Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na FAR Rabat ya Morocco zimefanikiwa kutinga hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kupata matokeo yaliyozifanya zisonge mbele katika mechi zilizochezwa Jumamosi, Aprili 18, 2026.

Timu hizo mbili zimefuzu kwa kubebwa na matokeo ya michezo miwili ya nyumbani na ugenini ambayo kila moja imecheza.

Katika Uwanja wa Lucas Masterpieces Moripe, Pretoria, Afrika Kusini, wenyeji Mamelodi Sundowns wameibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Esperance ya Tunisia.

Matokeo hayo yamewafanya wafuzu kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-0, shukrani kwa ushindi wa bao 1-0 walioupata katika mechi ya ugenini.

Bao pekee la ushindi la Mamelodi Sundowns nyumbani limefungwa na Brayan Leon katika dakika ya 35.

Katika Uwanja wa Manispaa jijini Berkane, Morocco, wageni FAR Rabat wamekata tiketi ya fainali licha ya kufungwa bao 1-0 na RS Berkane.

FAR Rabat wamesonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1 wakibebwa na ushindi wa mabao 2-0 walioupata katika mechi ya kwanza wiki iliyopita.

Fainali ya Mamelodi Sundowns na FAR Rabat inakutanisha timu mbili zenye uzoefu wa hatua hiyo.

Hii itakuwa ni mara ya nne kwa Mamelodi Sundowns kuingia Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo katika mara tatu zilizopita, waliondoka na taji mara moja na kupoteza fainali mbili nyingine.

FAR Rabat waliwahi kuingia fainali mara moja ambayo ni 1985 ma walitwaa ubingwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *