BAADA ya kipa wa Dodoma Jiji, Ally Salim kukaa nje kwa takribani mwezi mmoja alipoumia  mechi dhidi ya Mbeya City, iliyokuwa imepigwa Uwanja wa Sokoine, Machi 02, 2024 na kumalizika kwa sare ya bao 1-1 ni suala la muda kujiunga na wenzake.

Salim ni mmoja kati ya makipa wenye uzoefu wa kutosha kwenye ligi Kuu akiwa amepata umaarufu mkubwa akiwa kwenye kikosi cha Simba.

Mwanaspoti lilimtafuta Salim ili kujua maendeleo yake, amesema anaendelea vizuri tofauti na mwanzo, hivyo anasubiri kuruhusiwa na daktari kurejea kambini kujiunga na wenzake.

“Naendelea vizuri na nazingatia kila kitu ninachoambiwa na daktari, akiniruhusu kujiunga na wenzangu kambini nitafanya hivyo ila kwa sasa bado nipo nyumbani kwangu,” amesema Salim.

Kabla ya kupata majeraha hayo Salim alishaanza kuonyesha umwamba wake kwenye ligi akiwa ametumika kwenye michezo mitano bila kuruhusu bao.

“Msimu huu nilitarajia kufanya makubwa baada ya kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara Dodoma ili majeraha yameingilia kati, lakini nashukuru Mungu kwa sasa naendelea vizuri na naweza kurejea uwanjani wakati wowote kuanzia sasa.”

Kwa upande wa kocha wa timu hiyo, Aman Josiah amesema kukosekana kwa Salim kuna pengo kutokana na uzoefu wake na mchango katika timu, lakini uhakika aliyonao anaweza akadaka mechi za mwishoni.

“Kwanza ana nidhamu, kiwango chake ni cha juu, anapatana na wenzake na makocha, mcheshi mtu wa namna hiyo akikosekana kikosini lazima pengo lake litakuwepo, ingawa anaweza akarejea baada ya wiki mbili au tatu, tunawasiliana naye kumpa moyo na kumuombea,” amesema.

Dodoma Jiji ni moja kati ya timu za Ligi Kuu ambazo msimu huu zimefanya vizuri ikiwa imeshacheza michezo  19 ikiwa nafasi ya tisa kwenye msimamo na pointi 21, timu hiyo ambayo imekuwa ikifanya vizuri kwenye michezo yake ya nyumbani imeshinda mechi tano, imetoka sare sita na kupoteza sita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *