Asante Assumpta, kwa mujibu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa mzozo huu unaoendelea Mashariki ya Kati umeathiri kila Nyanja ya maisha katika Ukanda huo na sasa umevuka mipaka na Kwenda mbali zaidi ikiwemo barani Asia na Afrika hasa katika siuala la biashara na usafirishaji.

Taarifa iliyotolewa leo na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Miradi na Huduma UNOPS inaonya kuwa mamilioni ya watu duniani wako hatarini, wakati kutokana na madhara makubwa ya kibinadamu na kiuchumi yanayovuka mipaka ya eneo la mzozo.

Mkurugenzi wa shirika hilo, Jorge Moreira da Silva, amesema kuwa kuvurugika kwa njia muhimu za usafirishaji hasa kupitia Mlango Bahari wa Hormuz kumesababisha mshtuko mkubwa katika masoko ya kimataifa.

“Nchi zinazoendelea barani Asia na Afrika zina uwezekano mkubwa wa kubeba gharama kubwa zaidi. Kuvurugika kwa Mlango wa Hormuz kunahatarisha usambazaji wa nishati na masoko ya mbolea yanaathirika, hali inayotishia uhakika wa chakula katika nchi ambazo tayari zinakabiliwa na njaa au ukosefu wa chakula.”

Ameongeza kuwa idadi ya watu wanaoishi katika njaa duniani pia inaweza kuongezeka kwa “makumi ya mamilioni katika miezi ijayo”.

Pia amesema mgogoro huu unazidisha hali mbaya iliyopo katika nchi kama Sudan, Sudan Kusini, Afghanistan, Yemen, na Somalia, ambapo mifumo ya chakula tayari ni dhaifu

media:entermedia_image:dc0562d1-6a81-474c-8c69-658639f88791

Meli ikisafirisha makontena ya mafura baharini

Mashambulizi dhidi ya meli

Mashambulizi dhidi ya meli na kuvunjika kwa minyororo ya usambazaji kunazuia upatikanaji wa bidhaa muhimu, ikiwa ni pamoja na dawa na misaada ya kibinadamu hasa katika Ukanda wa Gaza.

Moreira da Silva ameonya kuwa “Vita vinavyoweza kuenea katika Ghuba ya Uajemi vinaweza pia kuhatarisha mtiririko wa fedha zinazotumwa nyumbani, hasa kuelekea Asia Kusini.”  

Nchini Lebanon,kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhuduia watoto UNICEF  gharama ya kibinadamu inaendelea kuongezeka kwa kasi kwani zaidi ya watu 1,000 wameuawa na wengine zaidi ya 2,500 kujeruhiwa tangu mapema mwezi huu wa Machi.

Miongoni mwa waliopoteza maisha ni wafhudumu wa misaada, waandishi wa habari, na tkriban wahudumu 31 wa afya.

Watoto wanabeba gharama kubwa

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Ted Chaiban, ametoa tathmini nzito kuhusu athari kwa watoto akisema “Kuongezeka kwa mapigano hivi karibuni kumesababisha kuuawa au kujeruhiwa kwa idadi ya watoto inayolingana na darasa moja kila siku.”

UNICEF imeongeza kuwa mbali na athari za kimwili, vita hivi vina athari kubwa za kisaikolojia, hasa kwa watoto na wahudumu wa misaada wa ndani.

Hofu, kukimbia makazi yao, na kushuhudia vurugu mara kwa mara kunawaacha wengi na majeraha ya muda mrefu ya kiakili, huku shughuli za misaada zikikabiliwa na changamoto kubwa.

Katika Ukanda wa Gaza, hali inaendelea kuwa mbaya huku raia wakikabiliwa na mashambulizi ya anga, mabomu, na risasi.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada kwa Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limesema mamia ya watu wamepata majeraha ya kudumu, wengi wao wakibaki na ulemavu wa maisha. Upatikanaji wa huduma za hospitali, ufikiaji wa vituo vya Umoja wa Mataifa, mashamba, na miundombinu ya umma umewekewa vikwazo vikubwa.

Kituo cha umeme cha nyuklia cha Iran chini ya ujenzi, kikiwa na jengo kubwa lenye umbo la nguzo, lililozungukwa na uzio wa usalama na minara ya ufuatiliaji.

© IAEA/Paolo Contri

Mtambo wa nyuklia ulioko Bushehr nchini Iran.

Hofu ya usalama wa nyuklia yaongezeka

Mgogoro huu pia umeibua wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wa nyuklia kufuatia ripoti za mashambulizi karibu na vituo nyeti vya nyuklia nchini katika Iran na Israel.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Nishati ya Atomiki IAEA, Rafael Grossi, amesisitiza hatari zilizopo akisema“Hatua yoyote ya kijeshi haipaswi kuhatarisha uadilifu wa kimwili na usalama wa vituo vya nishati ya nyuklia na wafanyakazi wake.”

Ingawa hakuna ongezeko la viwango vya mionzi lililoripotiwa hadi sasa, mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nyuklia yanachukuliwa kuwa tishio kubwa kwa afya ya umma na mazingira.

Mifumo ya afya yajitayarisha kwa hali mbaya zaidi

Kwa upande wake Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO,  tayari limeanza maandalizi ya dharura kwa uwezekano wa matukio ya nyuklia, ikiwafundisha wafanyakazi wake na wa Umoja wa Mataifa katika nchi 13 namna ya kukabiliana na hatari za afya ya umma.

Kadri vita vinavyoendelea, mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaonya kuwa mchanganyiko wa hatari za kibinadamu, kiuchumi na kimazingira unaweza kusababisha mgogoro mkubwa wa kimataifa wenye athari za muda mrefu.

Moreira da Silva amesisitiza kuwa “Dunia haiwezi kumudu kuongezeka zaidi kwa mzozo huu,”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *