
Dar es Salaam. Umoja wa Wahadhiri wa Kiislam Tanzania (Uwakta), umeshauri jamii kuendelea kuelimishwa kuhusu tatizo la kupanda kwa bei ya mafuta kwa kile ilichoeleza kuna upotoshaji unaendelea kuhusiana na jambo hilo huko uraiani.
Umoja huo umetoa kauli hiyo leo Jumatatu, Aprili 6, 2026 walipozungumza na waandishi wa habari kuhusu sakata la mafuta, ambapo pia waligusia taharuki inayoendelea ya wanaume kuibiwa nyeti inayoripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Kauli yao ya kupanda bei ya mafuta, Uwakta inazungumza ikiwa, zimepita siku tano tangu Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) itangaze ongezeko hilo la bei za mafuta linaloelezwa kuchochewa na mgogoro wa kimataifa unaoendelea kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, ulioanza Februari 28, 2026.
Mgogoro huo umeathiri uzalishaji na usafirishaji wa mafuta ghafi duniani, hasa baada ya kufungwa kwa Mlango wa Hormuz, ambao hupitisha takribani asilimia 20 ya mafuta yote yanayosafirishwa duniani.
Vilevile, kushambuliwa kwa visima vya mafuta, maghala ya kuhifadhi mafuta na viwanda vya kuyasafisha kumeigusa moja kwa moja Tanzania ambayo inaagiza mafuta kwa kiasi kikubwa, jambo linalotajwa kuongeza gharama za usafirishaji kutokana na kukosekana kwa meli za kuyasafirisha.
Hali hiyo imesababisha ongezeko kubwa ambalo halijashuhudiwa kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita ambapo kwa kila lita ya mafuta ya dizeli, petroli na mafuta ya taa imeongezeka kwa zaidi ya Sh900, na kuilazimisha Serikali kukuna kichwa kutafuta namna ya kupunguza athari hizo.
Juzi Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, aliimbia Mwananchi Digital, kuwa Serikali inafanyia kazi jambo hilo kwa umuhimu mkubwa.
“Wataalamu wanachakata namna bora ya kufanya na wakati wowote Serikali itatoa mwelekeo tutakaochukua. Tunawaomba wananchi wavumilie muda mfupi ujao watajulishwa,” alisema Msigwa.
Walichosema Uwakta
Wakizungumzia sakata hali hilo la mafuta, Kiongozi Mkuu wa Uwakta, Sheikh Rajab Juma, amesema licha ya sababu ambazo zimeshatajwa na mamlaka bado kuna watu wanapotosha jamii ili tatizo hilo lionekane ni la serikali.
Sheikh Juma amesema; “Kama Marekani, Uingereza mataifa ambayo ni makubwa kiuchumi yana kilio cha nishati hiyo, Tanzania ni nani hili lisituguse, hapa wananchi waendelee kuelimisha kuwa hilo si tatizo la nchi yetu bali ni tatizo la kidunia kwani hali hiyo ikiachwa itazidi kuketa taharuki zisizo na ulazima.”
Naye Mkuu wa Idara ya Kilimo, Ujasiriamali na Utafiti wa Uwakta, Sheikh Ibrahimu Bakoz, amesema kupanda bei kwa mafuta sio jambo la kufurahia kwa kuwa litasababisha kuwepo mfumuko wa bei na ni jambo ambalo linaumiza na linatia majonzi.
“Hata hivyo ni jambo la kusikitisha tunapozungumza sisi wapo watu wanasema tunaitetea Serikali na kutupa majina mbalimbali ikiwemo chawa, kupe, kunguni, yote haya hatujali kwani lengo letu ni kutaka kupunguza taharuki kwa wananchi.
“Hapa ieleweke kazi ya kiongozi wa dini ni kushauri pale anapoona mambo hayako sawa na kupongeza yanapokuwa sawa na sio kuwa mtu wa kukosoa tu kwani kazi hiyo wanapaswa kuachiwa wanasiasa,” amesema Sheikh Bakoz.
Amesema ni hivi karibuni, Taifa limetoka katika kipindi kigumu hivyo wasingependa kuona linarudi huko kwa kuzua taharuki zisizo na tija kwa nchi.
Kwa upande wa Serikali ameiomba kuharakisha mchakato wa ujenzi wa matenki ya kuhifadhi mafuta kwa kuwa ukikamilika shida kama hizi zikitokea nchi haitapata taabu.
Wagusia sakata la watu kuibiwa nyeti
Katika hatua nyingine, Umoja huo umezungumzia taharuki inayoendelea kuhusu wanaume kuibiwa nyeti kwa njia ya mazingira ya kishirikina ambapo inadaiwa mtu akiguswa bega zinapotea.
Hata hivyo tayari Jeshi la Polisi limekanusha kuwepo kwa matukio hayo huku likionya wanaoendelea kueneza uzushi huo kuwa watawachukulia hatua.
Akilizungumzia hilo, Naibu Amiir wa Uwakta, Sheikh Shabaan Muhoro, amesema suala la nyeti ni watu wamekaa wakatunga na halina ukweli isipokuwa ni kutaka kuharibu amani ya Watanzania.
“Kwani hatujaona taarifa ya Polisi ikithibitisha hilo kwa wote wanaodaiwa kufanya hivyo,” amesema Sheikh Muhoro.
Akifafanua zaidi kile wanachokiona kama Umoja, amesema inajulikana wanaume ndio wapo mbele katika majukumu ya kitaifa, hivyo ukiwatingisha watashindwa kushiriki vilivyo katika majukumu hayo.
Katika hilo amesema hata sasa hivi wanaume wengi wanajijua hali zao ni dhoofu bin hali ndio maana watu wanakula mkongo, alkasusu, supu ya pweza na vitu vingine ili kujiweka imara, hivyo likichanganywa hilo ni kutaka kuwadhoofisha kabisa washindwe kufanya kazi na mwisho ni kuja kuua uchumi wa nchi.