Katika taarifa yake, shirika hilo limesema ombi hilo la ufadhili linakusudia kuimarisha mifumo ya kibinadamu, kuongeza msaada wa kuvuka mipaka, kurejesha huduma za msingi na kusaidia jamii zilizoathirika kujijenga upya.

Mzozo wa muda mrefu waathiri mamilioni

IOM imeeleza kuwa tangu kuanza kwa mzozo mwezi Aprili 2023, zaidi ya watu milioni 12 wamelazimika kuyahama makazi yao, huku takribani milioni 9 wakiwa bado hawajarejea nyumbani. Aidha, karibu watu milioni 33.7 wanahitaji msaada wa kibinadamu wa dharura.

Walioathirika zaidi ni pamoja na familia zilizoathiriwa moja kwa moja na mapigano, wakimbizi, wahamiaji pamoja na wale wanaorejea katika maeneo yao ya asili.

Shinikizo laongezeka katika nchi jirani

Shirika hilo limebainisha kuwa mgogoro huo umeongeza mzigo mkubwa kwa nchi jirani, ambapo:

  • Nchini Sudan Kusini, zaidi ya watu milioni 1.3 wamekimbilia hifadhi 
  • Nchini Chad, zaidi ya watu milioni 1.2 wamepokelewa 

Nchi nyingine zilizoathirika na mtiririko huo wa watu ni pamoja na Libya na Misri, hali inayoongeza shinikizo kwa mifumo ya kijamii na huduma ambazo tayari ni dhaifu.

Changamoto kwa wanaorejea nyumbani

Wakati baadhi ya watu zaidi ya milioni 3.8 wameanza kurejea katika maeneo kama Gedaref, Khartoum na Jimbo la Mto Nile, wengi wao wanakutana na mazingira magumu.

IOM imesema wanaorejea wanakabiliwa na miundombinu iliyoharibiwa, ukosefu wa huduma muhimu kama maji, afya na makazi, pamoja na hatari kubwa ya mabomu ambayo hayajalipuka.

Hatua za dharura za IOM

Katika kukabiliana na hali hiyo, IOM inaendelea kuimarisha juhudi zake kwa:

  • Kuboresha ufuatiliaji wa mienendo ya watu wanaohama 
  • Kupanua vituo vya misaada, ikiwemo kitovu cha Farchana mashariki mwa Chad 
  • Kuongeza msaada wa kuvuka mipaka kuelekea maeneo magumu kufikiwa kama Darfur na Kordofan 
  • Kuwekeza katika programu za urejeshaji na ustahimilivu kwa jamii zilizoathirika 

Hatari ya hali kuwa mbaya zaidi

Shirika hilo limeonya kuwa bila ufadhili wa kutosha na juhudi za kisiasa kumaliza mgogoro huo, mamilioni ya watu wataendelea kuwa katika hatari kubwa.

Watu hao wanakabiliwa na changamoto za njaa, ukosefu wa maji safi, huduma za afya na makazi, pamoja na hatari za unyanyasaji, biashara haramu ya binadamu na kuvunjika kwa familia.

IOM imesisitiza kuwa hatua za haraka zinahitajika ili kuokoa maisha na kurejesha matumaini kwa mamilioni ya watu walioathiriwa na mgogoro huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *