Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu (OCHA), watu saba waliuawa na makumi kujeruhiwa wakati shambulio la anga lilipopiga mkusanyiko wa mazishi katika Milima ya Nuba, West Kordofan, Ijumaa iliyopita, kutokana na vyanzo vya ndani vya habari.
Vita hivyo, vilivyoanza Aprili 2023 kati ya wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka RSF, na Jeshi la serikali ya Sudan SAF, vinaendelea kuwa na athari kubwa na za kutisha kwa raia.
Shambulio hilo kwenye mazishi linafuatia shambulio la ndege zisizo na rubani droni kwenye Hospitali ya Mafunzo katika mji mkuu wa Darfur Mashariki, Al Deain, lililosababisha vifo vya watu 70 tarehe 20 Machi.
Kutokuwepo kwa usalama kunaendelea kuzilazuimisha familia kuhama makazi yao katika eneo la West Kordofan, limesea Shirika laUmoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM).
Katika jimbo jirani la Kordofan Kusini, mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na mapigano katika mji wa Dilling yameripotiwa kusababisha vifo vya watu watatu Jumamosi, huku mashirika ya kiraia yakionya kuwa hali ya kibinadamu inazidi kuzorota kwa kasi.
Kikosi cha pamoja cha Umoja wa Mataifa kinachoongozwa na WFP, UNICEF na UNDP kimetoa misaada muhimu kwa jamii zilizotengwa katika majimbo ya Kordofan Kusini nchini Sudan.
Upatikanaji wa misaada waathirika
Mapigano yanayoendelea na mashambulizi ya mara kwa mara ya ndege zisizo na rubani pia yanavuruga njia muhimu za usambazaji katika eneo la Kordofan.
Barabara kuu zinazounganisha mji wa El Obeid katika jimbo la Kordofan Kaskazini na miji ya Dilling na Kadugli katika jimbo la Kordofan Kusini zinazidi kuwa hatari, hali ambayo inaathiri moja kwa moja usafirishaji wa misaada ya kibinadamu na bidhaa za kibiashara.
“Masharti ya kiutawala yanaongeza changamoto hizi,” amesema msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Stéphane Dujarric, “huku shughuli muhimu za matibabu huko El Obeid zikiwa zimesimamishwa kwa karibu mwezi mmoja sasa.”
Wakati huo huo, katika eneo la Darfur, kuongezeka kwa ukosefu wa usalama na vikwazo kwa harakati za misaada kunadhoofisha zaidi upatikanaji wa misaada ya kibinadamu.
Wafanyakazi wa misaada wanakabiliwa na uporaji wa kutumia silaha na mashambulizi katika njia kuu, huku baadhi ya mashirika yakilazimika kusitisha kabisa shughuli zao, na kuwaacha watu walio katika mazingira hatarishi wakiwa na huduma chache zaidi.
Familia za wakimbizi kutoka Kordofan huosha nguo katika kituo cha mapokezi katika Jimbo la Gedaref.
Mapigano karibu na mpaka wa Ethiopia
Vivyo hivyo, kuongezeka kwa mapigano karibu na mpaka wa Ethiopia katika jimbo la Blue Nile kumezuia kwa kiasi kikubwa shughuli za misaada ya kibinadamu. Harakati nje ya mji mkuu wa jimbo hilo, Ed Damazine, kwa kiasi kikubwa zimesimamishwa, na hivyo kukata upatikanaji wa kuwafikia watu wanaohitaji msaada.
Kutokana na kuongezeka kwa ukosefu wa usalama, katika siku za hivi karibuni zaidi ya watu 1,600 wamekimbia makazi yao katika eneo la Geisan, jimbo la Blue Nile, kwa mujibu wa shirika hilo la uhamiaji IOM.
Licha ya changamoto hizi, Umoja wa Mataifa na washirika wake wanaendelea kutoa msaada nchini Sudan. Mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, OCHA, amesisitiza kuwa raia lazima walindwe wakati wote, kama inavyotakiwa na sheria za kimataifa za kibinadamu.
Bw. Dujarric aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano wa mchana Jumatatu kwamba “Mashambulizi dhidi ya raia na miundombinu muhimu lazima yasitishwe,”
Ameongeza kuwa “Tunarudia wito kwamba pande zote lazima zihakikishe upatikanaji wa haraka, salama, usiozuiliwa na usio na vikwazo wa misaada ya kibinadamu, ikiwemo katika njia zote muhimu na popote msaada unapohitajika.”