Unguja. Wakati Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) ikikusanya Sh100.606 bilioni kwa Machi sawa na ufanisi wa asilimia 109.01, kuwepo na kuunganisha mifumo ya walipa kodi na mifumo ya mamlaka hiyo ni miongoni mwa sababu zinazotajwa kuchangia ufanisi huo.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Aprili 2, 2026 na Mkuu wa kitengo cha habari, uhusiano na huduma kwa wateja wa ZRA, Makame Khamis Moh’d, imeeleza Machi,  ZRA ilikadiriwa kukusanya Sh92.292 bilioni.

Amesema makusanyo hayo yakilinganishwa na makusanyo halisi ya Machi ya mwaka wa fedha uliopita wa 2024/25, ambayo yalikuwa ni Sh73.750 bilioni, ambapo kuna ongezeko la makusanyo ya Sh26.856 bilioni sawa na ukuaji wa makusanyo halisi wa asilimia 36.42.

“Kuwepo kwa matokeo chanya yanayotokana na kazi ya kuunganisha mifumo kati ya walipa kodi na ya ZRA hasa katika biashara ya hoteli za kitalii,” amesema Makame.

Amesema katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/26, ZRA ilikadiriwa kukusanya Sh344.633 bilioni, na imefanikiwa kukusanya Sh320.480 bilioni, sawa na wastani wa makusanyo ya Sh106 bilioni kwa mwezi.

Kwa kulinganisha na makusanyo ya robo ya tatu ya mwaka uliopita wa 2024/25, ambayo yalikuwa ni Sh238.746 bilioni, yanaonesha ongezeko la makusanyo ya Sh81.734 bilioni, sawa na ukuaji wa makusanyo ya asilimia 34.23.

Akitaja sababu nyingine ya kufikia ufanisi huo, Makame amesema ni uwekezaji katika ujenzi wa miundombinu na huduma za kijamii pamoja na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi Zanzibar unaotokana na utekelezaji wa sera nzuri za kiuchumi za Serikali zote mbili.

”Kuongezeka kwa usajili wa walipakodi wapya wakiwemo wafanyabiashara wa kimataifa wanaofanya biashara Zanzibar na kuimarika kwa uingiaji wa watalii nchini kunakochochewa na uwepo wa utulivu na mazingira wezeshi ya kibiashara na kiutalii, hizi ni miongoni mwa sababu zilizochangia ufanisi,” amesema Makame

Akitaja mikakati ya kuendelea kufanya vizuri katika kipindi kijacho, Makame amesema wataongeza kasi katika kuhakikisha mifumo yote ya kibiashara ya walipakodi na inauganishwa na mifumo ya ZRA.

”Kuendeleza utaratibu wa utoaji wa huduma za kodi kwa ukaribu kwa walipakodi wa makundi tofauti sambamba na kuweka kambi katika maeneo ya karibu na biashara ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kodi kwa walipakodi,” amesema.

Wakitoa maoni yao wadau wa kodi, amesema licha ya kiwango hicho bado kuna fedha nyingi hakijakusanywa kwa baadhi ya wafanyabiashara kukwepa kwa kutotoa risiti.

”Bado kuna namna wafanyabiashara wanakwepa kodi kwenye kichaka cha mashine kutofanya kazi kisa mtandao, hivyo kutotoa risiti, wengi wanakuwa sio waaminifu kwa hiyo kuna kodi nyingi inapotea,” amesema Kassim Mbarouk mtaalamu wa masuala ya kodi na fedha.

Ameshauri mamlaka hiyo kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara na kutoa adhabu kali kwa wanaobainika kukwepa utoaji wa kodi hizo, huku akishauri pia kuendelea kuwepo utoaji wa elimu ya kodi kwa umma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *