Marekani. Baada ya mashabiki kusubiri kwa muda mrefu, hatimaye zimebaki siku 14 kuachiwa kwa filamu ya wasifu wa mfalme wa Pop, Michael Jackson.
Filamu hiyo iliyopewa jina la Michael inatarajiwa kuachiwa rasmi Aprili 24, 2026, ikiwa ni moja ya kazi kubwa zaidi kuwahi kufanyika ikielezea maisha ya mwanamuziki huyo mashuhuri aliyebadilisha historia ya muziki wa Pop.
Katika filamu hiyo, mwigizaji mkuu ni Jaafar Jackson, ambaye ni mpwa wa Michael Jackson. Jaafar, mwenye umri wa miaka 25, amepewa jukumu zito la kuigiza maisha ya mjomba wake, akionyesha kwa undani safari ya kipaji chake, changamoto alizopitia, pamoja na mafanikio makubwa aliyoyapata.
Mbali na Jaafar, filamu hiyo imewakutanisha mastaa wengine wakubwa wa filamu akiwemo Nia Long, Laura Harrier, Miles Teller na Colman Domingo ambao wameongeza uzito na ubora wa kazi hiyo.
Jaafar Jackson si mgeni kwenye tasnia ya burudani. Mbali na kufanana na mjomba wake, pia ni mwanamuziki na dansa. Alianza kuimba rasmi akiwa na umri wa miaka 12 na kujizolea umaarufu mwaka 2019 baada ya kuachia wimbo wake wa “Got Me Singing”, uliomfungulia milango zaidi kwenye tasnia ya muziki.
Filamu ya “Michael” inatajwa kuwa kumbukumbu muhimu ya maisha ya mwanamuziki huyo aliyekuwa na ushawishi mkubwa duniani. Ambapo itagusa vipindi mbalimbali vya maisha yake kuanzia utoto wake katika familia ya The Jackson 5 hadi kuwa nyota mkubwa wa kimataifa.
Ikumbukwe Michael Jackson alizaliwa mwaka 1958 na kufariki dunia mwaka 2009. Amewahi kutamba na ngoma kama Smooth Criminal, Thriller, na Will You Be There ambazo zimeendelea kukusanya watazamaji kila iitwayo leo katika chati za muziki.
Kwa upande wa mashabiki wake, sasa wameelekeza macho na masikio Aprili 24 kuona kama filamu hiyo itaweza kuendana na hadhi na historia ya jina la Michael Jackson.
Filamu hiyo ambayo imeandikwa na John Logan ikitayarishwa (producer) na Graham King, itaanza kwanza kuonyeshwa katika kumbi za sinema duniani kote baadaye itahamishwa katika majukwaa ya streaming ambayo ni Netflix, Amazon Prime Video na Apple TV+.