Katika ujumbe wake wa siku hii, Katibu Mkuu amesema kuwa ukosefu wa huduma hizo una athari kubwa mbayá kwa wanawake na wasichana, ambao hulazimika kutumia vyoo visivyo salama, kutunza wagonjwa wanaougua kutokana na kutumia maji machafu, na kutumia muda mwingi kutafuta maji.
“Hali hii inachangia baadhi ya wasichana kushindwa kuhudhuria masomo,” amesema Guterres.
Kunakotiririka maji, usawa nao hushamiri
Akinukuu kaulimbiu ya mwaka huu, “Kunakotiririka maji, usawa nao hushamiri,” Katibu Mkuu amesisitiza umuhimu wa uwekezaji zaidi katika miundombinu ya maji na huduma za usafi.
Amezitaka serikali kuboresha mifumo ya usambazaji, kuimarisha mafunzo kwa wataalamu, na kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali za kifedha kwa miradi husika.
Bonde la Rio Provaz ni chanzo kikuu cha maji katika mji wa Neves huko São Tomé na Príncipe.
Nchi zilizoendelea zina wajibu
Na kwa nchi zilizoendelea, “zisaidie juhudi za kimataifa kwa kutoa teknolojia, utaalamu na ufadhili ili kujenga mifumo salama, endelevu na yenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za baadaye.”
Amesisitiza pia umuhimu wa kuwashirikisha wanawake katika ngazi zote za maamuzi ili kuhakikisha huduma hizo zinakidhi mahitaji halisi ya jamii.
Maji yanaweza kuwa nyenzo ya kujenga ushirikiano
Katibu Mkuu amesema licha ya maji kuwa chanzo cha migogoro katika baadhi ya maeneo, rasilimali hiyo hiyo inaweza pia kuwa nyenzo ya kuleta ushirikiano na amani.
Amekumbusha kuwa Mkutano ujao wa Umoja wa Mataifa kuhusu maji unatarajiwa kuleta pamoja wadau wa kimataifa ili kuharakisha juhudi za kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na huduma za usafi kwa wote.
Katibu Mkuu amehitimisha kwa wito wa mshikamano wa kimataifa, akisisitiza kuwa” maji yanaweza kuwa kichocheo cha usawa wa kijinsia na maendeleo endelevu iwapo yatatumika kwa njia jumuishi na yenye haki.”
Kauli ya UN kupitia ukurasa mahsusi wa siku ya maji duniani |
|
Selin Al-Dada, mtoto kutoka Gaza, anajaza maji ya kunywa kwenye galoni ya plastiki.
Je wajua?
- Duniani kote, zaidi ya wanawake bilioni 1 – ikiwa ni zaidi ya robo ya wanawake wote duniani – hawapati huduma ya maji safi na salama yanayosimamiwa na huduma za utoaji maji (UN Women/UNDESA, 2023)
- Watu bilioni 1.8 duniani hawana maji safi ya kunywa kwenye maeneo yao, na katika kaya 2 kati ya 3, wanawake ndio wana jukumu la msingi la kutafuta maji. (WHO/UNICEF, 2023)
- Katika nchi 53 ambako takwimu zimepatikana, wanawake na wasichana hutumia saa milioni 250 kwa siku kusaka maji – ikiwa ni zaidi ya mara tatu ya wanaume na wavulana. (UN Women/UNDESA, 2024)
- Duniani kote, maji yasiyo salama, ukosefu wa huduma za kujisafi kila siku husababisha vifo vya watoto 1,000 wenye umri wa chini ya miaka 5. (WHO, 2023)
- Takribani asilimia 14 ya nchi duniani bado hazina mifumo ya kuhakikisha wanawake wanashiriki kwa usawa kwenye kupitisha uamuzi kuhusu usimamizi wa maji. (UNEP-DHI, GWP, UN Women, 2025)