Dar es Salaam. Mfumuko wa bei nchini unatarajiwa kubaki ndani ya wigo wa asilimia 3 hadi 5 katika robo ya pili ya mwaka 2026, licha ya shinikizo linalotokana na kupanda kwa gharama za bidhaa za mafuta katika soko la dunia.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Aprili 2, 2026 na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) anayeshughulikia Sera za Uchumi na Fedha, Dk Yamungu Kayandabila wakati akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) baada ya kikao chake cha hivi karibuni.

Amesema ongezeko la gharama za nishati na usafirishaji linaendelea kuwa chanzo kikuu cha shinikizo la mfumuko wa bei, likichochewa na kupanda kwa bei ya mafuta ghafi katika soko la dunia iliyotoka dola za Marekani 60 kwa pipa katika robo ya kwanza ya mwaka 2026 hadi zaidi ya dola 100 kwa pipa sasa.

Amefafanua kuwa licha ya hali hiyo, mfumuko wa bei uliendelea kubaki katika kiwango cha chini, ukiwa wastani wa asilimia 3.3 kwa Tanzania Bara katika robo ya kwanza ya mwaka 2026, huku ukitarajiwa kuendelea kudhibitiwa ndani ya malengo yaliyowekwa.

“Kamati inatarajia mfumuko wa bei kubaki ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5 katika robo ya pili ya mwaka 2026, bei nafuu za chakula pamoja na uthabiti wa thamani ya shilingi vinasaidia kupunguza kasi ya ongezeko la mfumuko wa bei,” amesema.

Haya yanasemwa wakati ambao tayari Watanzania wameanza kuonja maumivu ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma, ikiwa ni saa chache tangu kutangazwa kwa bei mpya za mafuta Aprili mosi mwaka huu likichochea nauli za bodaboda na bajaji na bei za vyakula kuanza kupanda.

Dk Kayandabila amesema mfumuko wa bei umeendelea kuwa wa chini katika nchi nyingi, lakini hatari zimeongezeka kutokana na kupanda kwa gharama za nishati na usafirishaji kufuatia mvutano wa kisiasa unaoendelea katika Mashariki ya Kati.

“Katika mazingira hayo, benki kuu inaweza kulazimika kurekebisha viwango vya riba ili kudhibiti mfumuko wa bei iwapo migogoro itaendelea au kuongezeka,” amesema.

Kutokana na hali hiyo, MPC imeamua Kiwango cha Riba cha Benki Kuu (CBR) kuendelea kuwa asilimia 5.75 kwa robo ya pili ya mwaka 2026, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha mfumuko wa bei unabaki chini huku ukuaji wa uchumi ukiendelea.

Amesema uamuzi huo unaakisi msimamo wa tahadhari unaolenga kusawazisha hatari za mfumuko wa bei na matarajio ya ukuaji wa uchumi, katika mazingira ya mvutano wa kimataifa unaoathiri biashara na uwekezaji.

Kwa upande mwingine, sekta ya benki imeendelea kuwa imara ikiwa na ukwasi wa kutosha na mitaji inayokidhi viwango, huku uwiano wa mikopo chechefu ukishuka hadi asilimia 2.9, chini ya kiwango kinachokubalika cha asilimia 5.

“Ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi umeendelea kuwa thabiti kwa asilimia 22.8, ukichochewa na sera nafuu ya fedha na mahitaji makubwa kutoka kwa biashara na kaya,” amesema.

Katika sekta ya nje, nakisi ya urari wa malipo imepungua hadi asilimia 2.2 ya pato la Taifa, ikichangiwa na ongezeko la mauzo ya nje, hususan dhahabu, mazao ya kilimo na utalii.

Aidha, uchumi wa Zanzibar umeendelea kurekodi ziada katika urari wa malipo kutokana na mapato makubwa ya utalii.

“Thamani ya shilingi imeendelea kuwa thabiti kutokana na uwepo wa akiba ya kutosha ya fedha za kigeni inayozidi dola za Marekani 6.2 bilioni pamoja na kupungua kwa uagizaji wa bidhaa kutoka nje,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *