Dar es Salaam. Heshima zimekuwa zikimiminika kutoka pande zote za dunia kwa Chuck Norris, mtaalamu wa muvi ya kivita na mapigano kutoka Hollywood ambaye alifariki akiwa na umri wa miaka 86.
Taarifa yake ya kuumaliza mwendo ilitangazwa juzi, Ijumaa kwa Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki huku ikiwa Alhamisi kwa Marekani na familia yake ambayo ilisema sababu za kifo angependa ibaki kuwa siri.
“Kwa huzuni kubwa mioyoni mwetu, familia yetu inatangaza kifo cha ghafla cha mpendwa wetu Chuck Norris kilichotokea asubuhi (Alhamisi).”
Taarifa hiyo ya familia iliendelea kwa kusema: “Ingawa tungependa kubaki faragha kuhusu mazingira ya kifo chake, tafadhali fahamuni kwamba alikuwa amezungukwa na familia yake na alikuwa katika hali ya amani.”
Binti yake, Danilee Norris, anasema: “Labda alionekana kama shujaa, lakini moyo wake ulikuwa umejaa upendo.”
Mwigizaji na mtaalamu wa sanaa za mapigano huko Sweden, Dolph Lundgren aliyeshirikiana naye anasema kupitia mtandao wake wa kijamii: “Daima niliyeangalia Chuck kama mfano wa kuigwa.”
Kwa upande wake mwigizaji wa Marekani, Sylvester Stallone maarufu kama Rambo, aliongeza: “Chuck Norris alikuwa ‘All American’ (mtu mwenye utu na tabia nzuri) kwa kila upande.”€
Akiungana na mastaa wakubwa duniani kote, mwigizaji na nyota wa filamu nchini, Hussein Lugendo ‘Mlilo’ ambaye ni mume wa Shamsa Ford amepokea kwa masikitoko msiba huo akimuongelea Chuck kama mfano katika sanaa.
“Nakumbuka katika makuzi yangu ni kati ya wasanii ambao nilikuwa navutiwa na kazi yake, movi zake nyingi za kivita nimetazama,” anasema.
Katika miaka ya 1980, Chuck alijizolea umaarufu kupitia filamu kama The Delta Force na Missing in Action, akijijengea jina kama shujaa asiyeogopa chochote.
Baadaye, alizidi kung’ara kupitia kipindi maarufu cha televisheni Walker, Texas Ranger, ambapo alicheza kama askari.
Nyuma ya kamera, Chuck Norris alikuwa alikuwa mtaalamu wa mapigano akiwa na mikanda myeusi kadhaa.
Umahiri wake ulimfanya aheshimiwe duniani kote na mwaka 1989 alitunukiwa nyota kwenye Hollywood Walk of Fame heshima kubwa kwa mchango wake.
Maisha yake pia yaligusa historia ya sanaa ya mapigano kupitia urafiki wake wa karibu na Bruce Lee.
Wawili hawa walifanya mazoezi pamoja na baadaye wakaonekana katika filamu ya The Way of the Dragon, pambano lao likibaki kuwa moja ya matukio ya kukumbukwa zaidi katika historia ya filamu.
Hata baada ya kupunguza uigizaji, Chuck hakuwahi kupotea mioyoni mwa watu. Alibaki kuwa gumzo mitandaoni kupitia hadithi za utani kuhusu nguvu zake.
Siku chache kabla ya kifo chake, alionekana mwenye furaha akisherehekea siku yake ya kuzaliwa ya miaka 86, akionesha kuwa bado alikuwa na nguvu na roho ile ile ya ushindi.
Alizaliwa mwaka 1940 huko Oklahoma na kabla ya umaarufu, alilitumikia jeshi la anga la Marekani.
Katika maisha yake, alijenga familia na kuacha watoto watano. Leo, dunia inamuaga shujaa wa kweli aliyewahamasisha wengi kuishi kwa ujasiri. Pumzika kwa amani, Chuck Norris aliyoyafanya yataendelea kuishi.