
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema inaonekana kuwa umewadia wakati wa kutekeleza mpango unaofuata uliopangwa hapo awali kwa ajili ya mashambulizi zaidi dhidi ya Israel.
Shirika la habari la Mehr limeandika kuwa Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Mohammad Qalibaf ametuma ujumbe kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii akisema: Kama utawala wa Israel umeshindwa kuzuia makombora ya Iran kupiga eneo lenye ulinzi mkubwa sana la Dimona, hii katika mtazamo wa kioperesheni ina maana ya kuingia katika awamu mpya ya vita: Anga ya Israel haina ulinzi.
Spika Qalibaf amesisitiza kuwa: Matokeo ya hayo yote ni kwamba, inaonekana umewadia wakati wa kutekeleza mpango unaofuata uliopangwa hapo awali.
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ametuma ujumbe huo baada ya majeshi ya Iran kufanya mashambulizi makubwa dhidi ya taasisi za nyuklia za Dimona kulipiza kisasi shambulizi lililofanywa kabla yake na utawala ghasibu wa Israel katika kituo cha kurutubisha urani cha Natanz nchini Iran. Makumi ya Wazayuni wanaripotiwa kuuawa au kujeruhiwa katika mashambulizi ya Iran dhidi ya taasisi hizo.
Katika muktadha huo, muda mfupi baada ya mashambulizi ya Iran dhidi ya taasisi za nyuklia za Dimona, mwandishi habari mashuhuri wa Marekani, Glen Greenwald, ametuma ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X akisema: Kwa sababu mbalimbali, Dimona inahesabiwa kuwa mojawapo ya maeneo muhimu sana ya kistratijia ya Israel.
Ameongeza kuwa: Iwapo Israel imeshindwa kuzuia hata kombora moja kati ya makombora yaliyotumiwa kushambulia kituo hicho, hii ni ishara ya wazi ya udhaifu mkubwa wa mfumo wa ulinzi wa anga wa utawala huo; haya ni mabadiliko ambayo yalikuwa tayari yameripotiwa sana hapo awali.