Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, katika mazungumzo ya simu na Waziri Mkuu wa Pakistan, ameonya kuhusu malengo hatari ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kupanua vita hadi nchi nyingine za kanda.

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, na Waziri Mkuu wa Pakistan, “Shehbaz Sharif,” walibadilishana maoni kuhusu maendeleo ya kikanda na athari za uchokozi wa kijeshi uliofanywa dhidi ya Iran na utawala wa Kizayuni pamoja na Marekani, katika mazungumzo ya simu yaliyofanyika Jumamosi.

Katika mazungumzo hayo, Rais wa Iran alieleza masikitiko yake kuhusu matumizi ya ardhi ya baadhi ya nchi za Kiislamu katika mashambulizi dhidi ya Iran, na akasisitiza: “Hatua ya Iran kujilinda dhidi ya chanzo cha mashambulizi haya ni jambo la kawaida. Hata hivyo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huzichukulia nchi za Kiislamu kuwa ndugu zake, na haitamani hata Mwislamu mmoja apate madhara.”

Amesisitiza pia kwamba utawala wa Kizayuni una nia mbaya ya kupanua vita hadi nchi za kanda, na akaonya kuwa nchi za Kiislamu zinapaswa kuwa makini ili ardhi zao zisitumike na wavamizi kufanya mashambulizi dhidi ya nchi nyingine za Kiislamu.

Pezeshkian ameashiria uhusiano wa pamoja wa kidini na kibinadamu kati ya nchi za Kiislamu, alisema kuwa kuna uwezo mkubwa miongoni mwa nchi za Kiislamu wa kukabiliana na vitisho vya pamoja, hasa uchokozi wa utawala wa Kizayuni.

Waziri Mkuu wa Pakistan, katika mazungumzo hayo, amesisitiza tena msimamo wa kimsingi wa nchi yake wa kulaani uchokozi wa kijeshi dhidi ya Iran. Amesisitiza hasa kulaaniwa vikali kwa mashambulizi ya hivi karibuni ya utawala wa Kizayuni dhidi ya miundombinu ya kiuchumi ya Iran, na akathibitisha mshikamano kamili wa serikali na wananchi wa Pakistan na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *