Dar es Salaam. Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na utabiri wa hali ya hewa ili kupunguza athari za majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi na kulinda maisha ya wananchi pamoja na mali zao.

Hatua inakuja wakati Tanzania ikiungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani leo Jumatatu, Machi 23, 2026.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema kaulimbiu ya mwaka huu, “Observing Today, Protecting Tomorrow” (Kuangalia Leo, Kulinda Kesho), inalenga kusisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya uangalizi wa hali ya hewa, maji na tabianchi.

Amesema uwekezaji katika mifumo hiyo ni muhimu ili kuongeza uwezo wa nchi kukabiliana na hatari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi ambazo zimekuwa zikiongezeka kwa kasi duniani.

“Ni muhimu kuendelea kuwekeza katika mifumo ya uangalizi wa hali ya hewa ili kuongeza uwezo wa nchi kukabiliana na majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi,” amesema Profesa Mbarawa.

Amefafanua kuwa taarifa sahihi na za wakati za hali ya hewa ni msingi wa maamuzi katika sekta mbalimbali zikiwamo uchukuzi, kilimo, maji, nishati, afya, ujenzi na miundombinu.

Akinukuu takwimu za World Meteorological Organization, amesema kati ya mwaka 1970 na 2021 majanga ya hali mbaya ya hewa yalisababisha hasara ya dola trilioni 4.3 na vifo vya karibu watu milioni mbili duniani, huku zaidi ya asilimia 90 ya madhara hayo yakitokea katika nchi zinazoendelea.

Amesema hali hiyo inaonyesha umuhimu wa kuimarisha mifumo ya tahadhari za mapema ili kupunguza athari za majanga hayo.

Aidha, amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya hali ya hewa, ikiwamo matumizi ya teknolojia mpya kama akili bandia, ili kuboresha usahihi wa taarifa.

“Uwekezaji katika huduma za hali ya hewa si gharama bali ni uwekezaji katika usalama wa taifa na ustahimilivu wa uchumi,” amesema.

Amesema pia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imetambua mabadiliko ya tabianchi kuwa miongoni mwa hatari kubwa kwa ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi.

Profesa Mbarawa amesema chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Serikali imeboresha huduma za hali ya hewa ikiwamo ujenzi wa Kituo cha Kalibu za Vifaa vya Hali ya Hewa jijini Dar es Salaam na ununuzi wa vituo vya kisasa vya kupima hali ya hewa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tanzania Meteorological Authority, Ladislaus Chang’a amesema maadhimisho ya mwaka huu yanaenda sambamba na miaka 76 tangu kuanzishwa kwa WMO mwaka 1950, huku Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi wanachama 193.

Amesema Serikali imewekeza katika miradi mbalimbali ikiwamo ujenzi wa jengo la Kanda ya Mashariki, Kituo cha Tahadhari ya Tsunami na Kituo cha Kalibu za Vifaa vya Hali ya Hewa ili kuongeza usahihi wa utabiri.

Chang’a amesema pia rada tano za hali ya hewa tayari zimefungwa katika mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam, Mtwara, Kigoma na Mbeya kati ya saba zilizopangwa, sambamba na uwekaji wa mifumo ya kisasa katika viwanja vya ndege na vituo vya kupima hali ya hewa.

Ameongeza kuwa matumizi ya teknolojia za kidijitali na akili bandia yameongeza ufanisi wa utoaji wa huduma, huku wataalamu 15 wa Tanzania wakishiriki katika kamati mbalimbali za kimataifa za WMO na Intergovernmental Panel on Climate Change.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *