Geita. Kelele za wateja waliokuwa wakinywa pombe ya kienyeji katika Mtaa wa mkoani, Kata ya Kalangalala, Manispaa ya Geita, ghafla zilibadilika kuwa mshangao na taharuki baada ya kugundulika kuwa debe la pombe aina ya mgoligoli lilikuwa limechafuliwa kwa kinyesi kinachodaiwa kuwekwa na mwanamke aliyekuwa akishuku mume wake kuwa na uhusiano wa kimapenzi na muuza pombe.

Tukio hilo lililotokea hivi karibuni limeacha majonzi kwa wafanyabiashara wa pombe za kienyeji katika eneo hilo baada ya wateja kuanza kususia biashara zao wakihofia kunywa pombe iliyochafuliwa.

Mwanamke anayehusishwa na tukio hilo ametajwa kwa jina la Zawadi Baraka maarufu Mama Salome, ambaye anadaiwa kujisaidia haja kubwa ndani ya chumba kinachotumika kuhifadhia pombe za kienyeji zinazomilikiwa na Elizabeth Francisco.

Kwa mujibu wa majirani na wafanyabiashara wa pombe za kienyeji katika mtaa huo, tukio hilo linadaiwa kuwa la pili kufanywa na mwanamke huyo, ambaye amekuwa akimtuhumu Elizabeth kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mume wake.

Akizungumza na Mwananchi Aprili 2, 2026, Elizabeth ambaye ni mmiliki wa pombe hizo amekanusha vikali tuhuma za kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mume wa mwanamke huyo.

Amesema siku chache kabla ya tukio hilo, mwanamke huyo alifika katika eneo lake la biashara akiwa amelewa na kuanza kufanya fujo mbele ya wateja.

“Juzi alifika hapa akiwa amelewa, akaanza kufanya vurugu na kumwaga baadhi ya pombe nilizokuwa nauza. Wateja wakakimbia bila kulipa bia walizokuwa wamekunywa,” amesema.

Elizabeth amesema awali hakujua nani aliyekuwa amehusika kuchafua pombe hiyo kwa kinyesi.

Amesema alidhani huenda tukio hilo lilifanywa na wageni waliokuwa wamelala katika chumba hicho cha biashara usiku huo.

Hata hivyo, baada ya kuwauliza wageni hao, walikana kuhusika na kitendo hicho na kueleza kuwa walimwona mwanamke huyo akifika usiku na kufanya fujo kabla ya kuondoka.

“Waliniambia alikuja usiku akiwafanyia fujo, lakini hawakujua kama alikuja kujisaidia kwenye pombe zilizokuwa chumbani humo,” amesema Elizabeth.

Baada ya taarifa hizo, ukaguzi ulifanyika chini ya usimamizi wa viongozi wa mtaa ambapo ilithibitika kuwa pombe hiyo ilikuwa imechafuliwa na kinyesi.

Elizabeth Fransisco, muuzaji wa Pombe ambaye amefanyiwa tukio lililoibua mshangao katika jamii, akidaiwa kuiba Mme wa mwanamke anayedhaniwa kujisaidia katika pombe hiyo ili kumkomoa.

Kutokana na hali hiyo, iliamuliwa pombe yote iliyokuwa katika debe hilo imwagwe ili kuepusha hatari kwa watumiaji.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mkoani, Salvatory Paul, amesema tukio hilo linahusishwa na wivu wa kimapenzi baada ya mwanamke huyo kumtuhumu Elizabeth kuwa na uhusiano na mume wake.

Amesema ofisi yake ilipokea malalamiko kutoka kwa Elizabeth kuhusu vurugu zilizokuwa zikifanywa katika eneo lake la biashara.

“Baada ya kusikiliza pande zote mbili tuligundua kuwa chanzo kikubwa ni wivu wa kimapenzi. Mwanamke huyo anamtuhumu mmiliki wa pombe kuwa na uhusiano na mume wake,” amesema.

Amesema katika kikao kilichofanyika, iliamriwa mume wa mwanamke huyo kulipa fidia ya Sh40,000 kwa ajili ya pombe zilizomwagwa pamoja na hasara iliyotokana na wateja kukimbia bila kulipa baada ya vurugu.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, mwanaume huyo aliahidi kulipa fedha hizo ifikapo Aprili 5, 2026.

“Tuliwapa angalizo pia kuwa kama ni vilabu vya pombe ni vingi, watafute sehemu nyingine ya kunywa. Yule baba pia tumemshauri aachane na tabia hiyo kwa sababu mke wake tayari ameshamshtukia,” amesema.

Wafanyabiashara wengine wa pombe za kienyeji katika eneo hilo wamesema tukio hilo limeathiri vibaya biashara zao kwa kuwa wateja wengi sasa wanaogopa kunywa pombe katika vilabu vya mtaa huo.

Hadija Elias, mmoja wa wauzaji wa pombe hizo, amesema wamekuwa wakipata hasara kubwa kutokana na wateja kupungua.

“Vitendo vya huyu mama vimetuchosha sana. Sisi tunafanya biashara halali, tunalisha familia zetu kupitia kazi hii. Lakini tukio kama hili linaharibu sifa ya biashara yetu,” amesema.

Amesema wanawake wengi katika mtaa huo wanategemea biashara ya pombe za kienyeji kuendesha maisha yao, ikiwa ni pamoja na kulipia kodi za nyumba na ada za shule kwa watoto.

“Naiomba Serikali imtafute na kumchukulia hatua ili iwe fundisho kwa wengine,” amesema.

Mfanyabiashara mwingine, Halima Rwige, amesema siku iliyofuata baada ya tukio hilo hakupata hata mteja mmoja katika biashara yake.

“Leo nimeivisha pombe lakini unaona hakuna mteja hata mmoja anayekanyaga hapa. Watu wanaogopa wakidhani hata sisi tunaweza kuwa tunauza pombe iliyochafuliwa,” amesema.

Amesema hali hiyo imeathiri mapato yao ya kila siku.

“Kwa mfano leo huenda nisipate hata Sh1,000 ya kununua chakula cha watoto. Pombe ikibaki tunalazimika kuimwaga,” amesema.

Wakati huo huo, juhudi za kumsaka mwanamke anayehusishwa na tukio hilo zinaendelea.

Viongozi wa mtaa kwa kushirikiana na polisi jamii wanasema mwanamke huyo pamoja na mume wake wameondoka katika eneo hilo na hawajulikani walipo.

Mwenyekiti wa mtaa amesema hatua zaidi zitachukuliwa endapo watapatikana ili kuhakikisha matukio kama hayo hayajirudii katika jamii.

Tukio hilo limeibua mjadala miongoni mwa wakazi wa eneo hilo kuhusu madhara ya migogoro ya kimapenzi, hasa pale inapogeuka na kuathiri maisha na shughuli za kiuchumi za watu wengine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *