“Katika Siku ya Kimataifa ya Kuelimisha Umma kuhusu Usonji, tunasherehekea heshima na thamani ya asili ya watu wote wenye usonji. Mkataba wa Haki za Watu wenye Ulemavu unaweka wazi kuwa sisi sote, bila kujali tofauti zetu za kiakili au nyinginezo, ni familia moja ya binadamu wenye haki ya kufurahia haki zote za kibinadamu. Hata hivyo, katika nyakati hizi za machafuko, unyanyapaa wenye madhara unaanza kujitokeza tena na kumomonyoa hatua tulizopiga kuelekea usawa na ushirikishwaji,” amesema Guterres kupitia ujumbe wake mahususi kwa ajili ya siku hii.
Siku ya Uelewa kuhusu Usonji Duniani huadhimishwa na UN kila mwaka tarehe 2 Aprili.
Usonji ni nini?
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la afya Duniani, WHO, Usonji au kwa lugha ya kiingereza ukifahamika kama Autism, ni muunganiko wa hali zinazohusiana na changamoto katika ukuaji wa ubongo, hali hizi zinatambulika zaidi kwa ugumu mkubwa wa kuingiliana na watu kijamii na matatizo ya mawasiliano, mifumo ya fikra na tabia za kujirudia. Uwezo na mahitaji ya watu wenye Usonji hutofautiana sana, ambapo baadhi yao wanaweza kuishi kwa kujitegemea, huku wengine wakihitaji msaada kwa maisha yao yote.
Kaulimbiu ya mwaka huu, “Usonji na Utu – Kila Maisha yana Thamani,” inalenga kupambana na unyanyapaa unaoanza kurudi kwa kasi na mmomonyoko wa haki za msingi kwa watu wenye usonji katika kipindi hiki cha mizozo duniani.
Tofauti za kiutendaji wa ubongo katika Maendeleo Endelevu
Ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs, ni lazima jamii zikubali na kuthamini mchango wa watu wenye usonji kwani uwezo wao wa kipekee unachochea ubunifu na uvumbuzi. Guterres, amesisitiza kuwa watu wenye usonji wana haki ya kuongoza maisha yao wenyewe na kusaidia kuunda mustakabali wa dunia pamoja.
“Kama mwanadamu mwingine yeyote, watu wenye usonji wanapaswa kuwa na uwezo wa kuongoza maisha yao wenyewe – na kusaidia kuunda mustakabali wetu wa pamoja. Wanaleta vipaji, mitazamo, na michango inayofanya dunia kuwa mahali bora zaidi. Kupitia elimu sawa, ajira za haki, na mifumo ya afya inayofikika, tunaweza kuhakikisha kuwa watu wenye usonji wanapata fursa wanazostahili ili kushiriki na kukuza uelewa wao. Kukumbatia utofauti kunatupa sote nguvu. Leo na kila siku, hebu tuthitibishe utu wetu wa pamoja na kutoa tena ahadi yetu kwa ajili ya dunia inayojumuisha kila mtu,” amesisitiza Guterres.
Watu wenye usonji wanapaswa kuwa na uwezo wa kuongoza maisha yao wenyewe.
WHO kupitia taarifa iliyochapishwa leo kwenye wavuti wake, imeungana na jamii kote ulimwenguni kutambua heshima na thamani ya watu wenye usonji huku likihimiza sera zinazoweka mazingira jumuishi.
Takwimu mpya za WHO zinaonesha kuwa duniani kote, mtu 1 kati ya 127 hugundulika kuwa na usonji, hali ambayo ni kati ya matatizo 10 makuu ya afya ya ubongo kote. Licha ya kuwepo kwa mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu, watu wenye usonji bado wanakabiliwa na unyanyapaa, ubaguzi, na vikwazo vikubwa katika kupata huduma bora za afya na msaada wa kijamii, jambo ambalo linaongeza ukosefu wa usawa katika maisha yao yote.
Umuhimu wa utambuzi wa mapema na malezi jumuishi
Ushahidi wa kisayansi unaonesha kuwa utambuzi wa mapema, elimu jumuishi, na malezi yenye upendo ndani ya familia na jamii yanaweza kuboresha sana afya na ustawi wa watu wenye usonji. Ili kusaidia juhudi hizi, WHO itazindua mafunzo mapya ya ustawi wa walezi wa watoto wenye changamoto za ukuaji tarehe 27 Aprili mwaka huu, yakilenga kutoa mbinu za vitendo za kuimarisha huduma jumuishi.