
Dar es Salaam. Wakati biashara ndogo na za kati (SMEs) zikiendelea kukumbana na changamoto ya upatikanaji wa mitaji, Benki ya Exim Tanzania imezindua jukwaa jipya la kidijitali la ufadhili wa mnyororo wa ugavi, ‘Exim Supply Chain’, likilenga kutoa suluhisho la haraka na nafuu kwa wafanyabiashara.
Uzinduzi huo uliofanyika Machi 19, 2026 jijini Dar es Salaam, unakuja wakati wafanyabiashara wengi wakikabiliwa na vikwazo vinavyohusisha mapengo ya mtiririko wa fedha (cash flow), gharama kubwa za mikopo na mifumo isiyounganishwa vizuri kati ya wadau wa biashara.
Kupitia jukwaa hilo jipya, wateja wanaweza kuwasilisha maombi ya ufadhili kwa njia ya mtandao na kupokea fedha ndani ya takribani dakika 15 baada ya kukamilisha taratibu zote.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Ofisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya Exim Tanzania, Shani Kinswaga, amesema suluhisho hilo ni sehemu ya mkakati wa benki hiyo kutumia teknolojia kutatua changamoto za biashara.
“Uzinduzi wa ‘Exim Supply Chain’ unaonesha dhamira yetu ya kutumia teknolojia kutatua changamoto halisi za biashara. Mfumo huu utawawezesha wafanyabiashara kupata mitaji kwa haraka, kupunguza presha ya mtaji wa uendeshaji na kuimarisha uhusiano kati ya wanunuzi na wasambazaji,” amesema.
Kwa mujibu wa benki hiyo, jukwaa hilo linatoa huduma mbalimbali za kifedha ikiwemo ufadhili kwa wasambazaji, ufadhili wa malipo (payable finance), ufadhili wa LPO, ufadhili kwa wasambazaji wa bidhaa pamoja na huduma ya factoring ya ankara.
Meneja Mwandamizi wa Uendeshaji na Utoaji Huduma wa Trade Finance, Innocent Buzoya, amesema mfumo huo umeundwa mahsusi kupunguza ucheleweshaji wa upatikanaji wa mitaji kwa biashara.
“Tumebuni suluhisho hili ili kushughulikia vikwazo vinavyokwamisha biashara kupata ufadhili. Mfumo huu wa kidijitali unapunguza muda wa uchakataji na kusaidia biashara kuendesha shughuli zake kwa ufanisi zaidi,” amesema.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Miamala ya Kibenki, Ishaq Samailla, amesema huduma hiyo itasaidia kujenga uaminifu na kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya wadau wa mnyororo wa ugavi.
“Wasambazaji na watoa huduma sasa wanaweza kupata mitaji kwa wakati bila masharti magumu, jambo litakalosaidia kukuza biashara na kuimarisha mzunguko mzima wa ugavi,” amesema.
Benki ya Exim Tanzania imeeleza kuwa huduma hiyo inapatikana katika matawi yake pamoja na kupitia Kitengo cha Trade Finance, huku ikiwahimiza wafanyabiashara kujitokeza kunufaika na fursa hiyo mpya inayolenga kukuza uchumi kupitia ujumuishi wa kifedha.