Akizungumza na waandishi wa habari mchana leo jkwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani amesema “Haki inapaswa kuwa kipofu. Lakini leo, wengi wanachagua kuifumbia macho haki yenyewe”.
Amesisitiza kuwa katika maeneo mengi ya migogoro, “kanuni zinazosimamia matumizi ya nguvu na mwenendo wa vita zinapuuzwa, na kuwaacha raia katika madhara yasiyovumilika.”
Eneo la Basta huko Beirut limesalia magofu kufuatia mojawapo ya mashambulizi makubwa zaidi ya Israeli nchini Lebanon.
Mgogoro wa Mashariki ya Kati mfano wa kuzorota kwa sheria
Katibu Mkuu ameitaja Mashariki ya Kati kama mfano wa wazi wa kupuuzwa kwa sheria za kimataifa, akionya kuwa wajibu wa kibinadamu unakiukwa na hata wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa hawalindwi.
“Hili ni shambulio la wazi dhidi ya sheria za kimataifa lenye madhara makubwa,” amesema. “Ukosefu wa sheria huzaa machafuko. Huchochea mateso. Husababisha uharibifu.”
Hakuna suluhisho la kijeshi
Guterres amesisitiza umuhimu wa diplomasia badala ya matumizi ya nguvu za kijeshi katika kutatua migogoro.
“Hakuna suluhisho la kijeshi kwa mgogoro huu,” amesema. “Makubaliano ya amani yanahitaji juhudi endelevu na dhamira ya kisiasa. Mazungumzo ya dhati lazima yaanze tena.”
Ameongeza kuwa usitishaji mapigano lazima udumishwe na kupanuliwa ili kuzuia kuzorota zaidi kwa hali ya usalama.
Ziara The Hague kuadhimisha miaka 80 ya ICJ
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa pia ametangaza kuwa atasafiri kwenda The Hague Uholanzi katika kuadhimisha miaka 80 ya ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ.
Amesema mahakama hiyo ni “nguzo muhimu ya mfumo wa sheria za kimataifa,” na kwamba ziara hiyo inalenga kutuma ujumbe wa wazi kuhusu umuhimu wa kuziheshimu sheria hizo.
“Sheria za kimataifa zinayahusu mataifa yote bila ubaguzi, na kuziheshimu si jambo la hiari,” amesisitiza.
Makao makuu ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, The Hague, Uholanzi
Kuheshimu njia muhimu za usafiri wa kimataifa
Katibu Mkuu amegusia pia umuhimu wa kuheshimu haki za usafiri wa kimataifa, hasa katika maeneo nyeti kama Mlango Bahari wa Hormuz.
Amewataka wahusika wote kuonesha kujizuia na kuwajibika ili kuepusha athari kubwa zaidi duniani.
Ni wakati wa diplomasia badala ya mvutano
Akihitimisha, tarifa yake Guterres ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kurejea katika misingi ya sheria na ushirikiano.
“Ni wakati wa kujizuia na kuwajibika. Ni wakati wa diplomasia badala ya kuongezeka kwa mvutano,” amesema. “Ni wakati wa kujitolea upya kwa sheria za kimataifa.”
Ameonya kuwa katika dunia inayozidi kugawanyika, kupuuza sheria za kimataifa kutaongeza kutokuaminiana na kuchochea migogoro zaidi.