Katika mahojiano haya na Anold Kayanda wa Idhaa ya Umoja wa Mataifa, mhandisi wa masuala ya anga, Alinda Mashiku anatafakari nafasi ya wanawake katika uchunguzi wa anga za mbali, umuhimu wa safari ya kihistoria ya mwezi ya Christina Koch, na kwa nini wasichana hasa kutoka Afrika na diaspora wasione mipaka dhidi ya ndoto zao katika sayansi na teknolojia.
Habari za Umoja wa Mataifa Alinda Mashiku ni mhandisi wa anga na mwanasayansi aliyefanikiwa anayeshughulikia kazi kama Meneja wa Programu ya Programu ya Uchambuzi wa Hatari ya Kukutana (Conjunction Assessment Risk Analysis – CARA) ya NASA katika Kituo cha Nafasi cha NASA Goddard, ambapo anaongoza jitihada za kulinda satelaiti kutoka au

Kwa Dkt. Mashiku, mwanamke mwenye asili ya Afrika aliyezaliwa New York, Marekani kwa wazazi Watanzania waliokuja kusoma Marekani na kisha kurejea Tanzania yeye akiwa na umri wa miaka mitano, hivi sasa ni  mwanasayansi mashuhuri anayehudumu kama Meneja wa Mpango wa Uchambuzi wa Hatari za Migongano Angani (CARA) katika Kituo cha Kitaifa cha masuala ya Anga za mbali cha NASA Goddard, Maryland nchini Marekani ambako anaongoza juhudi za kulinda satelaiti dhidi ya migongano angani.

Alipata shahada ya kwanza ya uhandisi wa anga kutoka The Ohio State University na shahada ya uzamili pamoja na uzamivu (PhD) katika uhandisi wa anga na astronautiki kutoka Chuo Kikuu cha Purdue. Tangu ajiunge na NASA mwaka 2013, amechangia misheni kubwa zikiwemo OSIRIS-REx na James Webb Space Telescope. Mbali na kazi yake katika sayansi ya anga, Dkt. Mashiku pia ni mwanzilishi mwenza wa Joule Foundation, taasisi inayokuza elimu ya STEAM kwa wasichana barani Afrika, jambo linalodhihirisha dhamira yake ya ulezi, ubunifu na kupanua fursa kwa kizazi kijacho.

Ujumbe mkubwa kuliko mwezi

Kwa Alinda Mashiku, misheni ya kihistoria ya Artemis II ni zaidi ya safari ya kuuzunguka Mwezi. Ni kuhusu uwezekano. Wakati misheni hiyo ikifungua ukurasa mpya wa uchunguzi wa binadamu angani  ikiwemo ushiriki wa Christina Koch, mwanamke wa kwanza kupangiwa kusafiri kuuzunguka Mwezi pia inatuma ujumbe wenye nguvu kwa wanawake na wasichana duniani kote: kuna nafasi yao katika sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati.
© NASA/John Kraus Wanaanga wa NASA Reid Wiseman, kamanda wa Artemis II; Victor Glover, rubani wa Artemis II; Christina Koch, mtaalamu wa misaada ya Artemis II; na Jeremy Hansen, mtaalamu wa misaada ya Artemis II wa Shirika la Anga la Kanada (CSA), wanapiga picha.

Akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa (UN News), Dkt. Mashiku anasema misheni hiyo inaonesha wasichana wadogo kuwa ndoto zao ni za kweli na zinawezekana kutimia. “Ikiwa tunaweza kuota kuondoka duniani na kurejea salama, basi chochote kinawezekana,” anasema. Kwa mtazamo wake, ishara ya mwanamke kusafiri mbali zaidi katika anga za mbali zaidi ya pale a,bapo binadamu wamewahi kufika si tu kuhusu hatua hiyo ya kihistoria, bali pia kuhusu mustakabali ambao zamani ulionekana hauwezekani.

Uwakilishi una umuhimu

Leo, akiwa Meneja wa Mpango wa Uchambuzi wa Hatari za Migongano Angani (CARA) katika programu katika kituo cha NASA kinachofahamika kwa jina NASA Goddard Space Flight Center, anasaidia kuhakikisha satelaiti hazigongani katika mzunguko wa anga, na hivyo kuchangia usalama na uendelevu wa misheni za anga.
© NASA/Brandon Hancock Alinda Mashiku, mhandisi wa angani wa NASA na mwanasayansi aliyefanikiwa, wakati wa Uwasilishaji wa Kiufundi.

Alinda anasema safari yake inaonesha kuwa vipaji na uwezo wa kiakili havina mipaka ya kijiografia. Anasisitiza kuwa utambulisho wake si kikwazo bali ni nyenzo, unaoleta mtazamo na thamani katika maeneo ambako wanawake bado hawajawakilishwa vya kutosha. Anaona kazi yake  na mwonekano wa wanawake kama Christina Koch kama sehemu ya mabadiliko mapana kuhusu nani ana haki ya kuota ndoto, na nani anaweza kuwa sehemu ya STEM yaani Sayansi, Teknolojia na Hisabati.

Kutoka ndoto za utotoni hadi NASA

Akiwa anakua nchini Tanzania, aliota kuwa mwanaanga, hata wakati ndoto hiyo ilipoonekana mbali na uhalisia. Hata hivyo wazazi wake waliilea ndoto hiyo. Baba yake alimpa mazoezi mengi ya hisabati; mama yake, mwalimu, alijenga imani ya kile kinachowezekana.

“Kwa sababu wao waliniamini, nami nilijiamini,” anaiambia Idhaa ya Umoja wa Mataifa. Msingi huo ulimpeleka kusomea uhandisi wa anga, kupata shahada ya uzamivu na hatimaye kuchangia baadhi ya misheni tata zaidi duniani. Simulizi ya Maisha yake anasema, ni ushahidi kwamba ndoto ya mtoto haipaswi kuzimwa kwa sababu njia ya kuifikia bado haijaonekana.

 “Mafuta ya roketi”

© NASA/Brandon Hancock Wanaanga wanne wakiwa kwenye chombo cha angani cha NASA cha Orion, wakiwa juu ya roketi ya SLS (Space Launch System), watazinduliwa kwenye ndege ya majaribio ya shirika la Artemis II, Jumatano, Aprili 1, kutoka Launch Complex 39B katika Kituo cha Anga cha NASA cha Kennedy huko Florida.

Kwa wasichana wanaokabiliwa na vikwazo, Dkt. Mashiku anatumia mfano wa roketi: tafuta “mafuta yako ya roketi.” Kama roketi inavyopaswa kushinda nguvu ya uvutano wa dunia ili kuondoka duniani, watu wanaweza kushinda vikwazo kupitia maarifa, uvumilivu na ubunifu.

“Watu hawakuitazama nguvu ya uvutano wa Dunia na kusema hatuwezi kwenda. Waliuliza, tunawezaje kwenda?” aanasema Dkt. Alinda. Ni somo analoamini linahusu elimu na fursa kama linavyohusu safari za anga. “Changamoto, hazipaswi kuonekana kama ukuta, bali kama matatizo yanayohitaji suluhisho.” Anasisitiza.

Kujenga njia kwa wasichana katika STEM

Dkt. Mashiku anasema kuwahamasisha wasichana pekee haitoshi; njia za kufika huko pia lazima ziwepo. Kupitia mpango wake wa ExcelliSpace, anatoa ushauri kwa wanafunzi wanaotafuta fursa katika sayansi na uhandisi, hasa kutoka jamii zisizo na huduma za kutosha.

Ushauri wake kwa wasichana Afrika na kwingineko ni kutosubiri fursa zikufuate, bali kuzitafuta  tafuta taarifa, uliza maswali, tafuta walezi na chora njia yako. “Milango itafunguka,” anasema na kuongeza msisitizo kwamba, “fursa hujitokeza unapofanya kazi.”

Urithi zaidi ya uhandisi

© NASA/Chris Williams Mtazamo huu kutoka kwenye dirisha la darubini ya Kituo cha Kimataifa cha Anga unaonyesha mkono wa roboti wa Canadarm2 wenye urefu wa futi 57.7 uliounganishwa na kifaa cha kushikilia nguvu na data kwenye moduli ya Harmony.

Katika wakati ambapo dunia inashuhudia kurejea kwa safari za kwenda kwenye Mwezi, Dkt. Mashiku anaiambia Idhaa ya Umoja wa Mataifa kuwa anatumaini urithi wa kudumu au alama ya kudumu itakwenda mbali zaidi ya mafanikio ya kihandisi. Anazungumzia matumaini, umoja na ubunifu wa binadamu  na kuwaonesha wasichana, hasa wa Kiafrika na wenye asili ya Afrika, kwamba wanaweza kuwa maabara, katika uelekezaji wa misheni, darasani, na labda siku moja ndani ya vyombo vya anga vyenyewe.

Kwa pamoja, hatua ya wazi ya Christina Koch na mchango wa wanawake kama Alinda Mashiku nyuma ya pazia vinaonesha ukweli mpana zaidi: wanawake wanaunda mustakabali wa uchunguzi wa anga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *