Arusha. Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imemwachia huru Tajiri Dibwa aliyekuwa akikabiliwa na mashtaka ya kusafirisha kilo 109.28 za dawa za kulevya aina ya bangi, baada ya kubaini mapungufu katika ushahidi wa upande wa mashtaka.

Hukumu hiyo ilitolewa Aprili 2, 2026 na Jaji Sedekia Kisanya, aliyesema ushahidi uliowasilishwa haukuthibitisha mashtaka hayo bila kuacha shaka, kama inavyotakiwa katika kesi za jinai.

Katika uamuzi wake, Mahakama ilibaini kuwapo kwa dosari kadhaa, ikiwemo kukatika kwa mnyororo wa ulinzi wa vielelezo, hali iliyozua mashaka kuhusu uhalali na uaminifu wa ushahidi uliowasilishwa.

Mahakama pia ilieleza kuwa kulikuwa na utofauti wa maelezo kati ya mashahidi wa upande wa mashtaka kuhusu namna mifuko iliyodaiwa kuwa na bangi ilivyogunduliwa ndani ya gari la mshtakiwa.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, baadhi ya mashahidi walidai mifuko hiyo ilionekana kwa kuchungulia ndani ya gari, huku wengine wakidai iligunduliwa baada ya mshtakiwa kufungua buti na milango ya gari. Tofauti hizo zilidhoofisha uaminifu wa ushahidi huo.

Aidha, kulibainika mkanganyiko kuhusu nani aliyekuwa na dhamana ya kusimamia vielelezo hivyo tangu vilipokamatwa hadi vilipowasilishwa mahakamani.

Jaji Kisanya alisema kutokuwepo kwa ushahidi unaoonyesha mnyororo kamili wa ulinzi wa vielelezo kulizua shaka kubwa juu ya uhalali wa vielelezo vilivyowasilishwa.

Alisisitiza kuwa katika kesi za jinai, upande wa mashtaka una wajibu wa kuthibitisha shtaka bila kuacha shaka yoyote, na pale panapokuwapo mashaka, lazima yatafsiriwe kwa faida ya mshtakiwa.

Kutokana na mapungufu hayo, mahakama ilihitimisha kuwa upande wa mashtaka haukuweza kuthibitisha kuwa mshtakiwa alikuwa akisafirisha dawa hizo au kwamba zilikuwepo tu ndani ya gari lake, kwa uhakika usio na shaka.

Mahakama pia ilikumbusha umuhimu wa kufuata taratibu sahihi katika ukusanyaji, uhifadhi na uwasilishaji wa vielelezo ili kuhakikisha haki inatendeka, ikibainisha kuwa kuvunjika kwa mnyororo wa ulinzi wa vielelezo kunaathiri uaminifu wa ushahidi.

Kutokana na hali hiyo, Mahakama ilimtangaza mshtakiwa kuwa hana hatia na kuamuru aachiwe huru mara moja, isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine za kisheria.

Aidha, iliagiza arejeshewe gari lake lililokuwa limetumika kama kielelezo.

“Ni dhahiri kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kwa kiwango kinachohitajika shtaka la usafirishaji wa dawa za kulevya dhidi ya mshtakiwa,” alisema Jaji Kisanya.

Mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Mei 17, 2025 akikabiliwa na mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya kinyume cha sheria.

Kesi hiyo ilitokana na ajali ya barabarani iliyohusisha gari aina ya Toyota Premio alilokuwa akiendesha mshtakiwa, na lori aina ya Howo lililokuwa limeunganishwa na trela, likiendeshwa na Ibrahim Nyange.

Ilidaiwa kuwa baada ya ajali hiyo, mifuko saba ya salfeti iliyokuwa imejaa majani makavu iligunduliwa ndani ya gari la mshtakiwa, na baadaye kuthibitishwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) kuwa ni bangi yenye uzito wa kilo 109.28.

Katika usikilizaji wa kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi tisa pamoja na vielelezo saba, wakieleza namna mifuko hiyo ilivyogunduliwa, kukamatwa na kuhifadhiwa kabla ya kupelekwa maabara kwa uchunguzi.

Hata hivyo, katika utetezi wake, mshtakiwa alikanusha kuhusika na dawa hizo, akieleza kuwa siku ya tukio alikuwa akitoka kuchukua dawa za asili kwa ajili ya mtoto wake mgonjwa.

Alidai kuwa baada ya ajali hiyo, kulitokea mvutano kuhusu fidia kati yake na dereva wa lori na baadaye alikamatwa na kuwekwa kizuizini. Aidha, alidai alilazimishwa kusaini nyaraka bila maelezo ya kina.

Mshtakiwa pia alipinga ushahidi wa mashtaka kwa kueleza kuwa kulikuwa na mkanganyiko mkubwa kuhusu namna vielelezo vilivyopatikana na kuhifadhiwa, akidai baadhi ya mifuko iliyowasilishwa mahakamani haikuwa na alama zinazolingana na maelezo ya awali ya mashahidi.

Aliiomba Mahakama imwachie huru, akisisitiza kuwa kesi dhidi yake ilikuwa na mashaka makubwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *