SERIKALI ya Tanzania imeipongeza timu ya Dar City kwa kuweka historia ya kufuzu hatua ya nane bora (mtoano) ya mashindano ya mpira wa kikapu ya Africa (Basketball Africa League).

Dar City baada ya kumaliza nafasi ya nne katika mashindano yaliyofanyika Afrika Kusini ikishinda mechi mbili kati ya tano ilizocheza, imefuzu hatua ya mtoano iliyopangwa kuanza Mei 22, 2026 mpaka Mei 31, 2026, jijini Kigali nchini Rwanda.

Dar City ilianza kwa ushindi dhidi ya Johannesburg Giants ya Afrika Kusini kwa pointi 100-70, kisha ikaichapa Nairobi City Thunders kwa pointi 90-85.

Baada ya mechi hizo, Dar City ilipoteza kwa mabingwa watetezi Al Ahly Ly ya Libya kwa pointi 118-97 na baadaye dhidi ya Petro Atletico ya Angola kwa pointi 100-75 na dhidi ya RSSB Tigers ya Rwanda kwa pointi 104-92.

Pamoja na kupoteza mechi hizo, Dar City imefanikiwa kufuzu kwa kufuatia ushindi wake dhidi ya Nairobi City Thunders wa pointi 90-85 ambapo waandaaji wanatumia matokeo baina ya timu hizo mbili zilipokutana (head to head).

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema Dar City imeiletea heshima Tanzania na kutoa hamasa kubwa kwa mchezo wa mpira wa kikapu nchini.

Msigwa alisema matokea hayo ni ishara kubwa kwamba mchezo wa mpira wa kikapu Tanzania unakuwa na kuomba michezo mingine kuhakikisha inafanya vyema katika mashindano ya kimataifa.

“Aidha, tunampongeza Mussa Mzenji kwa uwekezaji mkubwa alioufanya katika timu hii. Huu ni uthibitisho kuwa sekta binafsi ni nguzo muhimu katika maendeleo ya michezo.

“Serikali itakuwa tayari kushirikiana na wadau wote walio tayari kuwekeza katika michezo iwe katika vilabu au akademia za michezo. Tunawapongeza pia Shirikisho la Basketball Tanzania (TBF) kwa jitihada walizoweka hadi kupata mafanikio haya,” amesema Msigwa.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Dar City, Simon Mirondo, amewapongeza wachezaji na wadau wote walioiwezesha timu hiyo kufuzu hatua ya nane bora na kuweka historia.

Mirondo alisema mashindano yalikuwa magumu, lakini wameweza kufuzu hasa baada ya kuzifunga timu za Johannesburg na Nairobi City Thunders ambazo katika mashindano ya Kenya, zilitawala.

Amesema baada ya kuwasili nchini, wachezaji watapumzika kwa siku kadhaa, kabla ya kuanza kujiandaa na mashindano yatakayofanyika Kigali.

“Tutajiandaa vyema zaidi kwa ajili ya finali za Rwanda. Kule timu zote bora zitashiriki, hivyo lazima tujiandae kwa kikamilifu. Tunaamini, wachezaji wetu wawili, David Michineau na Michael Foster watakuwa wamepona kwani hawajacheza mchezo wa mwisho kutokana na majeraha,” amesema Mirondo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *