nje ya nchi, ikijenga daraja kati ya wazalishaji wa ndani na wanunuzi wa kimataifa. Kupitia juhudi hizo, mamlaka hiyo imekuwa chachu ya kuimarisha matumizi ya nembo ya Taifa ‘Made in Tanzania’, hatua iliyoongeza thamani na heshima ya bidhaa za ndani katika soko la dunia.
Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Mkurugenzi wa TanTrade, Dk Latifa Mohamed Hamisi, amesema safari ya miaka 50 si tu ushuhuda wa ukuaji wa sekta ya biashara, bali pia ni alama ya mshikamano wa kitaifa na dira ya maendeleo ya uchumi.
“Katika kipindi hiki chote, TanTrade imekuwa jukwaa la kuwaunganisha wazalishaji na masoko ya kimataifa, na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa Taifa,” amesema.
Sabasaba chachu ya mafanikio ya TanTrade
Moja ya mafanikio makubwa ya TanTrade ni kuendeleza Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba, ambayo yamejijengea heshima kubwa ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Dk Latifa, maonyesho hayo yamekuwa yakihusisha mamia ya kampuni kila mwaka, yakitoa fursa kwa wazalishaji wa ndani kutangaza bidhaa zao, kupata masoko mapya na kujifunza mbinu bora za biashara.
“Sabasaba si tu maonyesho, bali ni alama ya Taifa letu. Yamekuwa yakionyesha ubunifu wa Watanzania katika sekta mbalimbali, kuanzia kilimo hadi viwanda na huduma,” ameeleza.
Ameongeza kuwa kupitia maonyesho hayo, Tanzania imefanikiwa kuongeza mauzo ya nje, kuimarisha ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Aidha, TanTrade imefanikisha upanuzi wa masoko ya bidhaa za Tanzania kupitia ushiriki wa wafanyabiashara katika maonesho ya kimataifa katika nchi mbalimbali, zikiwamo Oman, China, Indonesia na Msumbiji. Hatua hiyo imewezesha bidhaa za Tanzania, hususan za kilimo na viwanda vidogo, kupata nafasi katika masoko mapya na kuongeza ushindani wake kimataifa.
Dk Latifa amesema mikataba ya kibiashara iliyopatikana kupitia majukwaa hayo imeongeza thamani ya mauzo ya nje na kuimarisha ajira kwa vijana na wanawake.
Katika kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia, TanTrade imeanza kutumia mifumo ya kidijitali kurahisisha huduma zake, ikiwamo usajili wa washiriki wa maonyesho ya Sabasaba. Mfumo huo umeondoa changamoto za usajili wa awali na kuongeza uwazi, huku ukirahisisha mawasiliano kati ya mamlaka na wadau wa biashara.
“Tunakwenda sambamba na dunia ya kidigitali ili kuhakikisha wafanyabiashara wanapata huduma kwa urahisi na kwa ufanisi zaidi,” amesema Dk Latifa.
Katika kuimarisha utambulisho wa Taifa, TanTrade imeendelea kuhamasisha matumizi ya nembo ya ‘Made in Tanzania’, ambayo imekuwa kichocheo cha uzalendo wa kiuchumi. Kupitia kampeni hiyo, wananchi wamehamasika kutumia bidhaa za ndani, huku wazalishaji wakiongeza ubora wa bidhaa zao ili kushindana katika masoko ya kimataifa.
Kwa miaka 50, TanTrade pia imefanikiwa kuunganisha Tanzania na masoko ya kikanda na kimataifa, hatua iliyoongeza fursa za biashara na uwekezaji. Kupitia ushirikiano huo, Tanzania imeimarisha nafasi yake katika biashara za Afrika Mashariki, Kusini mwa Afrika pamoja na masoko ya Asia na Ulaya, na hivyo kuongeza uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje na ajira.
Mafanikio hayo pia yamehusishwa na uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kuweka mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji kupitia sera za uwazi na diplomasia ya kiuchumi.
“Uongozi wa Rais Samia umeleta msukumo mkubwa katika kukuza sekta binafsi na kuongeza thamani ya bidhaa za Tanzania,” amesisitiza Dk Latifa.
Katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya jubilei ya dhahabu, TanTrade imetoa wito kwa wafanyabiashara, wawekezaji na wananchi kushiriki kikamilifu katika maonesho ya Sabasaba ya mwaka huu, Dk Latifa akisisitiza kuwa ni fursa ya kuonyesha bidhaa na huduma, kujenga mitandao ya kibiashara na kupata masoko mapya.